Makipa wetu watamrudisha Kaseja Stars

SIDHANI kama linaweza kuwa jambo la kushangaza iwapo kipa wa KMC, Juma Kaseja atarudishwa kwenye Kikosi cha Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ siku za usoni baada ya kuwa nje kwa zaidi ya miaka mitano.

Wengi wanamuona Kaseja kama amezeeka na huu ni wakati wa kuwapa nafasi vijana lakini zipo sababu kadhaa za msingi ambazo zinalazimisha Kaseja (34) kupewa nafasi kwa mara nyingine kwenye kikosi cha Stars. Kwanza amekuwa akifanya vizuri kwenye Ligi Kuu msimu huu na ni miongoni mwa makipa wachache waliocheza idadi kubwa ya michezo bila ya kuruhusu nyavu zao kutikiswa (clean sheet).

Kipa huyo amecheza zaidi ya mechi nane bila nyavu za KMC kutikiswa katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu. Ni makipa wachache wazawa ambao kitakwimu wanamzidi ama wapo sawa na Kaseja. Kimsingi mchezaji aliye kwenye fomu ndani ya nyakati husika ndio anatakiwa apewe nafasi katika Stars kwa sababu huwa sio cha majaribio. Lakini sababu nyingine inayomfanya Kaseja astahili kuwemo kwenye kikosi cha Stars ni kiwango cha chini kinachoonyeshwa na makipa ambao ndio wana mwelekeo wa kuitwa kwenye timu hiyo kulingana umri wao na uzoefu. Makipa wazawa wamekuwa wakifanya makosa ya kizembe ambayo ni nadra kuyaona kwa Kaseja hasa katika kucheza mipira ya krosi pamoja na nidhamu ndani ya uwanja.

Ndani ya kipindi cha siku nne tu zilizopita tumeshuhudia Ramadhani Kabwili, Metacha Mnata na Deogratias Kisembo wakifanya makosa mepesi ambayo yalizizawadia timu pinzani mabao mepesi.

Wakati wengine wakivurunda ndani ya uwanja, unakutana na taarifa za kipa mwingine wa Mtibwa Sugar, Benedictor Tinoco kumkanyaga kwa makusudi mchezaji wa timu pinzani.