Kule Yanga mambo safi, Leopards inakosea wapi?

Tuesday May 21 2019

 

By BONIFACE AMBANI

KLABU ya mbili za soka ambazo nimewahi kuzitumikia kwa nyakati tofauti, mambo yao sio poa msimu huu.

Kule Tanzania, kuna klabu ya Yanga ambayo hivi karibuni imefanya uchaguzi wake baada ya vurugu za hapa na pale.

Yanga iliongoza Ligi Kuu ya Tanzania kwa kitambo kirefu sasa ina uongozi mpya na inaandaa mikakati ya kufanya usajili wa nguvu kuweza kukabiliana na watani zao wa jadi, Simba Sport Club.

Yanga imepoteza ubingwa baada ya watani wao wa jadi, Simba kuelekea kujimilikisha kwa msimu wa pili sasa. Kinachotakiwa kwa Yanga ni kujipanga kuweza kukabiliana na Simba kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu.

Baada ya kufanikiwa kupata viongozi wa kuiingoza klabu hiyo kwa miaka minne, kinachofuata ni kwa viongozi hao ni kufanya usajili wa maana.

Pamoja na kuongoza Ligi Kuu ya Tanzania, Yanga haikuwa na kikosi kipana cha kuweza kushindana na Simba kwenye ligi hiyo.

Advertisement

Kumbuka Simba ilikuwa na msimu mzuri mwaka huu baada ya kufanya vizuri pia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kutinga hatua ya robo fainali.

Klabu nyingine ambayo nimewahi kuitumikia kwa mafanikio makubwa ni AFC Leopards ya Kenya. Kwa kweli haiko vizuri kwa muda mrefu katika mambo mawili.

Ni kama ilivyokuwa kwa Yanga, AFC Leopards inahitaji viongozi wa kuivusha kutoka sehemu ilipo sasa na kupiga hatua kuweza kushindana na Gor Mahia ambao wanaonekana kutaka kujimilikisha soka la Kenya.

Gor Mahia ndio mabingwa wa Ligi Kuu Kenya (KPL) na wanaelekea kutetea ubingwa wao kwa mara nyingine. Kumbuka nayo ilitolewa kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba na Gor Mahia zinaonekana bado zina tamaa za kuwatesa wapinzani wao wa Yanga na AFC Leopards. Afadhali Yanga imeanza kusimama na kuanza kujipanga ili kushindana na wapinzani wao hao kwenye Ligi Kuu ya Tanzania msimu ujao.

Kwa upande wa AFC Leopards hali ni mbaya sana, nayo inahitaji kujipanga kwani kwa miaka ya sasa imekuwa timu ya kawaida kabisa.

Juzi kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Kasarani ilifungwa katika 3-1 dhidi ya Gor Mahia na kupoteza mwelekeo.

Ilikuwa ni huzuni kubwa mbele ya hailaki wa mashabiki ambao kwa kweli walifika kwa wingi mno.

Ni kichapo cha pili msimu huu kutoka kwa mahasimu hao. Mzunguko wa kwanza mechi iliisha kwa mabao 2-0.

Mashabiki wa AFC Leopards wamekuwa wakijiuliza tatizo ni nini? Kwa muda mrefu sasa klabu hiyo haijawahi kupata ushindi dhidi ya Gor Mahia.

Jibu liko wazi lakini mashabiki hawafahamu kama wanalo. AFC Leopards kwanza kabisa ni shida katika uongozi kama ilivyokuwa Yanga ya Tanzania.

Pili, inatakiwa kufanya usajili kwa kuwa imekuwa na wachezaji duni mno. Nikiangalia tu kwa undani kidogo, kila msimu ni lazima isajili zaidi ya wachezaji 15.

Itakuwa vigumu sana kuweza kutengeneza timu ya kupigania mataji. Juzi tu kuna klabu ilishuka daraja na AFC Leopards ikakimbia kwenda kusajili wachezaji wa hiyo klabu.

Haya yanafanyika wapi? Hao wachezaji wangekuwa wazuri klabu yao si isingeshushwa daraja? Leopards imebaki kusajali magarasa tu. Imebaki ikisajili wachezaji wa kawaida tu. Klabu imebaki ya kufanya biashara na sio ya kupigania vikombe ama mataji tena.

Inakera sana. Klabu inaendeshwa kama kioski. Usajili uanafika kushoto kulia kila msimu. Usajili ambao hausaidii klabu hata kidogo.

Inaudhi sana. Mechi ya dhidi ya Gor Mahia imeonyesha gepu lililopo kwa klabu hizi kongwe mbili.

Mashabiki waliondoka uwanjani kama wamegadhabika kabisa. Yote tisa klabu ya AFC Leopards inahitaji uongozi mpya. Uongozi ambao kwa kweli utarudisha hadhi ya klabu hiyo.

Ni aibu ukiangalia Gor Mahia ndani ya miaka saba iliyopita imeshinda mataji matano.

AFC Leopards Mara ya mwisho kushinda taji ilikuwa mwaka wa 1998. Takriban miaka 20 iliyopita. Hatutazidi kuishi hivi. Itakuwa ngumu sana. Lazima tubadilishe mienendo. Ukiwa a viongozi ambao hawafahamu soka ni shida sana.

Hawafahamu umuhimu wa kushinda mechi kama hizi. Hawafahamu umuhimu wa kushinda mataji. Hawafahamu umuhimu wa kusajili wachezaji wenye viwango, hawafahamu uzito wa klabu zao. Tutakuwa tunajidanganya. Uchaguzi wa klabu hiyo unakaribia. Inabaki kwa mashabiki kuamua cha kufanya.

Ni lazima mashabiki wajitambue. Ni lazima pia wao wenyewe wafahamu ni nini wanahitaji. Mambo ya kuchagua viongozi ambao hawafahamu lolote kuhusu soka inafaa ikome. Ikome kabisa. Shabiki. una kura yako. Ni wewe utaamua. Utaamua pahali pa kuiweka. Siku njema.