Majeraha haya yanawasubiria wengi England

Friday August 10 2018

 

KILE kipute maarufu cha soka la Ligi Kuu England (EPL) kwa msimu mpya wa 2018/19 ndio kinaanza rasmi leo Ijumaa usiku katika Uwanja wa Old Trafford kwa mechi baina ya Manchester United na Leicester City.

Michezo mengine inatarajiwa kuendelea kesho Jumamosi na pia keshokutwa Jumapili kutakapokuwa na vumbi la Arsenal na Manchester City.

Sote tunajua ligi hii ni kati ya ligi bora za soka duniani na kwa kawaida hujaa ushindani mkubwa. Ni kutokana na hali hiyo, wachezaji wa timu za ligi hiyo hukumbana na majeraha ya mara kwa mara.

Pamoja na wanamichezo kufundishwa mbinu za kuyaepuka majeraha, kutumia vifaa vya kukinga majeraha na kupata matibabu sahihi na ya kisasa pale wanapoumia, lakini bado ni vigumu kukwepa majeraha ya michezoni.

Katika safu hii tunayaangalia majeraha matano ambayo yana asilimia kubwa ya kuwakumba wanasoka hao na hivyo kuwafanya baadhi yao kukaa nje ya uwanja.

Majeraha ya kifundo

Hili ndilo tatizo linaloongoza kuwapata wana michezo na hata watu wa kawaida wanapofanya mambo yanayoushughulisha mwili, ikiwamo kutembea na kukimbia.

Kama unakumbuka, wiki iliyopita kiungo mpya wa Manchester City Riyad Mahrez aliumia kifundo, lakini bahati nzuri yalikuwa maumivu ya kati na akaweza kucheza katika Ngao ya Hisani Jumapili.

Majeraha ya kifundo cha mguu yanahusisha kuvunjika vifupa vya vidole vya miguu, majeraha ya tishu laini ikiwamo kuvutika kwa kupitiliza, kukwanyuka au kuchanika kwa nyuzi ngumu (ligaments).

Nyuzi ngumu zinazoshikiza mfupa na mfupa huweza kupata michubuko midogo, kuchanika kiasi au kukatika kabisa na kuachana pande mbili.

Wakati wa kutembea, kukimbia kuruka na kutua, kifundo huweza kutua vibaya na kujipinda, hivyo kujeruhi tishu laini ikiwamo nyuzi ngumu ambazo hujivuta kupita kiasi na kusababisha jeraha.

Majeraha ya goti

Majeraha ya goti ikiwamo tishu zinazounda ungio la goti ni maumivu yanayowapata wachezaji wa EPL kutokana ligi hiyo kuwa yenye kasi na ushindani.

Wanapokimbia kwa kasi hupata maumivu sehemu ya goti mara kwa mara, mara nyingi eneo la mbele hupata shambulizi la nyuzi ngumu za miishilio ya misuli ya gotini (tendonitis).

Majeraha makubwa ya goti yanahusisha madhara au michubuko katika mfupa plastiki wa goti na nyuzi ngumu zinazounga mfupa na mfupa (ligaments).

Zipo nyuzi kuu nne za ligaments zinazopata majeraha ikiwamo yenye umbile la X katika eneo la nyuma ya goti, katika ya goti, mbele ya goti na pembeni mwa goti.

Majeraha ya ugoko

Majeraha ya ugoko pamoja na maumivu yake huwakumba wanasoka wa EPL kwa sababu wao hutumia miguu kucheza mchezo huo, hapo hukumbana faulo za mara kwa mara. Sehemu hii ambayo iko chini ya goti, maumivu yake hutokea sehemu ya mbele ambako kuna mfupa mkubwa wa mguu chini ya goti unaoitwa ‘Tibia’.

Vile vile maumivu ya eneo hili yanaweza pia kutokea katika makutano ya mifupa ya miguuni na sehemu ya mbele ya kifundo cha miguuni.

Matatizo ya magoti huchangiwa na kutopasha moto mwili, kutonyoosha misuli na viungo vya mwili kabla ya kuingia mchezoni, kutumia mbinu dhaifu za ukimbiaji na kutumia viatu visivyo stahili.

Vile vile mwanamichezo anaweza kuwa na kasoro ya kuzaliwa ikiwamo kuwa na maumbile nyayo ambayo ni bapa. Umbile hili husababisha majeraha ya mara kwa mara katika eneo la ugoko sehemu ya chini karibu na kifundo cha mguu.

Hii ndiyo sababu wanasoka huvaa kifaa tiba maalum ‘Shin Guard’ kinachokinga kupata majeraha ya ugoko, kifaa hicho kwa kiswahili huitwa Kikinga Ugoko.

Kuvunjika mifupa

Kuvunjika mfupa ni majeraha yanayotarajiwa kuwapata wanasoka wa EPL ingawa ni kwa uchache. Mfupa unaweza kuvunjika mara moja baada ya kukanyagwa vibaya au kujipinda vibaya wakati wa kucheza. Mara nyingine mfupa unaweza kupata ufa na hapo baadaye kuvunjika kabisa hii ni kutokana na kujirudia kupata shinikizo mara kwa mara katike eneo hilo hilo kwa kugongwa wakati wa kucheza.

Mara nyingi kuvunjika mfupa kunakotokana na shinikizo kubwa zaidi hasa kama mchezo unahusisha kugongana au kugongwa mara kwa mara.

Kuteguka mfupa

Kuteguka ni kunatokea pale mfupa unapolazimishwa kuhama kutoka katika pango la maungio ya mwili baada ya kupata shinikizo kubwa ikiwamo kupigwa na kutua vibaya wakiwa mchezoni. Kuteguka kitabibu huitwa ‘Dislocations’ au ‘luxation’. Tatizo hili kwa kawaida linahitaji matibabu kadhaa ikiwamo matibabu ya dharula.

Wanasoka wa EPL hupata majeraha haya wakati wanaporuka kuwania mipira ya juu na kutua vibaya na kuangukia mikono hasa katika eneo la ungio la bega. Inapotokea hivyo tishu hizo huvutika kupita kiwango na mfupa hukosa udhibiti na hivyo hutoka katika pango la ungio.

Mfupa ulio hama katika pango lake ulipounda ungio, unahitajika kurudishwa katika eneo lake, ingawa kuteguka huambatana na majeraha ya tishu laini zinazouzunguka mfupa huo katika maungio. Maungio ambayo mara kwa mara mifupa yake huteguka ni pamoja na vidole, mikono na mabega. Kuteguka kwa mifupa ya kiwiko, goti na paja hutokea mara chache.

Mfupa wa bega huteguka na kuhama katika pango la ungio la bega na kuhamia sehemu ya mbele, jeraha hilo la kuteguka hujulikana kitabibu kama ‘Anterior shoulder dislocation’. Hivyo basi Msomaji wa Mwanaspoti unapojiandaa kuanza kushuhudia uhondo wa EPL, tarajia pia kuwaona wachezaji wakikumbana na majeraha haya.