Tutazame sura nyingine ya Azam FC

Friday February 8 2019

 

By CHARLES ABEL

Kuna kitu fulani tunakikosea kuhusu Azam FC na tunashindwa kuwatendea haki.

Tumekuwa tukitazama zaidi upande wa kufeli kwao lakini tunasahau upande wao wa pili ambao ni mafanikio na mchango wao kwa soka la Tanzania.

Azam FC imekuwa ikitazamwa kwa sura nyingi hasi wakati huohuo tunashindwa kuiangalia kwa mtazamo chanya.

Kwa wale mashabiki na wanazi wa timu zetu zile mbili kongwe pale Kariakoo, wanaitazama Azam FC kama adui yao ambaye anataka kumaliza ufalme wao.

Wanaichukia kweli Azam na kama wangekuwa na mamlaka pengine wangeweza hata kuishusha daraja ili wapunguze presha ambayo inawapa kwenye Ligi Kuu na mashindano mengine tangu ilipopanda mwaka 2008.

Siku zote Simba na Yanga huwa hawataki kuona timu nyingine inawasumbua kwenye ligi au mashindano mbalimbali wanayoshiriki kama wanavyofanya Azam FC.

Kifupi hizi timu mbili zinaamini zenyewe ndio zina haki ya kushinda kila taji hapa Tanzania jambo ambalo kisoka sio sahihi.

Lakini, kuna wale wanaoitazama Azam FC kama timu inayopoteza fedha tu za familia ya mfanyabiashara tajiri, Said Salim Bakhresa.

Wanaamini mafanikio ambayo Azam FC imeyapata kwa kipindi cha miaka yake 11 ya ushiriki kwenye Ligi Kuu hayaendani na uwekezaji wa fedha ambao umefanywa ndani ya timu hiyo inayoendeshwa kwa mfumo wa kikampuni.

Ikumbukwe katika miaka 11 ambayo Azam wamecheza Ligi Kuu, wamefanikiwa kutwaa ubingwa mara moja, huku wakitwaa ubingwa wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.

Pengine wakati tunaitazama Azam kwa sura isiyo nzuri ni vyema pia tukaigeuza shilingi upande wa pili na kutambua faida za uwepo wa timu hiyo na mchango wake kwa soka la Tanzania.

Ni Azam FC ambayo imeleta mageuzi ya kiuchumi kwa wachezaji wa Kitanzania kwa kulipa kiwango kikubwa cha mishahara tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Mageuzi hayo ya kiuchumi kwa wachezaji ambayo Azam FC imeyaleta yamezilazimisha klabu nyingine kupandisha pia viwango vya mishahara kwa nyota wao badala ya kuwapa fedha kiduchu kama ilivyokuwa zamani.

Ni Azam FC ambayo imefanya uwekezaji mkubwa kule Chamazi kwa kujenga Uwanja na kituo cha kisasa cha soka jambo ambalo sio tu linatoa fursa kwa vijana wa Kitanzania kuonyesha na kuendeleza vipaji vyao bali pia limeimarisha uchumi wa wakazi wa Mbagala na kuongeza thamani ya mtaa wa Chamazi na Mbande.

Ni Azam ambayo ndani ya muda mfupi tumeshuhudia ikiandaa vijana na kuwapeleka nje ya nchi pasipo hiyana kujaribu bahati yao ya kucheza soka la kulipwa pasipo kujishauri pindi wanapopata nafasi.

Ndani ya uwanja, Azam FC imejaribu kuondoa ule wimbo wa Usimba na Uyanga ulioimbwa kwa muda mrefu ambao uliambatana na ufalme wa timu hizo mbili kongwe kwenye soka la Tanzania.

Kiufupi Azam FC imesimama katikati ya Yanga na Simba hivyo imezifanya ziingie katika ulimwengu wa soka la kisasa kwa kufanya usajili bora na kutoa huduma stahiki kwa timu ili zipate nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa kwani vinginevyo nafasi mojawapo inaweza kuchukuliwa na Azam FC tofauti na miaka ya nyuma na hazikuwa na timu imara ya kuwapa changamoto.

Wakati mwingine hatupaswi kuishambulia sana Azam FC kwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu mara moja katika kipindi cha miaka 11 ya ushiriki wake kwa sababu kwa sayansi ya soka huo ni muda mfupi ambao hautoshi kuwafanya wawe na mafanikio ya ndani ya uwanja yanayowafanya wawe sawa na waliowatangulia.

Falsafa hii wazungu wamekuwa wakipendelea kutumia msemi wa Roma haikujengwa ndani ya siku moja.

Kuna mengi mazuri ambayo yamefanywa na yanaendelea kufanywa na Azam FC.

Tukiyatazama kwa jicho na mtazamo chanya, yanaweza kusaidia soka letu lipige hatua kwa namna moja au nyingine na kupandicha Tanzania chati.