Hii Mtibwa Sugar inauza, inarudisha

Friday August 10 2018

 

By MWANAHIBA RICHARD

KATIKA timu za soka za Ligi Kuu Bara, wachezaji wamekuwa wakiingia na kutoka kupitia madirisha ya usajili; lile kubwa la mwanzoni mwa msimu na pia lile dogo la katikati ya msimu.

Kupitia madirisha haya, timu nyingi zimekuwa zikiachana na wachezaji kwa maelezo mbalimbali lakini kwa wengi wao huelezwa ni kwa sababu ya kushuka viwango vya kiufundi na hata kinidhamu ambapo nafasi za wanaoachwa hujazwa kwa kusajiliwa wengine. Katika timu nyingi hali ni hiyo ya ‘ingia toka’.

Lakini wakati mambo yakiwa hivyo pia hata kwa klabu kongwe za Simba na Yanga, mambo yamekuwa tofauti kwa Mtibwa Sugar, yenye maskani yake Uwanja wa Manungu, ulio katikati ya mashamba ya miwa katika mji mdogo wa Turiani, wilayani Mvomero, mkoani Morogoro.

Ukiziondoa Simba na Yanga, Wakata Miwa hao ndio timu pekee nyingine yenye rekodi ya kucheza ligi hiyo kwa miaka mingi mfululizo bila kushuka wala kunusurika kufanya hivyo tangu ilipopanda daraja kutinga Ligi Kuu mwaka 1996 (wakati huo ikiitwa Ligi Daraja la Kwanza), na ikiibuka na ubingwa mara mbili mfululizo, mwaka 1999 na 2000.

Ndiyo, Mtibwa, unaweza kuiita ‘chuo cha soka’. Ni kwa sababu timu hiyo imejipambanua kwa tabia yake ya kukuza vijana kuanzia chini na kusalia nao kwa muda mrefu ikiwapandisha hadi timu ya wakubwa. Kwa asilimia kubwa wachezaji wanaoondoka Mtibwa ni wale wanaouzwa, ndio maana hata Simba na Yanga zinaponea matunda ya Mtibwa.

Sifa kubwa ya Mtibwa katika ligi ni kulea vijana na kuwatumia, baadaye huuzwa ingawa si kwa kiasi kikubwa cha pesa, pengine hiyo inatokana na wamiliki wake kutokuwa na tamaa na pesa. Hawapendi kuwabania wachezaji wanapopata nafasi ya kusajiliwa kwingine.

Pia ukiiondoa Azam FC yenye miaka kumi tu kwenye ligi ma inayoenda kwa mfumo wa kisasa, Mtibwa bado inabaki kuwa timu kongwe yenye kuwatunza vizuri wachezaji wake kuanzia katika mishahara, lishe bora, matibabu na hata mfumo wa uendeshaji ikiwa na uwanja wa uhakika sambamba na vifaa vya mazoezi.

Ndio maana kuna wachezaji kadhaa waliondoka Mtibwa na kujiunga na klabu nyingine, lakini baadaye viwango vyao vikashuka huko pengine kwa kukosa matunzo na mafunzo bora, wakaona hakuna pengine pa kwenda, wakarudi Manungu. Wakapokewa na wakarejea tena katika viwango vya ubora.

Katika kundi hili kuna wachezaji kama vile Shaban Nditi, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na Shaaban Kado. Walitoka na wakarudi.

Katika makala hii, Mwanaspoti linakuletea baadhi ya wachezaji ambao sasa wamelazimika kurejea Mtibwa wakiwania kupandisha tena viwango vyao kutokana na mfumo bora uliopo katika klabu hiyo.

Juma Liuzio

Julai 2014, Juma Liuzio, alisajiliwa na Zesco United ya Zambia akitokea Mtibwa. Usajili wake kwa wakati huo ndiyo uliokuwa ghali kwani Zesco ilimsainisha mkataba wa miaka mitatu uliokuwa na thamani ya Sh60 milioni.

Wakati Liuzio akivuna kitita hicho, Mtibwa ililipwa dola 70,000 kwa ajili ya kuvunja mkataba wa mchezaji huyo uliokuwa umebakiza miaka miwili kati ya mitatu iliyosainiwa.

Liuzio alikianza vyema kibarua chake Zambia, lakini miezi michache baadaye akaanza kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara kiasi cha kupoteza namba. Akaamua kurudi nchini na akatua Simba kwa mkopo na bado hakurejesha makali na msimu uliopita akakumbana na mastraika wakali John Bocco na Emmanuel Okwi.

Liuzio sasa amerudi nyumbani, anajipanga kwa ajili ya msimu mpya pamoja na michuano ya kimataifa ambapo timu yake itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika. Hayatakuwa maisha mapya kwake ndani ya Mtibwa, lakini amegundua hapo ndipo sahihi kwa soka lake.

Ally Shomary

Hakika kabla ya kutua Simba beki huyu wa kulia alikuwa moto wa kuotea mbali, uwezo wake uliwashawishi Wekundu wa Msimbazi kumng’oa Mtibwa na kumpa mkataba wa miaka miwili kuwa mbadala wa Hassan Kessy.

Alikuwa akipata nafasi mwanzoni lakini tangu kocha Joseph Omog atoke Simba mambo yakabaki kuwa historia,akahamia benchi akinyanyaswa na akina Shomari Kapombe, Erasto Nyoni na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Shomary amesoma alama za nyakati na kuomba kurudi Mtibwa kwa mkopo. Kurejea kwake Mtibwa ni kama kumtumbukiza chura bwawani kwani ni timu iliyomlea tangu ajiunge nayo akitokea Moro Kids, kituo kilicholea nyota kibao wa soka nchini.

Mtibwa imempokea Shomary ikiamini bado ana uwezo ingawa sasa atakuwa akigombea namba na Mbwana Shomary. Uzoefu unaweza kumbeba lakini akiumudu upinzani wa Salum Kanoni.

Jaffary Kibaya

Ni winga ambaye hakuwa na msimu mbaya alipoichezea Kagera Sugar, ingawa alikumbwa na hali ya kuwa majeruhi mara kadhaa na hivyo kuzikosa baadhi ya mechi.

Sasa ameamua kurudi Mtibwa, alipowahi kucheza miaka ya nyuma, ni timu iliyomlea hivyo anaifahamu vizuri pengine kuliko timu nyingine.

Hata hivyo ana mtihani wa kuwapiku Haroun Chanongo na Salum Kihimbwa katika kikosi cha kocha, Zuberi Katwila.

Awadh Juma

Ni kiungo ambaye alipoondoka Mtibwa alijiunga na Simba kisha akaenda Madui FC na sasa amerejea nyumbani Manungu. Hapo amekuta viungo wengine, lakini ubora wake unaweza kumpa nafasi kwani viungo wakali waliokuwapo hapo, Mohamed Banka na Hassan Dilunga, wameoondoka hapo.

Banka amesajiliwa Yanga wakati Dilunga katua Simba. Changamoto ya Awadh kupata namba sasa ni dhidi ya Ayoub Semtawa na Ally Makarani, lakini yeye ana faida ya uzoefu.

Hussein Javu

Alipoondoka Mtibwa alisajiliwa na Yanga. Mambo hayakumwendea vizuri huko na hivyo mshambuliaji huyo akahamia JKT Ruvu ambako alicheza kwa muda mfupi na kurudi Mtibwa.

Pamoja na Javu pamoja na kiwango chake kuwa juu atakumbana na changamoto ya namba kutoka kwa Liuzio ambaye amerudi kikosini pamoja na Riphat Hamis.