#KARIAKOODERBY: Lazima mtu anapigwa taifa

SIMBA na Al Ahly zishamalizana na habari ndo kama ile. Sasa picha linahamia Yanga dhidi ya Simba katika mchezo ambao nchi itasimama kwa siku kadhaa kupisha joto la mechi hiyo.

Ugumu au utata wa mchezo huo haupo tu kabla na ndani ya mchezo huo, lakini pia joto zaidi linaweza kuwa hata baada ya mechi kumalizika na kuleta mambo mengi tofauti. Ebu tuangalie katika mechi hii mambo gani yanaweza kutokea na kuleta hisia tofauti kufuatia presha baina timu zote mbili.

Aussems

kikaangoni

Endapo Simba ikipoteza mechi hii mtu wa kwanza atakayekaa sehemu ngumu ni Kocha wa Simba, Patrick Aussems. Viongozi, wanachama na mashabiki wa klabu hizi kubwa huwa hawataki kusumbua akili wala kukumbuka mazuri ya mtu hata kama amemfunga Al Ahly, Aussems anaweza kujikuta lawamani katika namna mbili mojawapo ikiwani upangaji wa kikosi chake.

Presha ya Kakolanya

kuibuka

Yanga itaingia katika mchezo huo ikiwa na kipa, Ramadhan Kabwili anayeweza kukaa langoni kufuatia klabu hiyo kugoma kumrudisha kipa wake namba moja, Benno Kakolanya.

Kundi kubwa la wanachama na hata mashabiki wamekubali msimamo wa kocha wao, Mwinyi Zahera kutomrudisha Kakolanya lakini wapo pia ambao wanakubali kwa kulazimishwa, endapo Yanga itapoteza kundi la wanaomkubali Kakolanya linaweza kurudi na kuanza kuleta joto zito.

Mashabiki wa Simba kujaa

Simba wanaweza kuwa wengi zaidi uwanjani kuwashinda wenzao wa Yanga sababu ya kujaa kwao ni kutokana na imani ya kikosi chao. Kimeifunga Al Ahly siku chache zilizopita, kimeanza kula viporo vyake lakini kwa upande wa Yanga bado hawaimanini sana timu yao kutokana na kutofanya vizuri katika mechi za hivi karibuni.

Mtu anapigwa au sare

Mechi hii matokeo ya kwanza yanayoweza kutokea ni timu moja kupoteza. Ndiyo kuna timu inaweza kupoteza kulingana na itakavyojipanga lakini pia matokeo ya mwisho ni kutoa sare.

Presha ya uchaguzi

Yanga

Vuguvugu la Uchaguzi wa Yanga limetulia kwasasa baada ya mchakato kusimama lakini endapo Yanga ikipoteza presha hiyo inaweza kurudi kwa kasi na kuleta filamu mpya ndani ya klabu hiyo.

Zahera yuko salama

Yanga ikipoteza haitaweza kumuacha kocha wake Zahera na sababu ni moja tu, hali ya klabu hiyo ilivyo kwasasa. Mambo yanavyo kwenda Zahera ndiye kila kitu akiibeba mabegani na kama atapoteza jibu lake litakuwa moja tu, kujificha katika kivuli cha ukata na kikosi chepesi.