Messi na viwembe wenzake Ligi ya Mabingwa

LONDON, ENGLAND. UTAMU wa Ligi ya Mabingwa Ulaya umeshafika hatua ya nusu fainali kwa sasa, ambapo vigogo wanne Barcelona, Liverpool, Ajax na Tottenham Hotspur ndio waliobaki kwenye kinyang’anyiro hicho cha kuusaka ubingwa wa msimu huu.

Sambamba na hilo, kuna mastaa hao wameonyesha kuchuana jino kwa jino kwenye kufunga mabao ili kunyakua tuzo ya ufungaji bora kwenye michuano hiyo ambapo wakali wanaoongoza kwa kufunga kwa sasa ni hawa hapa. Supastaa, Lionel Messi ndiye kinara huku wapinzani wake wanaosogolea kwa karibu ni mmoja tu ndiye aliyebaki kwenye michuano hiyo, Dusan Tadic, lakini wengine wote wameshatupwa nje.

5. Dusan Tadic – dakika 900, mabao 6

Dusan Tadic amekuwa kwenye ubora mkubwa kabisa katika mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Amefunga mabao sita katika dakika 900 alizocheza na kuisaidia Ajax kutinga hatua ya nusu fainali tena wakipita kwenye msitu wenye wababe watupu ambapo imewasukuma nje Real Madrid na Juventus. Staa huyo mwenye umri wa miaka 30 hakuonekana kuwa ni wa maajabu alipokuwa kwenye kikosi cha Southampton huko England kabla ya kwenda Ajax, ambako amekwenda kuwa moto na msaada mkubwa kwa msimu huu wakisaka taji la Ulaya.

4. Cristiano Ronaldo – dakika 749, mabao 6

Juventus waliwekeza mkwanja mrefu kwa Cristiano Ronaldo ili awasaidie kutamba kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini mambo hayakuwa mepesi kihivyo na kukomea robo fainali wakitupwa nje na Ajax. Hata hivyo, straika huyo ameonyesha kuwa moto kwenye kupasia nyavu akifunga mara sita licha ya kwamba mabao yake yameshindwa kuifikisha mbali timu hiyo. Mabao yake sita aliyofunga msimu huu kwenye dakika 749 alizocheza yamemfanya Ronaldo kufikisha 126 na hivyo kuwa mfungaji kinara wa kihistoria katika michuano hiyo.

3. Sergio Aguero – dakika 510, mabao 6

Straika wa Manchester City, Sergio Aguero ameonyesha kuwa mmoja wa washambuliaji matata kabisa duniani kwa sasa baada ya kufunga mara sita kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya licha ya kushindwa kuisaidia timu yake kutinga nusu fainali. Staa huyo wa Kiargentina alifunga bao lake la sita juzi Jumatano wakati Man City ilipotolewa kwa bao la ugenini na Tottenham Hotspur licha ya kushinda 4-3 uwanjani Etihad. Mechi ya kwanza Man City ilifungwa 1-0, hivyo matokeo ya jumla ya 4-4 yaliwapa nafasi Spurs ya kusonga mbele wakitinga nusu fainali. Staa mwingine mwenye mabao sita ni Mousa Marega wa FC Porto.

2. Robert Lewandowski – dakika 714, mabao 8

Robert Lewandowski kama kawaida yake siku zote amekuwa matata sana anapokuwa mbele ya goli huko kwenye kikosi cha Bayern Munich, ndiyo maana msimu huu amefunga mara nane katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Timu yake imetolewa mapema sana, kwenye hatua ya 16 bora tu, lakini Lewandowski ameonyesha yeye ni hatari katika kuzipasia nyavu. Amecheza kwa dakika 714 tu, lakini ametumia muda huo ndani ya uwanja kuonyesha ubora wake kwa kufunga licha ya timu yake kwamba haijafika mbali sana katika michuano hiyo ya kusaka ubingwa wa Ulaya.

1. Lionel Messi – dakika 657, mabao 10

Mshindi mara tano wa Ballon d’Or, Lionel Messi amekuwa kwenye kiwango bora kabisa huko katika kikosi cha Barcelona msimu huu. Staa huyo wa kimataifa wa Argentina amefunga mabao 10 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya katika dakika 657 alizocheza na kuisaidia timu yake kutinga hatua ya nusu fainali huku wakiwaengua Manchester United kwenye robo fainali. Messi yupo bize kuwatafutia Barcelona ubingwa wao wa kwanza wa Ulaya tangu mwaka 2015, ambapo hapo katikati mambo yao yalikuwa hovyo na kuwashuhudia wapinzani wao Real Madrid wakitamba kwenye mikikimikiki hiyo kwa miaka mitatu mfululizo.