Pale langoni Simba, kocha atakuwa na mtihani mkubwa

Muktasari:

  • Mijadala hiyo inahusisha pia rekodi na historia zilizoandikwa ikiwa ni pamoja ya wababe waliozoeleka kwa miaka mingi kuonekana kumbe si lolote kutokana na wengi wao kuondolewa mapema kinyume na vile ilivyotarajiwa.

WAKATI dunia ya soka ikianza kupata utulivu kutokana na kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia, mashabiki wengi bado wanaendelea kuyazungumzia matukio mbalimbali yaliyojiri kwenye fainali hizo kule Russia.

Mijadala hiyo inahusisha pia rekodi na historia zilizoandikwa ikiwa ni pamoja ya wababe waliozoeleka kwa miaka mingi kuonekana kumbe si lolote kutokana na wengi wao kuondolewa mapema kinyume na vile ilivyotarajiwa.

Kimsingi tumekubali kwamba hilo ndio soka na maajabu yake. Mambo yaliyotokea Russia yalifurahisha na kuushangaza ulimwengu hasa pale bingwa mtetezi, Ujerumani, alipolazimishwa kufunga mabegi na kurejea kwao bila hata kuingia hatua ya 16 Bora.

Ngoja tusubiri mwaka 2022 huko Qatar tuone nini kitatokea endapo tutajaliwa uhai.

Kama ilivyo ada, ratiba za soka katika mataifa mengi duniani kipindi hiki shughuli kubwa ni kwa mashirikisho ya kuendelea kujipanga kwa ajili ya kuanza msimu mpya au kalenda ya awamu nyingine.

Hii inatokana na ukweli kwamba kwa desturi, mwaka mpya wa soka unaanza mwezi Agosti katika nchi nyingi ingawa kwa mwaka huu na kwa utaratibu ratiba ya fainali za Kombe la Dunia ilikuwa ni sababu iliyosimamisha shughuli za soka kwenye nchi nyingi.

Wakati heka heka kwenye mashirikisho ya soka zikipamba moto kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya msimu unaotarajiwa kuanza, wadau wakubwa wa soka katika nchi ambao ni klabu, nao hawapo nyuma katika harakati hizi.

Klabu kwa sasa zipo bize kupanga na kuratibu kalenda za majukumu yao ili kupigania uhai wao kwenye ligi zinazoshiriki. Nyingi zimeshaanza kazi ya kujiweka tayari kwa maana ya kuanza kambi za maandalizi ya msimu mpya.

Kwa hapa nyumbani Tanzania, hiki ni kipindi chenye vituko na vioja kwa ujumla wake. Yaani kipindi hiki cha usajili huwa tunashuhudia mengi yanayofanywa na klabu zetu.

Ni kipindi ambacho hughubikwa na kupigana vikumbo kwenye viunga mbalimbali kwa watendaji na viongozi waliokabidhiwa dhamana kuziongoza timu kwa ajili ya kutafuta wachezaji walio bora.

Kimsingi ni kipindi kizuri na muhimu kwa wachezaji kutokana na soko lao kuongezeka thamani. Kwa bahati mbaya kwa muda mrefu sasa, kipindi hiki kimeendelea kuwa na changamoto nyingi kwenye timu zetu kutokana na jinsi zoezi zima linavyoendeshwa, lakini hayo tuwaachie wanaohusika wapambane na hali zao.

Msimu huu miongoni mwa usajili uliovuta hisia za watu wengi ni wa Simba, ambao unafanyika pia baada ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, lakini pia ikiwa rasmi imeamua kuanza kuindesha timu hii katika mfumo wa kisasa zaidi wa uwekezaji, tofauti na ilivyokuwa awali.

Kutokana na nguvu ya kiuchumi iliyonayo klabu hiyo sasa, kuna mengi yanaonekana kubadilika ikiwa ni pamoja na kuwasajili wachezaji wengi wanaowataka kwa kigezo cha viwango na ubora. Ni jambo zuri kwa mustakabali wa mafanikio ya klabu, lakini umakini na weledi unahitajika mno.

Kuhakikisha inajenga ukuta imara utakaowapa matokeo chanya, Simba imeamua kuingia msituni na kumtafuta kipa mwingine anayeaminiwa atakuwa msaada mkubwa kwenye michuano yote, Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika hilo imemsajili Didas Munishi ‘Dida’ ili asaidiana majukumu na kipa aliyeisaidia klabu kutwaa ubingwa, Aishi Manula na wenzake wengine wanaocheza nafasi hiyo Msimbazi hapo.

Kwa shabiki yeyote wa soka nchini, hakuna asiyewafahamu Dida na Manula. Wawili hawa kwa pamoja wameweza kuitumikia timu ya taifa, Taifa Stars, na sifa zao kwa kiasi fulani zinalandana kutokana na ukweli kwamba wamewahi kuwa makipa namba moja Stars.

Lakini pia wamezitumikia timu kubwa na kongwe hapa nchini za Simba, Yanga na Azam na kufanikiwa kuzipa mataji.

Tofauti moja ndogo kati yao ukiachilia mbali uwezo wa kiufundi na mbinu zao uwanjani, Dida amepata bahati ya kwenda kucheza soka la kulipwa huko Afrika Kusini na Manula bado hajabahatika kucheza nje ya nchi, ingawa mara kadhaa amepata ofa hiyo lakini hakuamua kwenda huko alikohitajika.

Wakati Dida akisajiliwa katika usajili uliofungwa jana Alhamisi, ametokea Afrika Kusini alikokuwa anacheza soka la kulipwa. Mwenzake Manula amesajiliwa msimu uliopita akitokea Azam.

Kwa ujumla nafasi hiyo imepata watu sahihi licha ya tofauti zao za vipaji, ufundi na mbinu wakiwa langoni. Kiumri Dida ni mkubwa kuliko mwenzake, maumbile yao pia yakionekana tofauti.

Katika hali ya kawaida, inabidi Dida afanye mazoezi zaidi ili kurejesha kasi yake na unyumbulifu aliyokuwa nayo kabla ya kutimkia bondeni, hii itamsaidia kuwa na uwepesi wa kutosha kucheza mipira inayoelekea golini kwake ikiwa mbali na sehemu aliposimama.

Hiki ni kipengele kinachompa sifa na kumfanya Manula kuwa hodari katika kucheza mikwaju ya hatari. Katika kucheza mipira iliyokufa, mara nyingi ufundi wao ni kama unalingana, ingawa tofauti yao kwenye kipengele hiki itategemea kiwango cha maandalizi na mazaoezi ya kila mmoja kwenye mechi husika.

Lakini katika suala la ujasiri, kujiamini na ujanja uliojengeka katika misingi ya mazoezi, utaamua mwenyewe ni nani atakuwa bora zaidi ya mwenzake, kwani katika kuitumikia nafasi hii wote wamedhihirisha uwezo wa kutosha katika kucheza mipira ya kutenga.

Kushuka na kupanda kwa uwezo wa kipa kudaka mipira, kunategemea mno na aina ya washambuliaji anaokutana nao, idara yake ya ulinzi na mbinu anazofundishwa na kocha pamoja na uzoefu binafsi.

Wote hawa ni wazoefu katika michezo mikubwa ya kimataifa wakiwa wameshiriki Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho kupitia klabu zao na ile ya timu za taifa.

Kimsingi ujio wa Dida kikosini Simba umezingatia uzoefu wake alionao katika michezo mikubwa ya kimataifa, lakini pia ligi ya nyumbani.

Bila shaka wakuu wa timu ya simba wamezingatia vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na weledi, uzoefu, ukomavu na kulifahamu vizuri soka la kimataifa.

Wigo mpana wa walinda mlango utawasaidia Wekundu wa Msimbazi kuliwakilisha taifa katika msimu ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo upo uwezekano wa yeyote kati yao akawa chaguo la kwanza kutegemea watakavyojituma.