Mechi za Ugenini zilivyoiponza Azam

WAKATI vita ya ubingwa ikiwa kwa timu tatu zinazofuatana katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC ambayo ipo nafasi ya pili katika msimamo huo imeonekana kuyumba na kupoteza pointi nyingi ambazo zinaiondoa katika kinyang’anyilo cha ushindani huo.

Azam FC imecheza michezo 24 imeshinda michezo 14 imetoka sare michezo minne imefungwa michezo miwili na kufanikiwa kujikusanyia pointi 50 nyuma ya vinara wa msimamo huo Yanga ambao wanapointi 61.

Azam inayonolewa na Hans Van Pluijm katika michezo mitano ya hivi karibuni ikiwa katika viwanja vya ugenini imeonekana kuyumba na kupunguzwa kasi na baadhi ya timu kwa kupoteza pointi na kuambulia pointi moja katika baadhi ya michezo.

Yanga na Azam katika kinyang’anyilo hicho ndio wamemaliza mzunguko wa kwanza wakati Simba wakiwa na viporo. Je, wajua kuwa katika sare zote nne ambazo Azam FC wamezipata zimewapa pointi nne kutokana na michezo yao yote za kwanza kupata matokeo katika uwanja wa nyumbani?

Mwanaspoti inakuletea michezo sita imbayo imempa pointi nne tu katika viwanja sita alivyocheza kwa kutoka sare michezo minne na kufungwa michezo miwili.

AZAM VS MWADUI (1-1)

Katika michezo miwili waliyokutana Azam na Mwadui huku akiwa mwenyeji kwenye uwanja wake wa nyumbani alifanikiwa kupata pointi zote tatu baada ya mshambuliaji wake wa kimataifa, Donald Ngoma kuwafungia bao dakika ya 70 ambalo lilidumu hadi kipyenga cha mwisho cha mwamuzi kuashiria mpira umeisha.

Azam FC ikiwa katika uwanja wa ugenini ilitangulia kupachika bao la kuongoza dakika ya 55 bao lililofungwa na kiungo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ akiwa nje ya 18 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Ramadhan Singano ‘Messi’, dakika ya 72 Irakoze Ibrahim aliisawazishia timu yake na kuifanya timu yake iambulie pointi moja katika uwanja wake wa nyumbani.

AZAM VS BIASHARA (0-0)

Mzunguko wa kwanza Azam iliibuka na ushindi wa bao 2-1 katika Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam Biashara ndio ilikuwa ya kwanza kuliona lango la wenyeji wao baada ya dakika ya kwanza ya mchezo, Innocent Edwin kukwamisha mpira nyavuni hadi mapumziki wenyeji walikuwa nyuma kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili mabao ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Ramadhan Singano ‘Messi’ yaliyofungwa dakika ya 46 na 62 yaliwafanya Azam FC waibuke na ushindi na kuzoa pointi zote tatu na mzunguko wa pili wakiwa ugenini walitoka sare ya bila kufungana na kugawana pointi moja moja.

AZAM VS MTIBWA (0-2)

Mtibwa Sugar ndio ilikuwa wenyeji katika mchezo huo ukiwa ni mzunguko wa pili wa Ligi kuu Tanzania bara walipata bao la kuongoza dakika ya 14 na Jaffar Kibaya ndiye aliyekwamisha mpira nyavuni hadi mapumziko Azam FC alikuwa nyumba kwa bao moja.

Dakika 80 ya kipindi cha pili, Ally Makarani aliwaongezea msumali mwingine Azam FC ambao walishindwa kupata ata bao moja la kufutia machozi hadi kipyenga cha mwamuzi kilipopulizwa mchezo wa marudiano kwa timu zote mbili utachezwa katika Uwanja wa Chamaji jijini Dar es Salaam.

AZAM VS LIPULI (1-1)

Zimekutana mara mbili mzunguko wa kwanza na wapili zimegawana pointi mbili kila mmoja ni baada ya mzunguko wa kwanza wenyeji wakiwa Azam FC kukubali sare ya bila kufungana katika uwanja wao wa nyumbani.

Mzunguko wa pili Lipuli akiwa mwenyeji walifanikiwa kuandika bao lake la kuongoza dakika ya 45 na Azam FC walitoka mapumziko wakiwa nyuma kwa bao moja dakika ya 80 Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliwasawazishia wanalambalamba bao lililodumu hadi kipyenga cha mwisho cha mwamuzi kilivyopulizwa.

AZAM VS TANZANIA PRISONS (0-1)

Mshambuliaji chipukizi wa Azam FC ambaye ametimkia CD Tenerife ndiye aliyeichapa Tanzania Prisons katika uwanja wake wa nyumbani kabla ajatimka nchini aliifungia timu yake dakika ya 58 bao ambalo lilidumu hadi kipyenga cha mwisho cha mwamuzi kinapulizwa.

Ubabe ubabe hivyo ndio unaweza kusema baada ya Prisons kulipa matokeo kama hayohayo katika uwanja wao wa nyumbani kwa kufanikiwa kukwamisha mpira nyavuni kwa mkwaju wa penalti baada ya Yacob Mohamed kuunawa mpira ndani ya box na Jumanne Elfadil kuifungia timu yake dakika ya 35.

AZAM VS COASTAL

UNION (1-1)

Mzunguko wa kwanza Azam FC aliutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani kwa kupata pointi tatu na mabao mawili ambapo dakika ya 29 Donald Ngoma aliifunga Coastal Union na ndio lilikuwa bao lake la kwanza tangu amejiunga na klabu hiyo, bao la pili lilifungwa na Dany Lyanga dakika ya 70 ambapo aliingia akichukua nafasi ya Ngoma.

Mzunguko wa pili Costal Union ndiye alikuwa mwenyeji walitumia dakika 45 za kipindi cha kwanza kupata bao la kuongoza lililofungwa na Ayub Lyanga katika dakika za nyongeza na Azam FC walisawazisha bao kupitia kwa Obrey Chirwa dakika ya 51 bao lililodumu hadi kipyenga cha mwisho cha mwamuzi kilivyopulizwa.