Kiatu cha Dhahabu vuta nikuvute EPL

Monday May 13 2019

 

LONDON ENGLAND

HADI kufika saa 11:00 jioni ya jana Jumapili, bingwa wa Ligi Kuu England kwa msimu huu alikuwa hajapatikana. Kila kitu kilifahamika baada ya dakika 90 baadaye. Liverpool walikuwa na kazi ya kuwakabili Wolves na wapinzani wao kwenye mbio za kufukuzia taji hilo, Manchester City walikuwa na shughuli ugenini kwa Brighton.

Hata hivyo, wakati mashabiki wakiwa bize kufuatilia kile kilichokuwa kikitokea huko Anfield na Amex Stadium kulikuwa na taji jingine lililokuwa likishindaniwa kibabe, Kiatu cha Dhahabu kwenye ligi hiyo.

Msimu uliopita vita ilikuwa kwa Harry Kane na Mohamed Salah na staa wa Liverpool, Mo Salah akaibuka kidedea alipofunga mabao 32, lakini msimu huu vita ilikuwa kali zaidi.

Hadi kufikia mechi za mwisho za kumaliza msimu wa Ligi Kuu England hiyo jana, kulikuwa na mastaa watano waliokuwa na nafasi ya kukibeba Kiatu cha Dhahabu kwenye ligi hiyo huku Mo Salah kwa wakati mwingine alikuwa kileleni akiongoza.

Mohamed Salah,

Liverpool - mabao 22

Mechi ya mwisho: vs Wolves (nyumbani)

Supastaa wa Liverpool, Mohamed Salah alikuwa kwenye nafasi ya kuweka rekodi ya kuwa mchezaji watatu katika muongo huu kutetea Kiatu cha Dhahabu Ligi Kuu England.

Kabla ya mechi ya jana nyumbani Anfield na staa huyo alihitaji kufunga mabao dhidi ya Wolves kwanza kuiweka Liverpool kwenye nafasi nzuri ya kubeba ubingwa, pia alihitaji kufunga mabao kukinyakua Kiatu cha Dhahabu cha msimu huu.

Wachezaji waliopita waliowahi kutetea Kiatu dha Dhahabu ni Robin van Persie (2011/12-2012/13) na Harry Kane (2015/16-2016/17). Hadi kufikia jana, Mo Salah ndiye aliyekuwa kwenye nafasi nzuri ya kunyakua tuzo hiyo.

Sergio Aguero, Man City - mabao 20

Mechi ya mwisho: vs Brighton (ugenini)

Straika wa Manchester City, Sergio Aguero alinyakua tuzo ya ufungaji bora Ligi Kuu England msimu wa 2014/15. Jana Jumapili aliingia uwanjani huko ugenini kwa Brighton kuisaka tena tuzo hiyo kwa msimu huu.Katika ya mechi hiyo, Aguero alikuwa ameshafunga mabao 20, mawili pungufu ya aliyokuwa amefunga kinara Mohamed Salah, hivyo fowadi huyo wa Kiargentina kwanza alihitaji kufunga mara nyingi zaidi kuipa timu yake ubingwa wa ligi, lakini na yeye akikusanya mabao ya kumpa Kiatu cha Dhahabu.

Aguero alibeba tumaini la mabao ya Man City kwenye mechi hiyo muhimu kabisa ya ubingwa, lakini mwenyewe akitaka tuzo pia.

Pierre-Emerick Aubameyang, Arsenal - mabao 20

Mechi ya mwisho: vs Burnley (ugenini)

Straika wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang amefunga mabao 29 katika michuano yote aliyocheza msimu huu.

Lakini, amefunga mara nyingi zaidi kwenye Ligi Kuu England, akiweka wavuni mabao 20 ili kufukuzia Kiatu cha Dhahabu.

Katika kuisaka tuzo hiyo ya ufungaji bora, Aubameyang jana kwenye siku ya mwisho ya kumaliza msimu alikuwa ugenini kuwakabili Burnley na alihitaji kuendelea makali yake ya kufunga mabao pengine hata hat-trick kama alivyofanya katika Europa League Alhamisi iliyopita ili kuchukua usukani wa ufungaji bora na kukinyakua Kiatu cha Dhahabu hicho Ligi Kuu England.

Sadio Mane, Liverpool - mabao 20

Mechi ya mwisho: vs Wolves (nyumbani)

Staa wa Liverpool, Sadio Mane amekuwa na msimu mzuri sana hasa kwenye suala la kutumbukiza mipira wavuni. Kabla ya kushuka uwanjani huko Anfield jana Jumapili, Mane alikuwa tayari ameshatupia mabao 20 na aliingia uwanjani kuwakabili Wolves, kwanza akiwa na kazi kuipa ushindi timu yake ili wabebe ubingwa, pia kupiga mabao ya kumpa Kiatu cha Dhahabu Ligi Kuu England.

Katika ya mechi hiyo alikuwa amezidiwa mabao mawili na aliyekuwa kinara, hivyo Mane alihitaji kufunga hat-trick huku wenzake wengine wasifunge ili kuikamatia tuzo hiyo ya mfungaji bora kwenye ligi ya kibabe zaidi.

Jamie Vardy,

Leicester - mabao 18

Mechi ya mwisho: vs Chelsea (nyumbani)

Kabla ya jana, straika Jamie Vardy alikuwa amegfunga mabao 10 katika mechi 10 za mwisho, huku mabao tisa akifunga katika kipindi ambacho timu hiyo imekuwa chini ya Kocha Brendan Rodgers.

Katika siku ya kufunga msimu jana Jumapili, straika huyo alikuwa na kazi ya kuwakabili Chelsea uwanjani King Power.

Kushinda Kiatu cha Dhahabu cha msimu huu Vardy alihitaji kuwafunga Chelsea si chini ya mabao manne, kitu ambacho usingekitarajia kuwa chepesi kwa staa huyo hasa katika mechi ya mwisho ya msimu.

Rekodi nzuri kwake ni kwamba amekuwa na kasi nzuri ya kufunga tangu timu hiyo iwe chini ya kocha Brendan Rodgers.