Inakuwaje Cannavaro aagwe kirahisi hivi?

Friday August 10 2018

 

By CHARLES ABEL

NDANI ya Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro keshokutwa Jumapili, Yanga itamuaga rasmi nahodha wake wa muda mrefu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye sasa atabeba majukumu mengine. Anakua Meneja wa timu hiyo.

Baada ya kuichezea timu hiyo kwa mafanikio kwa miaka 15, hatimaye Cannavaro amekubali kutundika daluga na kuingia kwenye majukumu ya kiofisi zaidi. Anatoka uwanjani anaingia ofisini.

Mataji na mafanikio aliyoyapata akiwa na Yanga kwa muda wote huo, yanamfanya Cannavaro kuwa miongoni mwa wachezaji wachache ambao klabu hiyo inaweza kuwaweka kwenye orodha yake ya mastaa wa muda wote kwenye historia ya Yanga.

Akiwa na Yanga, Cannavaro ameshinda mataji manane ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ana medali mbili za dhahabu za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), ametwaa Ngao ya Jamii mara tano, medali moja ya ubingwa wa Kombe la FA.

Pia ameiongoza Yanga kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili.

Kuna mafanikio gani tena mengine ambayo yanaweza kukufanya umwondoe Cannavaro katika historia ya Yanga zaidi ya haya aliyoyapata kwa muda wote aliocheza Jangwani?

Inavyoonekana Cannavaro anaweza kuingia kwenye kundi la nyota watano ambao wameshinda idadi kubwa ya mabao wakiwa na kikosi cha timu hiyo kama kumbukumbu zangu zitakuwa zinaenda sawa.

Ondoa mchango wake ndani ya Yanga. Cannavaro pia alikuwa mchezaji tegemeo wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ aliyokuwa nahodha wake pia kwa muda mrefu kabla ya kujiondoa kwenye nafasi hiyo mwaka juzi.

Alikuwemo kwenye kikosi cha Stars ambacho kilifuzu mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN).

Kwa mchango na mafanikio aliyoyapata kwenye soka la Tanzania, tukio la kumuaga kwake baada ya kustaafu soka lilipaswa kufanywa kuwa kubwa na lenye hadhi na uzito wa hali ya juu kwa nchi nzima likihusisha kundi kubwa la watu ambao kwa namna moja au nyingine Cannavaro aligusa hisia zao pindi alipokuwa anacheza.

Ni tukio ambalo lilipaswa kuteka vyombo vyote hapa nchini kwani mbali ya mchango na mafanikio yake ndani ya uwanja, Cannavaro alikuwa ni miongoni mwa wachezaji wachache ambao wana mahusiano mazuri na wanahabari.

Nilitegemea kuona mechi ya kumuaga Cannavaro ihusishe kundi kubwa la mastaa wa soka kutoka ndani na nje ya nchi ambao waliwahi kucheza naye pamoja au kukabiliana na beki huyo kwenye mechi za mashindano tofauti.

Kwa bahati mbaya, mechi ya kumwaga Cannavaro imechukuliwa kama tukio la kawaida na ule uzito na thamani yake unaonekana wazi hautokuwepo.

Cannavaro ataagwa kwenye Uwanja wa Jamhuri kwa mchezo ambao utaihusisha Yanga na timu ya Mawenzi Market ya Morogoro inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Sitaki kuwakosea heshima Mawenzi Market, lakini mechi hii inapoteza uzito wa tukio lenyewe la kumuaga Cannavaro na matokeo yake inaonekana kama ni kwa ajili ya kuipima nguvu Yanga kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu msimu ujao. Hivyo ni vyema ingetangazwa kama mechi ya kirafiki tu.

Kwa mchezaji kama yeye ambaye alikuwa staa ndani ya Yanga na Taifa Stars, alipaswa angalau kuagwa kwa mchezo ambao ungehusisha timu mbili tofauti ambazo angeziteua yeye mwenyewe.

Timu moja ingeteuliwa kutokana na wachezaji aliowahi kucheza nao Yanga kwa kipindi cha zaidi ya miaka 12 aliyoichezea klabu hiyo ambacho kingecheza na kikosi kingine ambacho angekiunda kwa kuteua wachezaji aliowahi kucheza nao Taifa Stars.

Ilipaswa mechi hiyo angalau ichezwe kwenye Uwanja wa Taifa, kwani sehemu kubwa ya maisha ya Cannavaro tangu aliposajiliwa na Yanga yalikuwa Dar es Salaam, lakini haitoshi bado ilitakiwa kuwekwe kiingilio cha chini ili kuwapa fursa idadi kubwa ya mashabiki kumuaga beki huyo.

Mwisho wa siku wahusika wameshindwa kugundua fursa ambazo wangeweza kuzipata kutokana na tukio la kumuaga Cannavaro na matokeo yake wameamua kulirahisisha kwa kuligeuza mechi ya kupasha misuli.