Samatta- Gari langu ni shilingi 244 milioni

Tuesday May 21 2019

 

Ubelgiji Genk.

KATIKA mizunguko ndani ya Jiji la Genk, Samatta anazungumza kuhusu gari lake la kifahari aina ya Range Rover ambalo imezua gumzo mitandaoni. Mara kadhaa Samatta amewahi kutupia picha za gari hilo mitandaoni na kuzua gumzo.

Kutokea Mbagala mpaka Genk, asingetegemea siku moja angeendesha gari la kifahari la aina hiyo. Samatta anakiri alinunua gari hilo kwa pesa nyingi ambapo kwa kiasi cha pesa za madafu linafikia thamani ya shilingi 244 milioni.

“Nimenunua Euro 68,000. Nimenunua bila ya mkopo. Kwa Tanzania naweza kulipia kodi kama shilingi 70 milioni hivi. Ni gari zuri na naipenda. Huku unanunua gari ambalo halijatembezwa na mtu mwingine tofauti na Bongo.” anasema Samatta.

Miaka saba iliyopita nilikwenda Lubumbashi Congo wakati huo akimiliki gari aina ya Chrysler ambayo baadaye aliileta nchini inasemekana aliilipia kodi kiasi cha Sh 20 milioni za Tanzania. “Nina mpango wa kuileta Bongo. sijajua lini lakini nimelenga kulileta Dar hapo siku za usoni na nitalitumia kama kawaida tu ingawa lina usukani katika upande wa kushoto tofauti na magari ya nyumbani,” anasema Samatta huku akicheka.

Kwa hesabu za haraka haraka Euro 68,000 ni sawa ni shilingi za Tanzania 174,473,000 na unapopiga hesabu ya kodi shilingi 70 milioni inakupa hesabu ya shilingi 244 milioni. Samatta hashtuki sana kuhusu pesa na wala hataki kukumbukwa sana kuhusu pesa.

Advertisement

Anadai hata sababu ya yeye kujenga msikiti mkubwa katika eneo la Vikindu nje ya Jiji la Dar es Salaam katika eneo la Mkoa wa Pwani inatokana na dhamira yake ya kutaka kukumbukwa kivingine pindi atakapostaafu soka.

Anajishusha chini zaidi ya mastaa wengine wa zamani waliofanya mambo makubwa na kudai wao wataendelea kukumbukwa kwa siku nyingi zijazo huku yeye akikumbukwa kwa baadhi ya mambo aliyofanya katika jamii.

“Mimi ni mtu mdogo kuliko mastaa wengi wakubwa waliopita kina Peter Tino, Zamoyoni Mogella, Leodeger Tenga na wengineo hawa watakumbukwa kama wanasoka mahiri. Mimi natafuta namna yangu ya kukumbukwa. Lakini mimi pia mimi ni Muislamu na hakuna kitu cha kushangaza,” anasema Samatta.

Kuthibitisha hilo Samatta alitarajiwa kuondoka Genk Mei 21, siku mbili baada ya Ligi Kuu ya Ubelgiji kumalizika kuelekea Makka Saudi Arabia kwa ajili ya kufanya ibada ya Umra kama alivyofanya msimu uliopita ambapo aliambatana na staa mwenzake wa zamani wa Genk, Omary Colley ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Sampdoria. Samatta hataki kuzungumzia miradi mbambali binafsi anayoifanya kwa sasa akidai ni maisha yake binafsi.

Namuuliza kama ana mpango gani na wanasoka wa Tanzania, hasa wale makinda ambao wana ndoto ya kufikia alikofika na kung’aa kiasi cha kuhusudiwa na mashabiki wa soka nchini Ubelgiji na nyumbani kwao. Anajibu kwa umakini.

“Nina mpango huo kusema kweli. Natamani sana na nitafanya kitu lakini kwa sasa inabidi nijikite zaidi katika kucheza soka kwa sababu bado nina safari ndefu ya kucheza soka. Unajua hauwezi kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja. Inabidi uchague kitu kimoja.”

“Kwa sasa mimi ni mchezaji zaidi na inabidi nifanye kazi yangu. Watu wengi hawaelewi hili. Siwezi kuwa wakala muda kama huu. siwezi kuwa meneja au kujihusisha na biashara ya wachezaji kwa sasa nitakuwa napoteza mwelekeo lakini muda ukifika nina mpango wa kuwaleta madogo huku,” anasema Samatta.

“Inapowezekana huwa nasaidia tu lakini sio kazi yangu kwa sasa. Kuna mchezaji wetu mmoja wa zamani hapa Genk aliwahi kunipigia simu na kuniuliza kama ninamfahamu Kelvin John ‘Mbappe’. Nikamwambia ni mchezaji mzuri sana. Nadhani wakala wake alikuwa anataka kumchukua. Sijui kimeendelea nini” aliongeza Samatta.

Samatta anazikosoa timu kubwa na ndogo za Tanzania ambazo zinataka pesa nyingi kwa wachezaji pindi wanapotakiwa na klabu mbalimbali nje ya nchi huku akitaka ziache mara moja kujaribu kudai pesa wanayoiona ndefu na badala yake wasubiri pesa kubwa mchezaji akikomaa.

“Huwa nashangaa sana, wakati mwingine timu inamtaka mchezaji wao wanataka pesa nyingi badala ya kuwaruhusu tu waondoke na kuingia mikataba ya kupata pesa nyingi siku za usoni. Kama hawa vijana wetu inabidi waruhusiwe tu kuondoka kwa wingi halafu wakikomaa na kuuzwa kwenda kwingineko ndipo unapata pesa nyingi,” anaongeza Samatta.

Maongezi yetu na yanaendelea zaidi. Kesho katika gazeti hili Samatta ataongea kitu cha kusisimua zaidi. Endelea kufuatilia kwa karibu makala haya ya kusisimua kuhusu ustaa wa nahodha huyu wa Timu ya Taifa ya Tanzania na Genk ya Ubelgiji.