Simba inavyojiachia Uturuki we acha tu

Muktasari:

  • Mashabiki wa Simba kwa sasa wanatembea kifua mbele. Ndio, wao si ndo mabingwa!

HUWEZI kuizungumzia Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa bila kuitaja Simba. Ni sawa na kuuzungumzia ubingwa wa Ligi Kuu bila kuwafikiria mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara. Mashabiki wa Simba kwa sasa wanatembea kifua mbele. Ndio, wao si ndo mabingwa!

Kwa miaka mingi waliukosa ubingwa wa Ligi Kuu na hivyo kukosa ushiriki wa michuano ya kimataifa, kwa zaidi ya miaka minne ubingwa wa Ligi Kuu ukitawaliwa na mahasimu wao Yanga.

Asikuambie mtu, Simba iliteseka. Si mashabiki, si wanachama, si wachezaji na hata viongozi walikuwa wakikesha kuomba siku moja mambo yabadilike. Miaka minne si kidogo. Hatimaye dua zao zilifika na kujibiwa na sasa wanakenua. Ubingwa wanao. Furaha ikarudi Msimbazi.

Achana na ubingwa, msimu uliopita ulikuwa wa neema kubwa kwa Simba. Hawakuwahi kulia njaa kwa kukosa mishahara, hawakukosa posho zao na kambi, vyote hivyo walivipata.

Kama hujui tu, Simba kwa sasa haipo nchini. Ukipita mitaa ya Msimbazi pale Kariakoo kwa sasa utaona tu jengo lao na watu wachache ambao hawakusafiri na timu. Lakini kuanzia benchi la ufundi, wachezaji na baadhi ya viongozi wameenda Uturuki kwa ajili ya kambi. Unaambiwa si kambi ya kitoto.

Si unajua Simba imerudi kimataifa na inaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika, pia itashiriki Ligi Kuu kama bingwa mtetezi itakayoanza Agosti 22, kuna michuano ya Kombe la FA na mingine, sasa kwa hiyo kambi yao ukijumlisha na usajili wa maana ulioufanyika, wapinzani wajipange tu.

Kambi yao

Maandalizi ya huko Uturuki si ya kitoto, kwani wamefikia katika hoteli ya The Green Park Artepe Resort & Spa ambayo ipo katika ya Mji wa Istanbul. Ukiwa huko, unaona utofauti mkubwa na hapa nchini, mazingira ni tofauti hasa kwa hoteli. Wakiwa hapa nchini walikuwa wakiitumia hoteli ya Sea Scape kuweka kambi yao.

Simba iliondoka alfajiri ya Jumatatu na kikosi cha wachezaji 24, pamoja na benchi la ufundi likiongozwa na Kocha Mkuu, Patrick Asseums, Kocha Msaidizi, Masoud Djuma, Adel Zrane, Mwarami Mohammed, Dk Yassin Gembe, Meneja Richard Robart na Mtunza Vifaa, Hamisi Mtambo pamoja na viongozi saba.

Hata hivyo, kuna baadhi ya wachezaji hawakuweza kuondoka siku hiyo ambao ni Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni, Meddie Kagere na Said Ndemla nao kama wataungana na wenzao huko Uturuki wataongeza idadi ya wachezaji.

GHARAMA ZA CHAKULA KWA SIKU

Iko hivi. Katika hoteli hiyo, ili ule na kulala hapo itakubidi uwe na Dola 116 za Kimarekani ambazo ni sawa na Sh263,643 za Tanzania. Hapo ni kwa mtu mmoja tu.

Fedha hiyo kwa mujibu wa mkataba wa hoteli hujumuisha na milo miwili tu kwa siku japo imezoeleka kuwa milo ni mitatu kwa siku. Kwa maana hiyo, hotelini hapo kama utata mlo wa tatu, itabidi utoe hela nyingine. mbali ya ile ya upangaji.

Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu baada ya uongozi wa Simba kuona hayo, wakaingia mkataba na kampuni ya F12 Sports ambayo itakuwa inashughulikia mambo yote ya chakula kwa siku zote ambazo watakuwa nchini humo.

Kwa maana hiyo, wachezaji wa Simba watakuwa wakihudumiwa chakula na kampuni hiyo kwa milo yote mitatu, huku miwili ikiwa katika mkataba wa upangaji na mmoja ni wa malipo ya nyongeza yaliyofanywa na viongozi wa Simba kwa kampuni hiyo.

GHARAMA YA WOTE

Jumla ya wachezaji wa Simba walio katika msafara huo mpaka sasa ni 24. Ukizidisha Dola 116 kwa wachezaji hao ni sawa na Dola 2,784.

Hiyo ni sawa na Sh6,327,430 za Kitanzania ikiwa ni kwa siku moja tu wachezaji wa Simba hutumia kwa kula na kulala kwenye hoteli hiyo ya kifahari.

GHARAMA KWA JUMLA

Simba iliondoka alfajiri ya Jumatatu na inatarajia kurejea nchini Agosti 5.

Hizo ni sawa na siku 14 yaani wiki mbili kamili watakazokaa Uturuki wakijifua kwa ajili ya kazi ya msimu ujao.

Gharama hizo za siku moja Sh6,327,430 ukizidisha kwa siku zote 14, ni sawa na Sh88,584,020. Sio pesa kidogo.

Simba wanakula bata bwana huko Uturuki.