Sura ya Simba imeonekana Simba Day

Friday August 10 2018

 

By CHARLES ABEL

SIKU moja kabla ya tamasha la Simba Day juzi, Simba ilivuna zaidi ya Shilingi 100 milioni kutokana na mauzo ya jezi zake mpya ambazo ilizizindua Jumapili iliyopita.

Ndani ya Uwanja wa Taifa unaoingiza jumla ya ya mashabiki 60,000, zaidi ya mashabiki 56,000 walijitokeza kwenye tamasha hilo ambalo lilihitimishwa kwa mchezo wa kirafiki baina ya Simba na Asante Kotoko ya Ghana.

Kwa jicho la tatu, Tamasha la Simba Day mwaka huu limeleta mageuzi makubwa ya kifikra sio tu kwa klabu ya Simba bali pia mchezo wa soka nchini.

Simba ya kibiashara

Kabla ya kutambulisha jezi zake mpya itakazotumia msimu ujao, uongozi wa Simba ulifanya mambo mawili makubwa ambayo yanaleta mwanga wa mafanikio ya kiuchumi kwa timu hiyo msimu ujao.

Kwanza iliingia mkataba wa mwaka mmoja wa udhamini wa jezi na kinywaji cha Mo Energy ambao una thamani ya zaidi ya Sh 250 milioni kwa mwaka.

Hawa ni wadhamini wa ziada ambao wanaungana na wadhamini wakuu wa Simba, kampuni ya ubashiri ya michezo ya SportPesa kwa logo zao kukaa kwenye jezi ya Simba.

Kwa muda mrefu klabu za Tanzania zimekuwa hazijishughulishi kutafuta wadhamini wa ziada kwenye jezi yao na wamekuwa wakiridhika pindi wanapopata mdhamini mmoja tofauti na klabu nyingine za nje ya nchi ambazo jezi zao huchafuka matangazo ya wadhamini.

Kwa hili walilolianzisha Simba, maana yake wanaingia kwenye uwanja wa kuvuna kiasi kikubwa cha fedha kutokana na udhamini wa jezi lakini pia inatoa darasa kwa klabu nyingine kufunguka kifikra.

Kingine ambacho Simba walikifanya ni kuagiza wenyewe jezi zao kisha kuingia ubia na wafanyabiashara katika kuzisambaza na kuziuza jezi hizo.

Hapa inakuwa ni rahisi kwao kupunguza mauzo ya jezi feki kwani wafanyabiashara hao hawatokubali kuona wanakula hasara na badala yake watapambana kuwadhibiti wenzao wanaofanya biashara hiyo haramu.

Hii inatoa ishara kuwa angalau sasa Simba itaanza kunufaika na mauzo ya jezi zake kuliko zamani ambapo haikuwa inapata chochote.

Tamasha limejiuza

Tamasha la Simba Day, 2018 lilikuwa ni la 10 tangu lilipoanzishwa mwaka 2009 na uongozi wa Simba chini ya aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo Hassan Dalali.

Ni tamasha ambalo limekuwa kna mabadiliko makubwa kila mwaka pindi linapofanyika.

Awamu hii, tamasha hilo limejidhihirisha kuwa ni bidhaa hadimu ambayo tayari imeshakuwa utamaduni kwa mashabiki, wapenzi wa Simba pamoja na wadau wa soka nchini.

Kulikuwa na mwitikio mkubwa katika mtiririko wa matukio yaliyofanyika kwa kipindi cha wiki nzima kabla ya tamasha hilo kama vile ufanyaji wa usafi kwenye taasisi za afya, uchangiaji wa damu pamoja na utoaji wa misaada kwenye vituo vya watoto yatima ambayo yalifanywa na mashabiki, viongozi na wachezaji wa Simba.

Vyombo vyote vya habari vililipa uzito tamasha hilo na haikushangaza kuona umati wa zaidi ya mashabiki 56,000 ukijitokeza Uwanja wa Taifa siku ya kilele cha tamasha hilo.

Jiji zima la Dar es Salaam lilitawaliwa na rangi nyekundu kuanzia nyakati za asubuhi hadi tamasha hilo lilipomalizika.

Kuna idadi kubwa ya mashabiki ilitoka mikoani na Visiwani Zanzibar kuja jijini kwa maelfu kushuhudia tamasha hilo.

Kimsingi Simba imefanikiwa kulifanya tamasha hilo kuwa sehemu ya utamaduni wa kudumu kwa mashabiki, wapenzi na wanachama wake jambo ambalo sio baya kama klabu nyingine hata Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) likaiga.

Kikosi kipana kitaibeba

Kama kuna jambo ambalo uongozi wa Simba unapaswa kupewa sifa basi ni usajili wa kundi kubwa la wachezaji wenye kiwango cha juu ambao wanalipa wigo mpana benchi lao la ufundi katika uteuzi wa kikosi cha kwanza.

Nafasi ya mchezaji anayetolewa inaweza kuzibwa vyema na yule anayeingia na kusionyeshe utofauti wowote jambo ambalo litaisaidia wachezaji wa Simba kutopata uchovu wa kucheza mfululizo kwenye msimu ujao.

Hilo lilijidhihirisha kwa mabadiliko ambayo Simba iliyafanya kwa kumtoa James Kotei ambaye nafasi yake ilizibwa vyema na Hassan Dilunga aliyeingia badala yake.

Chama ni Haruna Moshi mpya

Baada ya kusota kwa muda mrefu, hatimaye Simba imempata mrithi sahihi wa pengo la muda mrefu lililoachwa na kiungo mshambuliaji wao wa zamani, Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye ni kiungo Cletus Chama kutoka Zambia.

Chama bana ni maneno mengine. Ana uwezo wa hali ya juu katika kuchezesha timu na kupiga pasi za mwisho na katika kuthibitisha hilo, kwenye mchezo dhidi ya Kotoko juzi, alipiga pasi sita za mwisho kwenda kwa washambuliaji wa timu hiyo ambao walishindwa kuzitumia vizuri.

Aussems ameibadili Simba

Kambi ya wiki mbili nchini Uturuki chini ya kocha Patrick Aussems imeonyesha kuleta mageuzi ndani ya timu hiyo kwani imekuwa ikicheza soka la pasi nyingi na la kufunguka tofauti na lile la kujihami chini ya Mfaransa Pierre Lechantre.

Katika kuthibitisha anahusudu soka la aina hiyo, Aussems ameirudisha Simba kucheza mfumo wa 4-4-2 badala ya ule wa 3-5-2 ambao iliutumia msimu uliopita.

Mpangilio ulienda poa

Changamoto kubwa kwenye matamasha yaliyopita ilikuwa ni mpangilio wa matukio hasa yale ya utambulisho wa wachezaji ambapo upande wa sauti ilikuwa inazidiwa na kelele za mashabiki.

Hata hivyo safari hii ilikuwa kinyume ambapo zoezi la utambulisho kwa viongozi waliofika uwanjani, timu ya wanawake, kikosi cha vijana na timu ya wakubwa ulienda vizuri na sauti ilisikika vyema muda wote.

SportPesa waendelea kuineemesha SimbaKama kuna klabu iliyovuta mkwanja wa kampuni ya ubashiri wa matokeo ya SportPesa basi Simba inaweza kuongoza.

Ukiondoa zaidi ya Sh 900 milion za udhamini, ilipata Dola 10,000 kwa kushika nafasi ya pili kwenye mashindano ya SportPesa Super Cup, ilipewa Sh 100 milioni kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu lakini pia juzi ilikabidhiwa Sh 50 milioni kama zawadi kwa kushika nafasi ya pili kwenye mashindano ya Kombe la Kagame.

Tusubiri ligi ianze tuone.