Tunasubiri miujiza ya Mnguto

Friday December 7 2018

Steven Mnguto  mwenyekiti mpya wa Bodi ya Ligi

Steven Mnguto  mwenyekiti mpya wa Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) 

By CHARLES ABEL

STEVEN Mnguto amechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) hivi karibuni huko Tanga.

Ni jambo lililotarajiwa kwa Mnguto kushinda nafasi hiyo kwa sababu uchaguzi ulifanyika kwa kura za ndio au hapana kutokana na kukosa mpinzani kwenye nafasi hiyo.

Ingekuwa ni sawa na ngamia kupenya kwenye tundu la sindano kwa Mguto kushindwa kwenye uchaguzi huo kwa sababu ni nadra mgombea kupigiwa kura za hapana hasa kwa nchi zetu za Kiafrika.

Haijalishi sana namna ambavyo Mnguto ameshinda kwa sababu amestahili na pia hakukuonekana mtu mwingine mwenye sifa stahiki wa kuwania nafasi hiyo.

Jambo kubwa ambalo linangojewa na wengi ni namna Mnguto atakavyoisimamia Bodi ya Ligi na kuweza kuondoa au kupunguza changamoto nzito ambazo zinaikabili.

Moja ya changamoto hizo ni uhuru wa bodi ya ligi ambapo kwa sasa haina mamlaka makubwa na imekuwa inaendeshwa kwa maelekezo kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Lakini pia kuna suala sugu la ubovu na uchakavu wa viwanja vinavyotumika kwa michezo ya Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili. Bila shaka chini ya Uongozi wake, angalau bodi itajitahidi kuhakikisha eneo la kuchezea la viwanja vyetu linakuwa zuri na salama. Kuna changamoto ya kukosekana kwa wadhamini wa ligi lakini pia hata mapato ya klabu zetu yameshuka kwa sababu ya kuporomoka kwa namba ya mashabiki wanaokwenda kutazama mechi.

Kwa bahati nzuri Mnguto anafahamu machungu ya changamoto hizo kwa sababu anatoka kwenye klabu ambayo haina misuli imara ya kiuchumi kulinganisha na Yanga, Simba au Azam.

Bado kuna changamoto nyingine nyingi kama vile mabadiliko ya mara kwa mara ya ratiba, nidhamu na uadilifu katika uendeshaji wa ligi, bodi kukosa rasilimali watu ya kutosha pamoja na ile ya waamuzi.Kasoro hizo zote zinaweza kutatuliwa na Mnguto iwapo ataamua kuisimamia bodi kwa misingi ya weledi ingawa waliomtangulia walipata wakati mgumu kufanya hivyo.

Ni changamoto ambazo zilikosa tu utayari na nia ya dhati ya kutafuta utatuzi wake na ndio maana leo hii zinaonekana kama zitamfanya Mnguto awe malaika wa heri iwapo uongozi utafanikiwa kuzishughulikia kikamilifu na sio vinginevyo.