Mastaa wa zamani wa Arsenal wanaiadhiri timu yao iliyowatoa

Friday February 8 2019

 

LONDON, ENGLAND. Kama kuna timu ambayo imekuwa ikinyanyaswa na wachezaji wake wa zamani basi ni Arsenal. Katika utawala wa kocha aliyepita, Arsene Wenger, Arsenal imeuza wachezaji wengi mahiri ambao pindi wanapokumbana na timu yao ya zamani huwa wanacheka na nyavu.

Wafuatao ni mastaa wa zamani wa Arsenal ambao waliwahi kuifunga Arsenal wakiwa na timu nyingine baada ya kuuzwa na wababe hao wa London Kaskazini.

Emmanuel Adebayor

Staa wa kimataifa wa Togo, Emmanuel Adebayor ambaye aliuzwa na Arsene Wenger kwenda Manchester City kwa dau la pauni 25 milioni katika dirisha kubwa la majira ya joto. Mwaka huo huo alwafunga Arsenal katika pambano lililojaa upinzani mkubwa huku bao lake likiipeleka City mbele 2-1. Adebayor alishangilia bao hilo kwa kukimbia kwa umbali mrefu kwenda kushangilia mbele ya mashabiki wa Arsenal ambao walikuwa wanamzomea kwa muda mrefu wa mechi hiyo. City walishinda 4-2 lakini Adebayor alitozwa faini ya pauni 25,000 na FA kwa kitendo chake cha kwenda kushangilia mbele ya mashabiki wenye hasira wa Arsenal. Ingawa aliomba radhi kwa kitendo hiki lakini mwenyewe alidai kwamba kilifanya atoe machungu yake kwa dhidi ya mashabiki wa Arsenal ambao walikuwa wanamzomea kwa muda mwingi wa pambano hilo.

Cesc fabregas

Kocha wa Arsenal wa zamani, Arsene Wenger alimpa unahodha Cesc Fabregas akiwa na umri wa miaka 21 tu. Fabregas alikuwa kipenzi kikubwa cha mashabiki wa Arsenal pale Emirates. Baadaye alikwenda Barcelona kabla ya kurudi nyumbani tena katika Ligi Kuu ya England akiwa na wapinzani Chelsea. Februari 4, 2017 Fabregas aliifunga Arsenal bao katika ushindi wa mabao 3-1 wa Chelsea dhidi ya Arsenal Stamford Bridge. Bao lake lilikuja kama zawadi baada ya kupokea pasi mbovu iliyopigwa na kipa wa Chelsea, Petr Cech na akafunga kwa urahisi. Hata hvyo kwa heshima yake dhidi ya Arsenal na mashabiki wake, Fabregas hakushangilia bao hilo.

Nicolas Anelka

Pengine huyu ndiye mchezaji wa zamani wa Arsenal aliyewadhuru zaidi Arsenal. Alinunuliwa kwa dau la pauni 500,000 tu na Arsene Wenger kutoka PSG na baadaye ilionekana kuwa Arsenal wamepiga bao baada ya Anelka kubuka kuwa mmoja kati ya washambuliaji tegemeo Highbury. Baada ya misimu miwili akalazimisha kuuzwa kwenda Real Madrid ambapo Arsenal walipata pauni 22 milioni.

Hata hivyo huo ulikuwa mwanzo wa Arsenal kuteseka naye. Anelka aliifunga Arsenal mara saba akiwa na timu pinzani za Manchester City, Bolton na Chelsea.

Alishindwa kufanya hivyo katika jezi ya Liverpool. katika orodha hii Anelka ndiye ambaye anaongoza kwa kucheza mara nyingi zaidi dhidi ya Arsenal huku pia akiongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi.

Robin van Persie

Staa wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi ambaye aliibuka kuwa mfungaji tegemeo katika kipindi chake Arsenal.

Hata hivyo wakati mkataba wake ukitiririka kwenda mwishoni Arsene Wenger alilazimika kumuuza kwenda Manchester United kwa dau la pauni 24 milioni wakati huo akiwa na umri wa miaka 29. Aliifunga Arsenal mabao matatu katika mechi tano alizocheza dhidi yao. Mechi yake ya kwanza hakushangilia.

Pambano lake la pili alishangilia baada ya mashabiki wa Arsenal kuendelea kumzomea muda mwingi wa mchezo kama ilivyokuwa katika mechi ya kwanza.

Kitu ambacho kiliwaumiza zaidi mashabiki wa Arsenal ni ukweli kwamba licha ya kuwafunga mabao lakini katika msimu wake wa kwanza aliokipiga na Manchester United van Persie alifanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu ya England na United huku wao wakiwa wanateseka kulisaka taji hilo tangu mwaka 2004.

Alexis Sanchez

Staa mwingine wa zamani wa Arsenal aliyeondoka kwa utata Emirates. Alitimkia Manchester United Januari mwaka jana katika dirisha dogo huku kwa upande mwingine Arsenal wakinufaika kwa kufanikiwa kumnasa kiungo wa kimataifa wa Armenia, Henrikh Mkhitaryan.

Tofauti na Van Persie na mastaa wengine wa orodha hii, mambo hayakumuendea poa staa huyu wa kimataifa wa Chile alipotua Old Trafford.

Katika utawala wa kocha, Jose Mourinho aliibuka kuwa nyanya na kulikuwa kuna fikra kwamba huenda Manchester United ingeachana naye kutokana na ukubwa wa mshahara wake wa pauni 500,000 kwa wiki.

Hata hivyo kwa sasa chini ya utawala wa kocha, Ole Gunnar Solskjaer Sanchez ameanza kuibua makali yake na wiki mbili zilizopita alirudi katika uwanja wake wa zamani wa Emirates na kufanikiwa kufunga bao moja katika ushindi wa mabao 1-3 wa Manchester United dhidi ya Arsenal kombe la FA.

Bao hilo linamfanya kuwa mchezaji wa mwisho wa zamani wa Arsenal kufunga bao dhidi ya timu yake hiyo ya zamani.