Unakijua kinachoitafuna Chelsea? Kiko ndani yake

Muktasari:

  • Ndio, hii ni stori ya muda mrefu kuwa Conte ataondoka darajani baada ya msimu huu na kama kutakuwa na mchezo rasmi wa kimashindano atakaoushuhudia kama kocha basi ni fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester United, Mei 19 mwaka huu.

CHELSEA FC imemaliza msimu wa 2017/18 kwa aibu ya aina yake baada ya kukubali kipigo kichungu cha mabao 3-0 kutoka kwa Newcastle United. Kipigo hiki kinakuja katika mchezo unaosemekana kuwa wa mwisho kwa Kocha Antonio Conte.

Ndio, hii ni stori ya muda mrefu kuwa Conte ataondoka darajani baada ya msimu huu na kama kutakuwa na mchezo rasmi wa kimashindano atakaoushuhudia kama kocha basi ni fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester United, Mei 19 mwaka huu.

Kuondoka kwa Conte ni mazao ya matokeo mabovu kwa Chelsea msimu huu ambao iliuanza ikiwa mabingwa watetezi. Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Chelsea kuuanza msimu kama mabingwa watetezi na kuumaliza kwa aibu iliyogharimu kibarua cha kocha.

Katika miaka takribani 15 ya Roman Abramovich klabuni Chelsea, makocha zaidi ya 10 wameingia na kutoka kwenye viunga vya Cobham.

Claudio Ranieri (2003-04), Jose Mourinho (2004-07), Avram Grant (2007-08), Luiz Felipe Scolari (2008-09), Guus Hiddink (2009), Carlo Ancelotti (2009-11), Andre Villas- Boas (2011-12), Roberto Di Matteo (2012), Rafael Benitez (2012-13), Jose Mourinho (2013-15), Guus Hiddink (2015-16), Antonio Conte (2016-18).

Makocha hawa wameisaidia Chelsea kushinda mataji 14 na kuifanya kufanikiwa zaidi England. Ligi Kuu mara tano, Kombe la FA mara nne, Carabao mara tatu, Ligi ya Mabingwa mara moja, Europa League mara moja. Hapo ni bila kuhesabu Ngao za Jamii.

Msimu wa 2014/15, Chelsea chini ya Mourinho, ilibeba ndoo ya EPL lakini katika kuitetea msimu uliofuata, mambo hayakwenda vizuri na Mourinho akaondoka. Akaja Conte akafanya balaa lake na ndiyo kamaliza msimu kwa aibu, tatizo ni nini? Mzee wa Upupu nakupitisha mitaa ya NW6 London ilipo kablu hiyo na kukuchabulia The Blues inapofeli.

Tatizo kubwa la Chelsea ni muundo wa uongozi. Ukimtoa mmiliki Roman Abramovich, muundo wa utawala wa Chelsea unaanzia kwa bodi ya wakurugenzi, menejimenti, mtendaji mkuu, kurugenzi ya ufundi na mwisho ni kocha mkuu.

1. BODI YA WAKURUGENZI YA CHELSEA

Bodi ya wakurugenzi inasimama badala ya mmiliki kwa sababu kiutawala yeye haingii moja kwa moja kwenye uendeshaji wa timu, kwa hiyo hiki ni chombo kinachosimama kama mmiliki wa klabu. Ni chombo kinachofanya kazi kwa niaba ya Roman Abramovich katika kuangalia maendeleo ya klabu. Chombo hiki kinaundwa na Mwenyekiti Bruce Buck, Katibu David Barnard na Wajumbe Eugene Tenenbaum na Marina Granovskaia.

2. MENEJIMENTI

Hiki ni chombo kinachosimamia uendeshaji wa timu kwa niaba ya bodi ya wakurugenzi. Kinaundwa na Mtendaji Mkuu, Mkurugenzi wa Ufundi, Mkurugenzi Mwendeshaji na kocha mkuu. Kiutendaji, menejimenti huwa inawajibika kwa Bodi ya Wakurugenzi, hivyo Mtendaji Mkuu Marina Granovskaia na Kocha Mkuu, Antonio Conte, mamlaka yao ya uteuzi na utenguzi ni bodi.

Sasa tuanze na nafasi ya Mtendaji Mkuu. Tangu Abramovich alipochukua timu 2003, Chelsea imekuwa na Peter Kenyon kama Mtendaji Mkuu tangu 2004 hadi 2009. Baada ya Kenyon, akapokea Ron Gourlay aliyedumu hadi 2014. Baada ya Ron Gourlay kuondoka, Chelsea haikuwa na Mtendaji Mkuu hadi Januari 2018 ilipomuajiri Guy Lawrence, ambaye alianza kazi Februari.

Kwa miaka mitatu, menejimenti ya Chelsea haikuwa na Mtendaji Mkuu, badala yake Mkurugenzi Mwendeshaji Marina Granovskaia au Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi Bruce Buck ndio walikuwa wakikaiumu. Hili ni tatizo namba moja ambalo nitalieleza mbele.

3. MKURUGENZI WA UFUNDI

Tangu Michael Emenalo alipoondoka mwanzoni mwa msimu huu, klabu haijapata mbadala wake. Nafasi hiyo kwa sasa, inakaimiwa na Marina Granovskaia (De facto technical director). Hapa kuna tatizo namba mbili ambalo nitalieleza mbele.

4. WAJUMBE WA BODI YA WAKURUGENZI

Bwana Eugene Tenenbaum (Mkurugenzi wa Bodi), anajulikana kama rafiki wa karibu wa Roman Abramovich. Bi Marina Granovaskaia anaingia kwenye bodi ya wakurugenzi kama mwakilishi wa Roman Abramovich (proxy director) na kwa maana hiyo ana nguvu za kufanya maamuzi ambayo Abramovich angeyafanya kwenye bodi. Hili ni tatizo namba tatu.

Matatizo na maana yake

Menejimenti inapofanya wajibu wake (na makosa yakiwemo), bodi ndiyo mamlaka yake ya uwajibishaji. Kama Kocha Mkuu Antonio Conte ana makosa, bodi ndiyo inamuwajibisha. Na hii ni kwa Marina Granovskaia pia, kama sehemu ya menejimenti, anapaswa kuwajibishwa na Bodi.

Lakini tofauti na Kocha Conte, Marina anaingia kwenye bodi, na akiwa kwenye bodi ana mamlaka zaidi ya mwenyekiti wa bodi (tukumbuke anavaa mamlaka ya mmiliki ).

Kwa hiyo kwa kifupi.....bodi haina sauti juu ya Marina. Anaweza kufanya lolote kwenye utendaji (kununua au kutonunua mapendekezo ya Conte) na hatawajibishwa, labda personally na RA.

Mgongano wa utendaji ni mwingi sana pale Marina anapovaaa kofia ya mkurugenzi wa kawaida, na wakati huohuo anakaimu nafasi ya mtendaji mkuu na wakati huohuo anakaimu nafasi ya mkurugenzi wa ufundi.

Kwa lugha rahisi, Marina ana mamlaka yote ya kuidhinisha mambo. Anapokea mahitaji kutoka kwa kocha, anayatengeneza kama Mkurugenzi wa Ufundi na anapata ridhaa kutoka kwa Mtendaji Mkuu (ambaye ni yeye mwenyewe) na kwenda kununua (kama mkurugenzi anayehusika na mikataba ya wachezaji).

Maamuzi yake yanapotakiwa kuhojiwa na bodi, na yeye anakuwepo ndani kama mwakilishi wa mwenye timu. Kuna uwajibikaji kwenye muundo huu? Kweli kuna mwenyekiti wa bodi mwenye meno kwenye muundo huu?

Hapo ndipo shida ya Chelsea inapoanzia na kumalizikia, na makocha watashindwa sana kumudu mfumo huu kutokana na kubanwa kila kona na kukosa sauti kufanya maamuzi.