Schalke 04 hii, Guardiola angeisoma namba

Muktasari:

  • Timu  ya Manchester City iliifunga timu ya FC Schalke 04  mabao 3-2 kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya mtoano ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya huko Ujerumani.

MUNICH, UJERUMANI. MANCHESTER City ilihitaji kufunga mara mbili katika dakika tano za mwisho kushinda ugenini kwa FC Schalke 04 kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya mtoano ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya huko Ujerumani. Katika mechi hiyo, Man City ilishinda 3-2.

Kikosi hicho cha Kocha Pep Guardiola kilitangulia kwa bao la Sergio Aguero, lakini FC Schalke ikaja kupata penalti mbili, zilizofungwa na Nabil Bentaleb kabla ya Man City kujikuta ikicheza pungufu kutokana na Nicolas Otamendi kutolewa kwa kadi nyekundu. Hata hivyo, hilo halikuwatia unyonge Man City, hivyo ikafunga mara mbili katika dakika tano za mwisho kupitia kwa Leroy Sane na Raheem Sterling kushinda mechi.

Man City ilionekana kama inakuwa na kazi nyepesi uwanjani, lakini mambo yasingekuwa hivyo kama FC Schalke 04 ingeendelea kubaki na kikosi chake kilichokuwa na mastaa wa maana watupu kabla ya kuwapiga bei. Cheki FC Schalke hii ilivyokuwa, nani angechomoka?

Kipa: Manuel Neuer

Anacheza: Bayern

Munich

Mechi Schalke: 156

Manuel Neuer alijiunga na Schalke kipindi hicho akiwa na umri wa miaka mitano tu na kubaki hadi karibu miaka 20. Kipa huyo alikuwa mmoja kati ya makinda wenye mafanikio zaidi waliobuliwa kwenye klabu hiyo kwani amekuja kuwa kipa bora kabisa duniani kwa sasa.

Baada ya kushinda ubingwa wa Kombe la Ujerumani akiwa na Schalke katika msimu wa 2010/11, alikwenda kujiunga na Bayern Munich. Ameondoka Schalke baada ya kucheza karibu mechi 200 na kujiunga na Bayern alikoshinda mataji sita ya Bundesliga, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Dunia la Fifa mwaka 2014. Ni bonge la kipa.

Beki wa kulia: Rafinha

Anacheza: Bayern Munich

Mechi Schalke: 153

Baada ya kuanzia kucheza soka huko kwao Brazil, Rafinha alionwa na skauti wa Schalke wakati alipokuwa kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la Vijana mwaka 2005. Kiwango chake kilizivutia klabu za Ulaya kibao, lakini alikwenda kujiunga na wababe hao wa Ujerumani mwaka 2005.

Alicheza kwenye kikosi cha Schalke zaidi ya mechi 153 kabla ya kujijenga na kuwa beki mahiri kabisa kabla ya kwenda kujiunga na Genoa mwaka 2010. Kiwango chake bora huko Serie A kilimpa dili la kwenda kujiunga na Bayern Munich anakocheza hadi sasa.

Beki wa kushoto:

Sead Kolasinac

Anacheza: Arsenal

Mechi Schalke: 123

Beki Sead Kolasinac alikuwa kama mtalii kipindi anaanza soka kutokana na kupita kwenye timu nyingi, Kalsruher, Hoffenheim na Stuttgart kabla ya kwenda kutulia Schalke. Uwezo wake wa kucheza beki wa kati na hata kiungo, ulimfanya Kolasinac kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Schalke na hapo alijivutia mashabiki wengi na timu kibao kumtaka. Alinaswa na Arsenal kwa uhamisho wa bure mwaka 2017 huku akitajwa kwenye kikosi bora cha msimu kwenye Bundesliga.

Beki wa kati:

Joel Matip

Anacheza: Liverpool

Mechi Schalke: 194

Beki huyo Mcamerooni aliibukia kwenye timu ya watoto ya Schalke kabla ya kuanza kutumika kwenye kikosi cha wakubwa na kucheza kila dakika kwenye Bundesliga katika msimu wa 2015/16. Licha ya kuwa na thamani kubwa kwenye klabu hiyo, Matip aliamua kukatisha mkataba wake na kwenda kujiunga na Liverpool baada ya Kocha Jurgen Klopp kuonekana kumhitaji zaidi katika usajili wa dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2016.

Beki wa kati: Benedikt Howedes

Anacheza: Lokomotiv Moscow

Mechi

Schalke: 335

Benedikt Howedes alijiunga na Schalke akiwa na miaka 13, akakuwa na kuanza kuichezea timu hiyo kwenye kikosi cha kwanza akiwa na miaka 19 mwaka 2007. Howedes alijijenga na kuwa moyo wa safu ya mabeki ya Schalke, akicheza kati na wakati mwingine kushoto. Kiwango chake kilimfanya ajumuishwe kwenye kikosi cha Ujerumani kilichobeba ubingwa wa dunia mwaka 2014 huko Brazil.

Howedes kwa sasa anaichezea Lokomotiv Moscow ambako alisaini mkataba wa miaka minne baada ya kuachana na Schalke mwaka jana.

Kiungo wa kati:

Leon Goretzka

Anacheza: Bayern

Munich

Mechi Schalke: 147

Katikati ya msimu uliopita, Bayern Munich ilithibitisha kumnasa kiungo Leon Goretzka mwishoni mwa msimu kwa kuwa mkataba wake ulikuwa unafika mwisho huko Schalke. Klabu nyingi sana zilihitaji huduma ya Mjerumani huyo, ikiwamo Barcelona, lakini Goretzka alishawishika na Bayern Munich na kwenda kujiunga na timu hiyo msimu ulipomalizika. Mambo yake mazuri huko Bayern, akifunga mabao sita katika mechi 19 alizocheza kwenye Bundesliga msimu huu.

Kiungo wa kati: Ivan Rakitic

Anacheza: Barcelona

Mechi Schalke: 135

Kiungo Ivan Rakitic naye alinaswa na skauti wa Schalke licha ya kuwapo na kundi kubwa la klabu zilizokuwa zikihitaji huduma yake. Baada ya kucheza mechi kadhaa kwenye ubora wake, kipindi hicho akiwa na FC Basel ya Uswisi, Schalke ilikwenda kumsajili mwaka 2007.

Rakitic alikwenda kuonyesha kiwango bora kabisa akicheza kiungo wa goli kwa goli na kufanikiwa kufunga mabao 16 na kuasisti 29 katika mechi 135 alizocheza hapo. Ubora wake uliwafanya Sevilla waende kumsajili na muda si mrefu akaenda kujiunga na Barcelona anakocheza hadi sasa.

Kiungo wa kulia:

Julian Draxler

Anacheza: PSG

Mechi Schalke: 119

Moja kati ya zao bora kabisa la kutoka kwenye akademia ya Schalke ni Julian Draxler, ambaye alisajiliwa na timu hiyo kipindi hicho akiwa na umri wa miaka minane tu na kuanza kutikisa dunia mwaka 2011. Kiungo huyo mbunifu uwanjani alionyesha kiwango bora kabisa katika mechi kibao alizocheza kwenye timu hiyo na kujitengenezea jina kubwa.

Timu nyingi zilihitaji saini yake ikiwamo Borussia Dortmund na klabu za England, lakini cha kushangaza alikwenda kujiunga na Wolfsburg mwaka 2015 kabla ya kuamua kujiunga na PSG anakocheza hadi sasa.

Kiungo wa kushoto:

Leroy Sane

Anacheza: Man City

Mechi Schalke: 57

Leroy Sane bado kinda kabisa, lakini hadi anaondoka kwenye kikosi cha Schalke alicheza mechi 57. Usiku wa juzi, Sane aliifunga timu yake ya zamani kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya 16 bora katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Sane ni zao jingine la kutoka kwenye akademia ya Schalke, alipoibukia sambamba na Max Meyer na Geis.

Mwaka 2016 alikwenda kujiunga na Manchester City, anakotamba hadi sasa akiwa mmoja wa wachezaji makinda wenye vipaji vikubwa sana huko kwenye soka la Ulaya.

Kiungo mshambuliaji: Mesut Ozil

Anacheza: Arsenal

Mechi Schalke: 39

Ozil alikwenda kujiunga na akademia ya Schalke mwaka 2005 na mwaka mmoja baadaye akaanza kupata namba kwenye kikosi cha wakubwa.

Kiungo huyo mshambuliaji alidumu kwenye timu hiyo kwa miaka miwili tu kabla ya kutibuana na uongozi wa Schalke na kuhamia zake Werder Bremen. Kwenye kikosi cha Schalke, Ozil alipiga asisti tano katika mechi 39 na hakuna ubishi, klabu hiyo ilijutia kumwaacha aondoke kirahisi akienda kupita Real Madrid kabla ya kujiunga na Arsenal aliko hadi sasa.

Straika: Klaas-

Jan Huntelaar

Anacheza: Ajax

Mechi Schalke: 240

Mshambuliaji wa kati wa ukweli, Klaas-Jan Huntelaar. Kazi yake yeye ni kufunga tu mabao. Straika huyo wa Kidachi alijiunga na Schalke mwaka 2010 baada ya kucheza kwa miaka michache huko Real Madrid na AC Milan. Kwenye kikosi hicho cha Wajerumani alijitengeneza vyema na kusahau kabisa kuchemsha kwake huko Bernabeu na kurudi kwenye ubora wake kama ilivyokuwa zamani alipokuwa katika kikosi cha Ajax.

Alicheza mechi zaidi ya 200 kwenye kikosi cha Schalke na kufunga mabao 126 kabla ya kurudi kwenye klabu yake ya zamani ya Ajax mwaka 2017.