Tushike vizuri majina ya vijana hawa

KABLA hata Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U-17) zinazofanyika hapa nchini hazijaanza, tayari baadhi ya nchi shiriki zilikuwa na nyota wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi zao.

Inashangaza kidogo kuona nyota mwenye umri chini ya miaka 17 anarudi Afrika kuchezea timu yake ya taifa ya vijana akitokea Ulaya anakocheza kwenye moja ya klabu za huko tofauti na utamaduni uliozoeleka ule wa kuona wachezaji wa timu ya taifa ya wakubwa wakifanya hivyo tu.

Mfano kwenye kikosi cha Morocco kuna Yacine Kechta anayecheza nafasi ya kiungo, huyu ametokea kwenye klabu ya Le Havre inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Ufaransa na kwenye safu yake ya ulinzi kuna kidume kimoja kinaitwa, Saad Bahir ambaye yuko Orleans ya Ufaransa.

Ukiondoa hao kuna kiungo, Haitam Abaida anayecheza Malaga ya Hispania ambaye anaungana na mshambuliaji Bilal Ouacharaf wanayecheza klabu moja huku pia akiwepo Faissal Boujemaoui wa Genk ya Ubelgiji na Mohammed Asri wa Estac Troyes ya Ufaransa.

Nigeria nao wana Adrian Akande anayecheza Chelsea pamoja na kipa Joseph Oluwabusola ambaye yeye amejumuishwa kikosini akitokea Bournemouth.

Ni wazi wachezaji hawa wapo kwenye klabu salama ambazo zinawalea katika misingi imara ya kuwafanya waje kuwa mastaa wakubwa wa soka siku za usoni.

Lakini, wakati tukiwatazama hao ambao tayari wameshavuka kwenda ng’ambo kucheza soka la kulipwa mapema, tunapaswa pia kuhakikisha tunakalili na kuweka kumbukumbu ya majina ya nyota mbalimbali ambao wamekuja na mataifa yao kushiriki fainali hizo ambazo zinafanyika hapa nyumbani.

Kuna macho ya mawakala na wasaka vipaji ambayo yamekuwa yakiwatazama nyota mbalimbali tangu mwanzoni mwa mashindano hayo ili wawapelekea katika klabu mbalimbali barani Ulaya.

Mawakala na maskauti hao wanaamini kuwa umri chini ya miaka 17 ni sehemu sahihi ya kupata kipaji halisi cha soka ambacho kikiandaliwa vyema kitakuwa staa mkubwa siku za usoni na kitadumu kwa muda mrefu.

Fursa kama hizi ndizo hutumiwa zaidi na mataifa kutoka Afrika Magharibi na Kaskazini na ndio maana yamekuwa yakiwaandaa vyema wachezaji wao ili waweze kujiuza kupitia mashindano ya aina hii.

Kwa bahati mbaya bado Tanzania tunashindwa kuwa na uwekezaji imara wa soka la vijana kwa sababu hatujaona kama tunaweza kupeleka nje wachezaji wetu pindi wanapokuwa na umri mdogo.

Tukiweka kumbukumbu ya wachezaji hawa wanaoshiriki AFCON U17 na baadaye wakafanikiwa kutoka na kutamba kwenye timu mbalimbali barani Ulaya, pengine tutajua thamani ya soka la vijana na kuanza kujifunza jinsi ya kuwekeza kwa vijana wetu.