Sarri lazima asajili fowadi, la itakula kwake

VITA ni vita. Kwenye Ligi Kuu England kuna vita nyingi. Januari imeshafika, kuna wanaosaka ubingwa, kuna wanaotaka tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, kuna wa Europa League na kuwa wanaotaka kubaki kwenye ligi.

Kipindi hiki ni muhimu kwa kila timu kutazama udhaifu kwenye kikosi chao na kuufanyia marekebisho. Usajili upo wazi.

Man United watajitazama zaidi kwenye safu yao ya mabeki. Wanahitaji mtu huko kuweka mambo sawa. Arsenal wanahitaji mabeki pia. Lakini, shida kubwa ipo huko Chelsea.

Kocha Maurizio Sarri anahitaji nguvu mpya kwenye safu yake ya ushambuliaji.

Kwa sasa timu hiyo inaonekana kumtwisha mzigo mkubwa Eden Hazard, kitu ambacho kinamfanya anashindwa wakati mwingine kuiongoza timu hiyo kufanya vyema.

Sarri anahitaji kufanya marekebisho kwenye safu yake ya ushambuliaji, la sivyo jambo hilo litamgharimu kwenye mbio za kuwania tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Msimu huu Chelsea wameshindwa kukamatia tiketi hiyo, hivyo kufeli tena kwa mara ya pili itakuwa pigo kwao. Kwenye fowadi, mchezaji wao bora kabisa ni Hazard.

Lakini, naye anahitaji kuwa na wasaidizi ili kufanya mambo kuwa mepesi. Kwenye mechi dhidi ya Crystal Palace, Chelsea ilionyesha udhaifu mkubwa kwenye safu yake ya ushambuliaji.

Ilihitaji bao la kiungo N’Golo Kante kupata pointi tatu. Lakini, Chelsea wamekuwa wakishinda pia kwa idadi ndogo ya mabao, jambo ambalo linaweza kuja kuwagharimu kama itatokea wameringana pointi na wengine.

Kwenye Top Six, Chelsea ndio waliofunga mabao machache kuliko timu nyingine zote. Wamefunga mabao 38. Wamezidiwa na vigogo wenzao wote. Hilo litawaweka kwenye gharama kubwa kwenye siku za baadaye.

Wakati mwingine kuwa na pointi nyingi ni sawa, lakini unahitaji kuwa na mabao mengi pia, yanaleta mtaji mzuri.

Kulingana pointi ni rahisi, hivyo hilo linapotokea mabao yanakuwa msaada ya kukufanya uwe kwenye sehemu ya juu kwenye msimamo kuliko mpinzani wako. Sasa hilo la kufunga mara nyingi litawatesa Chelsea.

Safu yao kuna mastaa kama Olivier Giroud na Alvaro Morata. Wawili hao wote wamepoteza viatu vyao vya kufungia. Hali inatisha kweli kweli. Ina maana asipofunga Hazard, basi hali inakuwa ngumu zaidi.

Sarri amemfanya Willian kuwa mchezaji wa kawaida. Si tishio tena kwenye kufunga.

Hilo linaleta shida. Hakuna ubishi kwamba Sarri anahitaji kuingia sokoni kwenye dirisha hili la Januari kunasa mshambuliaji atakayekuja kuleta uhai kwenye safu hiyo ili kutengeneza mazingira ya kuipata kirahisi tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Kinyume cha jambo hilo, Chelsea itakula upande wao, Ligi ya Mabingwa Ulaya wataisikia tu kwenye bomba.