Alliance imetuelewa, sasa tunaielewa

Friday February 8 2019

 

By CHARLES ABEL

Alliance FC walianza Ligi Kuu msimu huu vibaya na kila mmoja alianza kuhisi watashuka daraja mapema

Nakumbuka katika mechi sita za mwanzo, walipoteza michezo mitano na kupata sare moja tu na katika mechi hizo tano walizofungwa, mbili ilikuwa ni kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Ilifika hatua watu ndani ya timu hiyo walitaka kuanza kumsaka mchawi anayesababishwa wafanye vibaya kwenye Ligi Kuu.

Wachache wanaoamini siasa za mpira wa wetu, walidhani kuwa ndani ya Alliance au jiji la Mwanza, kuna wasaliti ambao wanaihujumu timu hiyo ili ifanye vibaya kwenye Ligi Kuu.

Hata hivyo, kiini cha matatizo ya Alliance wala hakikuwa ni uwepo wa usaliti ndani ya timu, uwezo mdogo wa makocha waliokuwa wanainoa wala kiwango kibovu ndani ya uwanja bali ni uwepo wa kundi kubwa la wachezaji ambao hawakuwa na uzoefu wa Ligi Kuu.

Alliance ilikuwa ikitumia kundi kubwa la wachezaji ambao hawajapevuka hivyo walipata wakati mgumu kukabiliana na timu zenye uzoefu wa ligi ingawa ndani ya uwanja imekuwa ikionyesha kiwango bora kwenye kila mchezo.

Kwa bahati nzuri wakati wa dirisha dogo la usajili, uongozi wa Alliance FC ulipokea kwa mtazamo chanya ushauri iliopewa wa kuongeza wachezaji kadhaa wazoefu ili wawe chachu ya kuwaongoza vijana waliopo waweze kufanya vizuri.

Waliongezwa Hussein Javu, kipa John Mwenda, kiungo kiraka Paulo Maona na mshambuliaji Blaise Bigirimana kutoka Burundi ambao wote waliingizwa na kocha Malale Hamsini, moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza.

Matunda ya usajili huo yameonekana kwani kwa sasa imekuwa ikifanya vizuri na haijapoteza jumla ya mechi tisa ilizocheza hivi karibuni na kubwa zaidi imejiondoa kwenye kundi la timu zinazopigania kubaki Ligi Kuu.

Pengine Alliance wasingefuata ushauri wa kusajili wachezaji wazoefu, leo wangekuwa wanaendelea kukabana koo na akina Biashara United na African Lyon kule mkiani mwa msimamo wa ligi.

Hata hivyo, kwa vile ilifanyia kazi hilo, leo wanavuna matunda ya kuheshimu kile walichoshauriwa.

Kiufupi wananufaika na mbegu ya usikivu waliyopanda wakati wa dirisha dogo la usajili.