Cheki teknolojia mpya inavyobamba kwenye soka

LONDON, ENGLAND. HIVI ndivyo maisha yanavyokwenda kasi. Teknolojia inabeba kila kitu.

Unajua kwa sasa wanasoka mastaa wanaowasoma wapinzani wao kwa kupitia simu tu?

Huko kwenye Ligi Kuu England, masupastaa kama Willian wa Chelsea na Romelu Lukaku wa Manchester United wamekuwa wakitumia uchambuzi wa video unaopatikana kwenye App ya Wyscout kusoma udhaifu wa wapinzani wao kabla ya kwenda kukabiliana nao uwanjani.

Mastaa hao wanapata kila kitu kupitia simu zao. Wyscout inatoa nafasi kwa wachezaji kutazama video ya uchambuzi mwingine wa kitakwimu kufahamu nguvu ya wapinzani wao kabla ya kukabiliana nao.

Makocha kwa sasa hawana sababu ya muhimu tena kusafiri umbali mrefu kwenda kutazama mechi ya wapinzani ili kutambua wanachezaje. Kila kitu kimekuwa rahisi kupatikana.

App hiyo ilizinduliwa mwaka 2004 ikiwa na lengo ya kuzisaidia klabu kutambua wachezaji mbalimbali duniani kote ili kuwasajili, huku ikifanya shughuli za wale wasaka vipaji kuwa hafifu kwa sababu makocha wanawaona wachezaji wanaowataka kuwasajili kupitia kwenye teknolojia hiyo.

Leicester City ilitumia teknolojia hiyo kumfuatilia Riyad Mahrez kabla ya kumsajili mwaka 2014, sawa na Genoa ilivyotumia Wyscout kusoma maelezo ya straika, Krzysztof Piatek. Straika huyo wa zamani wa Cracovia alinaswa na Genoa kwa Pauni 4 milioni tu kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana kabla ya kuuzwa kwa Pauni 31 milioni miezi sita baadaye kwenda AC Milan.

Kwenye App hiyo kuna maelezo ya wachezaji zaidi ya 550,000 na video za uchambuzi wa mechi zaidi ya 1,800 zinawekwa kila wiki kuwafanya wachezaji wenyewe, makocha na mawakala mbalimbali kutazama na kuona mchezaji gani wanataka kumsajili au kutambua nguvu za wapinzani wao uwanjani. Klabu mbalimbali za soka zimekuwa zikitumia Wyscout kuweka maelezo yao ya kabla na baada ya mechi.

Wachezaji wengi wamekuwa wakitumia App hiyo kutambua kitu gani cha kwenda kufanya uwanjani, mpinzani anayekwenda kukabiliana naye na mbinu za kocha wa timu pinzani. Miongoni mwa wachezaji wanaotumikia teknolojia hiyo ni staa, Zlatan Ibrahimovic.

App hiyo ina video mbalimbali za mechi na mazoezi, ambayo yanawafanya wachezaji na mabenchi ya ufundi kutambua namna ya kukabiliana na wapinzani. Kwenye Ligi Kuu England, Mbrazili, Willian ndiye anayeongoza kwa kutumia teknolojia hiyo sambamba na Lomelu Lukaku.

Straika Lukaku wakati mwingine amekuwa akitumia App hiyo kufuatialia maendeleo ya mdogo wake, Jordan, anayekipiga beki wa kushoto huko Lazio.

“Natazama mechi zote za mdogo wangu kupitia Wyscout: mapambano yake yote ya ana kwa ana, anavyokaba na anavyoshambulia,” alisema Lukaku.

Mastaa wa Italia wanaotumia teknolojia hiyo ni pamoja na magwiji wa Juventus, Giorgio Chiellini, 34, na Andrea Barzagli, 37. Pamoja na uhodari wa mabeki hao, wamekuwa wakitumia App hiyo kuwapeleleza washambuliaji wanaokuja kukabiliana nao, wanachezaje, staili zao za chenga na kama wanapenda kupiga mashuti wakiwa mbali au hawafungi hadi waingie ndani ya boksi.

Mario Balotelli ni staa mwingine anayetumia teknolojia hiyo kuwasoma wapinzani wake. Straika huyo mtukutu, amewahi kuzichezea Manchester City na Liverpool kwenye Ligi Kuu Englandn na Inter na AC Milan huko kwenye Serie A kabla ya kutimkia Ufaransa alikocheza Nice na baadaye kujiunga nja Marseille.

“Anatumia sana Wyscout,” ilisemwa kuhusu Balotelli.

“Watu wanadhani Balotelli ni mtu anayechezacheza tu. Hapana. Anajifunza sana.”

App hiyo inatoa uchambuzi mbalimbali wa kuhusu namna ya kupiga kwa ustadi mkubwa mipira ya adhabu pamoja na kona na hata kurusha mipira pia. Kwa kifupi, ukiwa na App hiyo pengine unaweza hata usihitaji kocha, unatazama tu video na data mbalimbali na kujifunza mwenyewe mbinu za kisoka uwanjani.

Katika fainali za Kombe la Dunia 2018, timu nyingi sana zilitumia App hiyo kujifunza namna wapinzani wao wanavyocheza pamoja na kumtazama mchezaji mmojammoja umahiri na udhaifu wake. Hata waamuzi pia wamekuwa wakitumia teknolojia hiyo kuwatambua wachezaji kwenye mechi wanazokwenda kuziamua, ili kukwepa kufanya uamuzi utakaoharibu utamu wa mchezo husika.