Mfumo huu wa Ligi Kuu ya Vijana U20 hauna tija

MAISHA ya mwanadamu kwa upande mmoja yametawaliwa na mazoea kwa maana kuionyesha jamii naye anafanya jambo fulani hata kama halina faida kwake, ilimradi aonekane amefanya.

Mei 4, 2019, Ligi ya Vijana U20 kwa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara imeanza kutimua vumbi kwa mechi ya ufunguzi ambayo iliwakutanisha Kagera Sugar na Mbao FC kwenye dimba la Kaitaba mjini Bukoba na Mbao FC kuibuka na ushindi wa magoli 2-1.

Ligi hiyo inashirikisha timu 20 za vijana kutoka katika klabu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara.

Timu zinazoshiriki ligi hiyo zimepangwa katika makundi manne yenye timu tano tano na itachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini na fainali ya ligi hiyo itachezwa mwezi ujao katika kituo kimoja ikiwezekana itakuwa tena Dodoma kama msimu uliopita.

Timu mbili za juu za kila kundi zitaenda hatua ya Nane Bora kwenye kituo kimoja na hapo zitachezwa mechi kwa mfumo wa mtoano.

Kuanzia Nane Bora (robo fainali) mpaka fainali na bingwa kupatikana.

KWANINI HAINA FAIDA?

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ndiyo baba mlezi wa klabu nchini, hivyo katika kanuni zake inazitaka klabu zote zinazocheza Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL) kuwa na timu za vijana, lakini ina jukumu pia la kuandaa Ligi ya Vijana.

Nasema Ligi ya haina maana kwa sababu haina faida kwa nchi katika kuendeleza soka letu. Ni ligi ambayo haijengi wachezaji wazuri wenye kuleta ushindani, ni ligi ambayo haina tofauti na mashindano ya Jimbo Cup yanayoendeshwa na rafiki yangu Seif Gulamali (Mbunge wa Manonga).

Ligi inachezwa kwa mwezi mmoja na siku kadhaa inaisha, hivi tunawezaje kusema hiyo ni ligi? Kwa nini tusiite mashindano tu ya timu za vijana?

Ninachokiona hapa ni mazoea tu, kuna mashindano ya vijana kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu, ila TFF inaendesha haya mashindano katika huu mfumo ili kupunguza lawama kutoka kwa wadau wasionekane wameshindwa kuandaa ligi hiyo.

TATIZO MFUMO

Mfumo wa haya mashindano siyo rafiki hata kidogo katika kukuza vijana maana mwaka mzima unakuta timu za vijana zimekaa tu, hazina mashidano yoyote.

Halafu ukifika wakati wa kuita timu za vijana za Taifa tunatupa lawama kwa makocha kwamba wanaokota wachezaji au wanaita watoto wa ndugu zao.

Kuna haja ya kubadilisha mfumo wa haya mashindano ya vijana kwa timu za Ligi Kuu badala ya kuchezwa kwa mfumo wa sasa iwe ligi inayochezwa mwaka mzima.

Tukiwa na ligi ya vijana yenye ushindani itatusaidia kuwa na timu nzuri za Taifa za vijana, pia itatusaidia kutengeneza vijana wengi ambao wanaweza kuuzika nje.

Mfano, timu 20 za vijana zinaweza kuwekwa katika makundi mawili ya timu 10 na ligi ikachezwa kama ilivyo Ligi Kuu na mwisho timu mbili za juu kwa maana ya timu moja inayoongoza kundi A inaenda kucheza na timu inayoongoza kundi B na mshindi ndiyo anakuwa bingwa wa ligi ya vijana kwa msimu mzima.

Tukitumia mfumo huu kila timu itacheza mechi 18 kwa maana mzunguko wa kwanza kutakuwa na mechi 9 kwa kila timu na mzunguko wa pili kutakuwa na mechi 9 tena kwa kila timu.

Hii inaweza kutusaidia kujua wachezaji bora na wenye uwezo watakaoweza kucheza hata kwenye timu za taifa.

Wachezaji watapata mechi nyingi za kuimarisha viwango vyao, wachezaji wanaweza kuwa na mwendelezo mzuri, wachezaji wataweza kujijenga vizuri hata katika utimamu wa mwili.

Haya mashindano kwa sasa yanazalisha wachezaji wachache sana wanaoingia kwenye mfumo wa Ligi Kuu kwenye klabu zao kutokana na kukosa uzoefu wa kutosha na ubovu wa mashindano yenyewe.

Ukisoma kanuni za TFF 2018-2019 kwa klabu za Ligi Kuu, Ligi Daraja la kwanza na Ligi Daraja la Pili unaweza kusema sasa mpira wetu unaenda mbele, yaliyomo kwenye kanuni ni tofauti na yanayofanyika.

Tunaambiwa kwenye kanuni klabu za Ligi Kuu zinatakiwa kuwa timu za vijana chini ya miaka 20 (U20) na U17, lakini wakati huo huo timu za Ligi Daraja la Kwanza na Daraja la Pili zinatakiwa kuwa na timu za vijana chini ya miaka 17 (U17).

Yako wapi mashindano ya vijana chini ya miaka 15 (U15) yanayoshirikisha timu za Bara na Zanzibar?

UTATA UPO HAPA

Lazima TFF waache ubabaishaji na mazoea ya kufanya mambo ili kutimiza matakwa ya kikanuni bali wafanye mambo ambayo yana faida kwa soka la nchi yetu.

Tunalalamika mpira wetu hauendi mbele na kujiuliza tatizo liko wapi, ukweli tuna vitu vingi vya kubadilisha ili kuleta mabadiliko na maendeleo.

Najua kilio cha TFF kinaweza kuwa changamoto ya wadhamini, lakini naweza kusema siyo kweli kwani wadhamini wanaweza kupatikana bali tatizo ni ubabaishaji wao wenyewe TFF ndiyo maana wadhamini wanakosekana mpaka Ligi Kuu nayo inakosa mdhamini mkuu.

TFF badilikeni mazoea hayawezi kuleta mabadiliko.

NB: Emmanuel Makalla amejitambulisha kama msomaji wa Mwanaspoti anapatikana kwa

+255716605949