Mbinu za Zahera ghafla zimebana!

Friday February 8 2019

 

By MATEREKA JALILU, SINGIDA

MARA ya mwisho Yanga kuchomoza na ushindi ilikuwa 3-1 Januari 15 pale Uwanja wa Taifa dhidi ya Mwadui FC, ambapo mabao ya Amissi Tambwe, Feisal Salum (Fei Toto) na Ibrahim Ajibu yalitosha kumfanya Mkongomani Mwinyi Zahera kuendelea kufurahia kazi yake kwa mabingwa hawa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara.

Ushindi wa Januari 15 ndio ulikua wa mwisho kwa Yanga kutoka uwanjani wakiwa na furaha, ushindi ambao unawafanya wazidi kuongoza ligi japo imepoteza mchezo mmoja tu dhidi ya Stand United uwanjani Kambarage mjini Shinyanga ilipolala kwa bao 1-0.

Lakini, tangu kupata ushindi huo, Yanga imepoteza alama saba kwenye mechi tatu za Ligi Kuu Bara, kwanza ilichapwa na Stand United ambayo pia ilitibua rekodi ya Zahera ya kutofungwa mechi hata moja kisha ikadondosha alama nne kwa kulazimishwa sare mara mbili dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwa kwenda sare ya bao 1-1 kisha juzi Jumatano ikabanwa mbavu na Singida United kwenye Dimba la Namfua.

Katika mchezo wa juzi ulikuwa na ushindani ndani na nje ya uwanja, lakini mwisho wake haukuwa na mbabe kwani, walitoka uwanjani bila kufungana licha ya timu zote kutengeneza nafasi nyingi za mabao lakini washambuliaji wake hawakuwa makini katika kumalizia nafasi walizokuwa wanazipata.

Mwanaspoti lilikuwepo uwanjani hapo kushuhudia mchezo, Uwanja haukujaa sana kama mechi mbili za zilipokutana timu hizo msimu uliopita, hii hapa tathmini fupi ya mchezo huo uliomalizika kwa suluhu.

PRESHA YA MCHEZO

Kabla ya mchezo kuanza kulikuwa na hisia tofauti kwa pande zote mbili kuelekea mchezo wenyewe, presha ya mchezo ni jambo lililopelekea ndani ya uwanja wachezaji kucheza kwa tahadhari kubwa.

Ukiachana na kelele za mashabiki majukwaani ambayo ni kawaida, wachezaji wa pande zote mbili walishindwa kutulia wakati walipokuwa na mpira na kupelekea mipira kutokaa kwa timu moja muda mrefu zaidi ya kupiga mipira mirefu iliyokosa uhakika na kupotea.

MKONGO ASHITUA JUKWAA

Zahera alishangaza wengi kwa kitendo cha kumuacha nje nahodha wake, Ibrahim Ajib na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo kinda Gustafa Saimon, ambaye alianza kwenye kikosi cha kwanza kwa mara ya kwanza.

Pia, alianza na Deus Kaseke kwenye mchezo huo pamoja na Matheo Anthony kwenye eneo la juu wakimzunguka mshambuliaji Heritier Makambo, lakini mbinu hizo hazikuwa na matokeo chanya katika kupachika mabao.

Hatua ya Ajibu kuanzia benchi ilionekana kama ni adhabu kutokana na mechi ilizopita kuonekana kutokuwa kwenye kiwango chake, lakini baadaye ilibainika ni mbinu za Zahera kuwapumbaza wapinzani wake, jambo ambalo pia halikuzaa matunda.

POPADIC ALIVYOPANGUA

Kocha wa zamani wa Singida United ambaye miaka ya nyuma aliwahi kukinoa kikosi cha Simba, Dragan Popadic ulikuwa mchezo wake wa kwanza wenye upinzani mkali kukipiga na vinara hawa wa Ligi Kuu Bara, alimuanzisha Boniface Maganga kwenye nafasi ya ushambuliaji tofauti na alivyozoeleka kama beki wa kulia japo ni kiraka.

Pia alimuanzisha chipukizi wa timu hiyo Athanas Mdamu, ambaye hata hivyo alishindwa kuonyesha makeke yake na kutolewa kipindi cha pili.

UWANJA HAUKUWA RAFIKI

Unaweza kusema sio sababu kulingana na viwanja vingi vinavyotumika kwenye Ligi Kuu Bara havina ubora sana hususani sehemu ya kuchezea jambo ambalo huufanya mchezo usiwe na ladha tofauti na baadhi ya viwanja vyenye ubora hapa Tanzania kama vile Uwanja wa Taifa, uhuru na Samora.

Kiujumla uwanja wa Namfua sio rafiki sana kwa kila timu kucheza soka lenye kuvutia hasa pasi na kupitisha mipira kwenye njia zake ndio sababu pengine timu zote mbili zilishindwa kupiga pasi kwa ubora zaidi ya kutumia mipira mirefu.

Karibu uwanja mzima kwenye eneo la kuchezea ulikuwa mbovu kiasi cha mpira kuonekana kama wa butua butua na timu kulazimika kutumia mipira ya juu zaidi badala ya soka maridadi la pasi za chini.

MVUA YATIBUA

Wakati mpira ukiwa unaelekea ukingoni huku kila timu ikijaribu kusaka pointi tatu, mvua kubwa iliyoanza taratibu ilianza kunyesha na kutibua mipango yote ya timu hizo na kuanza kupiga mipira mirefu isiyokuwa na mpangilio ili kusindikiza mchezo umalizike.

Kama sio mvua matokeo yangeweza kuwa tofauti kwani ni wakati huo Yanga walichachamaa kutafuta bao, hata hivyo baadhi ya michomo iliokolewa kwa ustadi mkubwa na kipa Said Lubawa.

Mvua hiyo ilileta taharuki kwa mashabiki waliokuwepo uwanjani ambao hawakuwa na sehemu ya kukimbilia zaidi ya kubanana katika jukwaa kuu ambalo limefunikwa kwa bati sehemu ndogo na kuwaacha mashabiki wengi kulowana huku wengine wakikimbilia nje kusaka hifadhi.

YANGA BADO SHUGHULI

Kikosi cha Yanga kinaendelea na harakati za kucheza mechi ngumu za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya msimu uliopita kuutema kwa wapinzani wao Simba.

Baada ya kubanwa na Singida United, Yanga watarudi tena Mkwakwani na kesho Jumamosi watakipiga na JKT Tanzania ambao kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wapo nafasi ya saba wakiwa na pointi 32 wakicheza mechi 25.

Mechi haitakuwa rahisi kwa Yanga, kwanza hawana matokeo mazuri kila wanapocheza katika Uwanja wa Mkwakwani, lakini wachezaji wengi wa kikosi hiko wameonekana kucheza katika viwango vya chini na kufanya makosa mengi katika safu ya ulinzi ambapo hufungwa mabao kirahisi na pia wanashindwa kutumia nafasi za kufunga wanazopata.

Wachezaji wa Yanga wanapata wakati mgumu kucheza katika uwanja huo kutoka mazingira ya eneo la kuchezea si rafiki, lakini JKT Tanzania ambao wamepanda Ligi Kuu msimu huu nao wanazidi kuimarika

Yanga baada ya kumalizana na JKT Tanzania, watarudi Dar es Salaam wakimngoja mtani wa Simba kwenye mchezo utakachezwa Februari 16.

Mara nyingi mechi ya Watani huwa si ya kutabiri hasa ukiangalia kikosi cha Yanga katika mechi nne zilizopita kinaonekana kucheza chini ya kiwango tofauti na kilivyoanza ligi, wamekuwa na makosa mengi ambayo yanawaghalimu kushindwa kupata ushindi.

Kukosekana na kwa Kipa wa Yanga Benno Kakolanya, ambaye alikuwa mchezaji bora katika mechi ya mwisho ya watani iliyopita kwa kuokoa nafasi nyingi za wazi ambazo Simba walikuwa na uwezo wa kupata mabao.

Yanga mara baada ya kumalizana na Simba watakwea pipa kuelekea Mwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba kucheza dhidi ya Mbao ambao tangu kupanda kwao Ligi Kuu hawajawahi kupoteza katika uwanja huo kila wanapokutana na Yanga na hapo ndio mtihani mwingine kwa kwao.