Huyu Ninja bado ananishangaza

Katika mchezo uliokuwa mgumu huku ukigubikwa na matukio ya hapa na pale, Kamera za Azam TV zilimuonyesha beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ akimpiga kiwiko mchezaji mmoja wa Coastal Union.

Ninja alikuwa anamiliki mpira na mchezaji wa Coastal alikuwa nyuma yake lakini ghafla beki huyo wa Yanga akimpiga kiwiko.

Hakujali kama angeonyeshwa kadi nyekundu. Hakujali sana kuhusu mwamuzi wa kati ambaye huwa hawi umbali mrefu na mahali uliko mpira wala hakuonekana kuhofia sana mwamuzi wa pembeni kama ataweza kumuona na kumuadhibu kwa tukio hilo.

Bahati nzuri kwake alifanikiwa kumaliza mechi bila kuonyeshwa kadi nyekundu kutokana na waamuzi kutomwona lakini pasipo kujua, alikuwa anajiweka kwenye hatari kubwa ya kukutana na adhabu ya kufungiwa mechi zisizopungua tatu na faini ya fedha.

Katika michezo hiyo mitatu ambayo iwapo angekutana na adhabu hiyo ambayo hadi sasa haijatolewa, mmojawapo ni ule wa kesho dhidi ya Watani wao wa jadi, Simba ambao ndio huteka hisia za wadau wa soka hapa nchini.

Hakuonekana kujali kuhusu mechi ya watani na aliamua kumpiga kiwiko mwenzake ambaye hakuonekana kuwa na madhara kwake. Pengine alitukanwa na huyo mchezaji lakini hiyo siyo sababu ya kujitetea kwa kosa alilofanya.

Kwanza alijiweka kwenye hatari ya kuonyeshwa kadi nyekundu. Lakini pia angekuwa hatarini kufungiwa na kutozwa faini ingawa kubwa zaidi ni kuwa alikuwa anahatarisha usalama wa mchezaji mwenzake.

Tabia kama hiyo iliyoonyeshwa na Ninja imeonekana kuanza kuwa sugu miongoni mwa wachezaji wa Kitanzania na iwapo hatua za dhati zisipochukuliwa inaweza kuharibu taswira ya mpira wetu na kuhatarisha usalama wachezaji. Ilitokea kwa Erasto Nyoni kumchapa ngumi mchezaji wa Ndanda akafungiwa.

Ikafuatia kwa John Bocco aliyempiga mchezaji wa Mwadui FC naye akafungiwa na katika hali ya kushangaza ikatokea kwa Mrisho Ngassa na rafiki yangu Laurian Mpalile ambao walipiga vichwa wenzao katika mchezo baina ya Yanga na Prisons kule Mbeya mwaka jana. Badala ya wachezaji kujutia na kubadilika, tumeshuhudia Ninja naye akiingia kwenye rekodi ya utovu wa nidhamu kama walivyofanya wenzake.

Kwa bahati mbaya matukio hayo yanatokea katika mazingira ambayo mchezaji husika anakuwa hayupo kwenye mazingira hatarishi wala sababu ya kufanya hivyo.

Inavyoonekana wachezaji wetu wanajifunza na kufanyia kazi utovu wa nidhamu badala ya mambo mazuri ambayo yatawafikisha mbali kisoka. Inashangaza sana.