Ronaldo na ujanja wake wote haya yamemshinda

Muktasari:

  • Lakini, mshambuliaji huyo matata kabisa ameondoka kwenye La Liga na kuacha rekodi kadhaa ambazo alishindwa kuzivunja licha ya kudumu kwenye soka la Hispania kwa miaka tisa. Hizi hapa rekodi tano ambazo Ronaldo alishindwa kuzivunja kwenye La Liga kwa muda wote aliokuwa na Real Madrid hadi anaondoka kwenda Juventus.

MADRID, HISPANIA. SUPASTAA, Cristiano Ronaldo amevunja na kuweka rekodi nyingi kwenye mchezo wa soka, achana na La Liga pekee yake. Lakini, hivi karibuni alitua kwenye soka la Italia, Serie A na kuachana na soka la Hispania kwa uzuri tu.

Lakini, mshambuliaji huyo matata kabisa ameondoka kwenye La Liga na kuacha rekodi kadhaa ambazo alishindwa kuzivunja licha ya kudumu kwenye soka la Hispania kwa miaka tisa. Hizi hapa rekodi tano ambazo Ronaldo alishindwa kuzivunja kwenye La Liga kwa muda wote aliokuwa na Real Madrid hadi anaondoka kwenda Juventus.

5.Kucheza mechi nyingi La Liga

Watu walidhani kwamba Ronaldo angetumikia maisha yake yote yaliyobaki kwenye soka katika kikosi cha Real Madrid. Jambo hilo lingemfanya kuingia kwenye orodha ya wachezaji waliocheza mechi nyingi zaidi kwenye La Liga. Lakini, kwa bahati mbaya, Ronaldo ameondoka akiwa hata kwenye 10 bora hayumo. Rekodi ya kucheza mechi nyingi kwenye La Liga inashikiliwa na kipa wa zamani wa Barcelona, Andoni Zubizarreta, aliyecheza mechi 629.

4.Bao la mapema zaidi La Liga

Kwenye La Liga, rekodi ya bao la mapema zaidi, kwa lugha nyingine bao la haraka inashikiliwa na staa wa Mali, Seydou Keita. Kipindi hicho akiwa kwenye kikosi cha Valencia, Keita alifunga bao lake ndani ya sekunde 7 tu baada ya mechi kuanza dhidi ya Almeira. Rekodi hiyo imebaki imara hadi sasa, haijavunjwa licha ya kuwapo na washambuliaji kibao matata kwenye ligi hiyo, akiwa Ronaldo na Messi na wengineo. Hadi Ronaldo anaondoka kwenye La Liga, ameshindwa kuivunja.

3.Hat-Trick tatu mfululizo

Mastaa Messi na Ronaldo wote waliwahi kufunga Hat-Trick kwenye mechi mbili mfululizo mara kadhaa. Lakini, hawajawahi kufunga Hat-Trick kwenye mechi tatu mfululizo jambo ambalo lingewafanya kuvunja rekodi iliyokuwa imewekwa kwenye La Liga. Mchezaji pekee ambaye aliwahi kuandika rekodi hiyo kwenye kitabu cha kihistoria alikuwa staa wa Real Oviedo, Isidro Langara, ambaye alifunga mabao matatu katika mechi tatu mfululizo mwaka 1935.

2.Hat-Trick ya haraka zaidi

Supastaa David Villa si tu kwamba anashikilia rekodi ya kuwa kinara wa mabao kwenye kikosi cha Hispania, bali pia anashikilia rekodi ya kufunga Hat-Trick ya haraka zaidi kwenye historia ya La Liga. Katika msimu wa 2005/06, msimu ambao alikuwa akiitumikia Valencia, Villa alifunga hat-trick ndani ya dakika nne tu na sekunde 47. Ronaldo kuna wakati alitaka kukaribia rekodi hiyo, wakati alipofunga hat-trick yake akitumia dakika nane kwenye mechi dhidi ya Granada mwaka 2015.

1.Kufunga mabao saba katika mechi moja

Kuna wachezaji wawili tu kwenye historia ya La Liga ndiyo waliowahi kuweka rekodi ya kufunga mabao saba katika mechi moja ya ligi hiyo. Mmoja wao alikuwa gwiji wa Barcelona, Laszlo Kubala. Alifanya hivyo mwaka 1952 wakati alipoweka kambani kwenye mechi dhidi ya Sporting Gijon. Ronaldo ameishia kufunga mabao matano tu, akifanya hivyo mara mbili, wakati Messi amewahi kufunga mabao manne kwenye mechi moja.