Ndoa ya Aaron Ramsey ipo salama huko Juventus

ALIKUWA jukwaani Allianz Stadium kuwaona wenzake wakishangilia kubeba taji lao la nane mfululizo kwenye Serie A.

Alikuwa mgeni na pengine Juventus wamefanya makusudi kumtia uchu Aaron Ramsey kabla hajaanza kuitumikia timu hiyo msimu ujao.

Mataji, ndicho kitu alichokuwa akikikosa Ramsey huko Arsenal. Miaka yake yote 11 aliyodumu Emirates, hajawahi kuonja utamu wa ubingwa wa ligi. Lakini, wenzake huko Juventus, wanabeba ubingwa wa ligi kila kukicha.

Ramsey amekuwa akicheza kiungo ya kati yenye kufikiria zaidi kwneye kushambulia. Amekuwa akicheza pia kama namba 10. Hivyo ndivyo yalivyo maisha yake ya uwanjani. Anakuwa kwenye ubora wake anapopanda mbele kwenda kushambulia.

Ramsey ana madhara zaidi anapokuwa kwenye lile eneo la goli la wapinzani. Mjanja sana anapokuwa na mpira kwenye eneo hilo na hata asipokuwa na mpira. Mjuzi pia wa kupiga pasi za mwisho.

Kwa kumlinganisha na viungo waliopo Juventus kwa sasa, Ramsey amewaacha mbali sana linapokuja suala la mchango kwenye kushambulia.

Kwa miaka mitano iliyopita, Ramsey amefunga mabao 23 na kuasisti 28 kwenye ligi.

Viungo wa Juventus, akiwamo Miralem Pjanic, Blaise Matuidi, Emre Can, Rodrigo Bentancur, Federico Bernardeschi na Juan Cuadrado, wote hao hawamuwezi Ramsey. Pjanic peke yake ndiye aliyefunga na kuasisti mara nyingi kuliko Ramsey.

Kutokana na hilo suala la Ramsey kwenda kupata namba katika kikosi cha Juventus hilo halikuwa na utata. Lakini, shida inakuja sehemu moja tu, Max Allegri. Huyu ndiye mshenga wake huko Turin.

Ni jambo lisilofichika kwamba Ramsey lilikuwa chaguo la Allegri wakati ananaswa na Juventus. Kocha huyo aliona kabisa Ramsey anakwenda kufiti bila ya shida kwenye mfumo wake wa 4-4-2 au ule wa 4-3-3. Shida ni kwamba Allegri hatakuwapo kwenye timu hiyo msimu ujao.

Ndoa yake na Juventus imefikia tamati mwishoni mwa msimu huu na kwamba msimu ujao Allianz Stadium kutakuwa na kocha mpya. Ramsey ana uwezo pia wa kucheza namba nane.

Kwenye fomesheni ya 4-4-2 angetumika kwenye winga, wakati ile 4-3-3 anamudu zaidi kucheza kwenye kiungo ya juu au pale kwenye Namba 10. Uzuri wa Ramsey ni kwamba anampa kocha machaguo mengi ya fomesheni ndani ya uwanja.

Anaweza kufiti pia kwenye mfumo wa 4-3-1-2 au ule wa 3-5-2. Hata kwenye 4-2-3-1, Ramsey yupo vizuri akicheza nyuma ya mshambuliaji wa kati, ambaye bila ya shaka atakuwa Cristiano Ronaldo.

Shida ni kwamba kocha atakayekuja msimu ujao atakuwa chaguo lake? Hatakuwa na wakati mgumu Mauricio Pochettino akitua kwenye kikosi hicho. Poch anamfahamu vyema Ramsey na makali yake ndani ya uwanja.

Haitakuwa shida Juventus ikiwa chini ya Jose Mourinho. Kuna wakati Mreno huyo alipokuwa Man United alipiga hesabu za kwenda kunasa saini yake.