Cannavaro aonekana mguuni kwa Ninja

NADIR Haroub ‘Cannavaro’ tofauti yake na Shaibu Abdallah ‘Ninja’ ambaye alimrisisha jezi aliyokuwa anaitumia ni umbo la mwili wake na umri.

Aina ya ufundi ama staili ya uchezaji wa Ninja ni kama anafuata nyendo za Cannavaro ambaye amestafu soka mwanzoni mwa msimu huu, na baadaye uongozi wa Yanga uliandaa mechi ya kumuaga dhidi ya Mawenzi Markert ilichezwa mkoani Morogoro.

Inaonyesha Cannavaro alitambua mapema madini yaliopo mguuni kwa Ninja akaamua kumpa jezi ili kudumisha alichokifanya enzi zake.

Mwanaspoti limebaini baadhi ya vitu ambavyo Ninja amefanana na Cannavaro na ambavyo atatakiwa kufanya kazi ya ziada ili afiti viatu vyake asilimia 100.

WAJIBU WA ENEO LAKE

Ninja hana kulemba mpira unapokuwa eneo lao la hatari, kazi yake amekuwa akiuondoa bila kufanya madoido, ndivyo alivyokuwa Cannavaro ambaye alikuwa makini kuhakikisha wapinzani hawadumu ndani ya 18.

Ukiachana na umakini wa kuondosha mipira langoni kwao, Ninja aina ya upigaji pasi hautofautiani sana na Cannavaro na namna anavyokimbia pindi timu inapokuwa haina mpira kuusaka ili uwe kwenye miliki yao.

Amekuwa mwepesi wa kurudi kukaba inapotokea amekuwa mbali na eneo lake na sio mtegezi wa kusubiri mwingine kuokoa hatari anapopata nafasi amekuwa akiondosha mipira bila mambo mengi ya kutaka kucheza na jukwaa kama ilivyo kwa wengine wanaopenda kupigiwa makofi na miluzi na mashabiki wao.

MIPIRA YA VICHWA

Cannavaro alikuwa mtaalamu wa kuokoa mipira ya juu kwa kutumia kichwa na wakati mwingine kufunga hasa kwa mpira wa kona, jambo hilo limeonekana kwa Ninja akitumia staili hiyo hiyo katika kuokoa hatari hasa wapinzani wakipiga mipira ya juu ingawa wakati mwingine amekuwa ikimgharimu.

KUJITUMA

Ninja hachezi mbali na staili alizokuwa anatumia Cannavaro, anajituma kwa muda anaoaminiwa na kocha amekuwa akionyesha uzalendo wa kuona timu yake inakuwa inabaki salama ndani ya dakika 90 ingawa matokeo ni ya aina tatu kufungwa, ushindi na sare.

Si mchezaji wa kulazimishwa na kocha kufanya majukumu yake awapo uwanjani amekuwa akifanya majukumu kikamilifu na msikivu anaposhauriwa.

Amewahi kukaririwa akisema “Cannavaro ni mfano wa kuiga kutokana na kazi aliyoifanya kwenye klabu ya Yanga na timu ya taifa, ameacha rekodi ya kuheshimika, natamani kuifikia” kauli ya Ninja.

VITU HIVI AVIFANYIE KAZI

Cannavaro alikuwa kiongozi wa wachezaji wenzake uwanjani, alikuwa mwepesi wa kutuliza hasira ama jaziba pindi ilipokuwa ikitokea sintofahamu katikati ya mechi.

Kuna wakati Ninja amekuwa na jaziba zinazompelekea wakati mwingine kupata kadi za adhabu jambo linalompasa alifanyie kazi ili kiwango chake kiendelee kuinufaisha Yanga.

NIDHAMU

Nidhamu ya hali ya juu ambayo alikuwa akiionyesha Cannavaro ndio iliomfanya adumu na unahodha kwa muda mrefu mpaka alipostafu na kuuacha mikononi mwa Kelvin Yondan ambaye hata hivyo hajadumu nao, kocha Mwinyi Zahera alimvua na kumkabidhi madaraka kwa Ibrahim Ajib.

Ninja jezi anayoitumia atapaswa kupambana ili aweze kuyafikia aliyokuwa anayafanya Cannavaro itamlazimu kuwa na nidhamu ya hali ya juu ili siku moja aje kuvaa beji ya unahodha kama kutimiza ama kutunza heshima ya jezi anayotumia.

UZOEFU

Cannavaro alikuwa mchezaji mzoefu kutokana na kucheza kwa muda mrefu, kujitunza kwa Ninja na akizingatia miiko ya kazi yake atafikia kile ambacho alikifanya staa na nahodha wa zamani wa timu hiyo aliyemkabidhi kijiti cha jezi.

KAULI YA CANNAVARO

“Ninja ni mchezaji mzuri jambo la msingi ni kuzingatia miiko ya kazi yake pia ajitume kwa bidii ili aweze kufika mbali zaidi na aje afaidi matunda ya kipaji chake kwa sababu umri nao bado uinamruhusu kupambana,” anasema.