Msimu wa Liverpool huu, washindwe wenyewe

Tuesday January 1 2019

 

By BONIFACE AMBANI, NAIROBI

JANA tuliumaliza mwaka wa 2018 na leo tunaukaribisha Mwaka Mpya wa 2019. Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuvusha salama kwa mwaka huu mpya na hongereni mashabiki wote wa soka na wapenzi wa gazeti la Mwanaspoti.

Kama wewe ni shabiki wa soka, hususan wa klabu ya Liverpool, nadhani utakuwa umevuka mwaka huu ukiwa umetabasamu.

Huko kwenye Ligi Kuu England hapapoi,. Mwanzoni hakuna aliyeweza kutabiri nani atanyakua taji hilo. Ni ligi ambayo kamwe huwezi kutabiri bingwa mpaka dakika za mwisho tofauti na ligi nyingine kama La Liga ya Hispania.

Hata hivyo, kwa sasa Liverpool inayonolewa na Kocha Jurgen Norbert Klopp inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na alama 54 kutokana na mechi 20 walizocheza hadi sasa, wakishinda mechi 17, sare tatu na hawajapoteza hata moja.

Ikumbukwe, mara ya mwisho kwa Liverpool kushinda taji hili ilikuwa mwaka 1989-90 chini ya Kocha Kenny Daglish na hadi sasa ni takriban miaka 27 imepita. Pia Liver imeshinda taji la FA mara ya mwisho mwaka 2006.

Nikiangalia kwa undani msimu huu, ni wazi taji hilo linakwenda Anfield.

Liverpool ilianza msimu vizuri sana na wameendeleza huo mziki hadi leo. Matokeo hayo mazuri kwa kweli yameletwa na juhudi za wachezaji kama mlinda lango Alison Becker na Simon Mignolet.

Andrew Robbertson, Virgil Van Dijk, Wijnaldum, James Milner, Fabinho, Naby Keita, Sadio Mane, Danny Sturidge, Xherdan Shaqiri, Roberto Firmino na King Mohammed Salah wamekuwa gumzo kubwa sana Liverpool. Kwa walichokifanya msimu huu, ni wazi wanastahili taji hilo.

Kuwachapa Manchester United na Arsenal Utd na Arsenal kuliwaongezea matumaini makubwa mno, pamoja na kusuasua kwa Manchester City walio nafasi ya pili kwa alama 47.

Msimu huu Klopp akishindwa kunyakuwa taji hili, hawatakaa watwae tena na hii itajulikana kuanzia Januari hii. Hata hivyo, niwatakie heri kwani raha ya soka ni mataji na sio kushinda mechi tu.

Wakati huo huo, Man United chini ya Kocha wa muda, Ole Gunnar Solskjaer wamezidi kuonyesha makali yao, huku kiundgo wao Paul Pogba akadhihirisha ni kwa sababu gani alisajiliwa kwa fedha nyingi.

Kamwonyesha Jose Mourinho ni kiwango gani alichonacho na ni wazi atabaki akijilaumu. Ndani ya mechi mitatu tu, Pogba kapiga mabao manne na kutoa asisti zaidi ya nne zilizozaa mabao. Ameonyesha umahiri wake.

Ole Gunnar amerudisha furaha kwa nyuso za wachezaji na mashabiki wa United kwa jumla.

Kazi anayoipiga pale Old Trafford sio mchezo. Balaaa kweli. Ukiona jinsi timu inavyocheza kwa sasa, utaamini kweli soka sio kocha kuwa na makaratasi tu, bali maelewano na wachezaji wake. Sio mbwembwe nyingi kama za Mourinho.

Kwa sasa umoja pale United unaonekana na kama wataendelea hivyo, basi sina budi kusema watamaliza ndani ya nne bora. Wachezaji United wamejituma sana katika mechi zao tatu zilizopita.

Kazi ipo kwa Arsenal ya Kocha Unai Emery. Masahibu ya mwezi Desemba yameanza kuonekana. Tayari wameshachapwa na Liverpool mabao 5-1. Hii inaonyesha wazi kikosi hicho hakijakamilika. Bado hakijawa cha ushindani kushinda mataji makubwa duniani. Walionekana wadhaifu na wanyonge sana. Lazima Unai afanye kazi ya ziada.

Kwa leo nafikia kikomo hapo. Nawatakia wasomaji na wapenda michezo na ndugu na dada zangu wote duniani heri na fanaka kwa Mwaka Mpya huu wa 2019. Mwenyezi Mungu awalinde. Asanteni.