Kepa wa Chelsea awaongoza makipa ghali zaidi duniani

Kepa Arrizabalaga.

Muktasari:

  • Klabu zote 20 zilikuwa bize kwenye kukamilisha dili zao kabla ya dirisha kufungwa jioni jana. Manchester United ilikuwa na uhitaji zaidi wa wachezaji, lakini kwa upande wao ilikuwa ishu ya kusubiri tu na kuona kitakachotokea.

LONDON, ENGLAND. DIRISHA la uhamisho wa wachezaji kwenye Ligi Kuu England lilifungwa jana Alhamisi saa 6:00 usiku kupisha kuanza kwa msimu mpya wa 2018/19 utakaoanza rasmi leo Ijumaa.

Klabu zote 20 zilikuwa bize kwenye kukamilisha dili zao kabla ya dirisha kufungwa jioni jana. Manchester United ilikuwa na uhitaji zaidi wa wachezaji, lakini kwa upande wao ilikuwa ishu ya kusubiri tu na kuona kitakachotokea.

Chelsea na Liverpool, wao walionekana kukamilisha dili zao baada ya kufanya usajili mkubwa kwenye dirisha hilo, ikiwamo kunasa huduma za makipa kwa pesa nyingi.

Liverpool ilivunja rekodi kwa kumnasa kipa Alisson Becker kutoka AS Roma, kabla ya Chelsea kuja kuvunja rekodi hiyo na kumsajili kipa kwa pesa nyingi zaidi ambayo haijawahi kutokea kwenye usajili wa kipa, wakati iliponasa Kepa Arrizabalaga kutoka Athletic Bilbao. Hii hapa ndio orodha ya makipa sita walionaswa kwa pesa nyingi zaidi duniani.

6.Bernd Leno – Pauni 19.3milioni

Kocha mpya wa Arsenal, Unai Emery, alionekana mwenye wasiwasi mkubwa na ndio maana alifanya uwekezaji mkubwa kikosini mwake.

Arsenal imesajili, lakini mastaa wake wapya si wenye viwango bora sana ukilinganisha na Naby Keita, Fred na Jorginho waliosajiliwa kwingineko. Emery katika usajili wake, upo pia wa kipa Bernd Leno, aliyemnasa kutoka Bayer Leverkusen kwa Pauni 19.3 milioni.

5.Jordan Pickford – Pauni 25milioni

Kocha Ronald Koeman hakufurahia nyakati njema huko Everton kama alivyokuwa Southampton. Hata hivyo, Mdachi huyo alikuwa mwenye furaha kubwa kwa kumshuhudia Jordan Pickford akitamba na England kwenye Kombe la Dunia 2018 huko Russia.

Kipa huyo alikuwa moja ya usajili wake kutoka Sunderland, wakati alipomnasa kwa Pauni 25 milioni. Kipa huyo ni uwekezaji mkubwa huko Everton kwa sababu umri wake ni miaka 24, hivyo ana miaka mingine 10 mbele ya kuendelea kutamba.

4.Gianluigi Buffon – Pauni 32.6 milioni

Gianluigi Buffon alinaswa na Juventus kutoka Parma mwaka 2001 kwa ada iliyoweka rekodi ya dunia wakati huo kwa upande wa makipa, Pauni 32.6 milioni. Ilikuwa pesa nyingi kulipwa kwa kipa na kutengeneza rekodi ambayo ilidumu hadi mwaka 2017 wakati Manchester City ilipolipa Pauni 34.7 milioni kumsajili Ederson kutoka Benfica. Juventus walimtumia Buffon kwa miaka mingi hadi hapo mwishoni mwa msimu uliopita walipomwaacha aende PSG.

3.Ederson- Pauni 34.7milioni

Baada ya kushindwa kuridhishwa na kiwango cha Joe Hart na kisha Claudio Bravo, Pep Guardiola aliamua kunasa kipa mwingine kwenye msimu wake wa pili klabuni Manchester City, wakati alipolipa Pauni 35 milioni kunasa huduma ya kipa wa Kibrazili, Ederson, ada ambayo ilivunja rekodi ya uhamisho wa makipa iliyokuwa imedumu kwa miaka mingi. Uwekezaji huo kwa kipa ulileta matunda kwani Man City ilibeba ubingwa wa Ligi Kuu England na Kombe la Ligi.

2.Alisson Becker- Pauni 67 milioni

Liverpool ilishtua ulimwengu baada ya kutoa Pauni 67 milioni kumsajili kipa Alisson Becker kutoka AS Roma mwezi uliopita. Jambo hilo lilimfanya kipa huyo wa Kibrazili kuwa ghali duniani.

Lakini, rekodi yake hiyo haikudumu muda mrefu, kwani Chelsea walikuja kuivunja mwezi mmoja tu baadaye wakati ilipolipa Pauni 72 milioni kusajili kipa.

Kwa msimu uliopita, Alisson alicheza mechi 37 kwenye Serie A, akaruhusu mabao 28 huku akiokoa hatari 109 na kucheza mechi 17 bila ya kuruhusu bao. David De Gea alichaguliwa kipa bora kwenye Ligi Kuu England kwa kucheza mechi 17 bila ya kuruhusu bao.

1.Kepa Arrizabalaga- Pauni 72 milioni

Chelsea ilifahamu kwamba kipa wake Thibaut Courtois anang’ang’ana kwenda Real Madrid. Jambo hilo liliwaweka kwenye wakati mgumu wa kutafuta mrithi wake huko Stamford Bridge. Wakajikuta wakianza kuhusishwa na makipa kadhaa akiwamo Jordan Pickford wa Everton na Jack Butland wa Stoke City.

Lakini, mwisho wa yote waliamua kulipa Pauni 72 milioni kumsajili kipa Kepa Arrizabalaga kutoka Athletic Bilbao na kumfanya kuwa kipa ghali zaidi duniani kwa sasa. Kipa huyo Mhispaniola amesaini mkataba wa miaka saba Stamford Bridge.