Sajili za kibabe Jose Mourinho hakuna kulala United

Tuesday August 7 2018

 

HAKUNA furaha kabisa kwenye korido za Old Trafford huku uhisiano wa Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho na Mtendaji Mkuu wake, Ed Woodward ukionekana kutikisika.

Kipigo kutoka kwa Bayern Munich pale Allianz Arena, Ujerumani, juzi Jumamosi usiku nacho kimeongeza wingu zito huku Mourinho akionekana kuanza kukata tamaa kama anaweza kupambana na mahasimu wake, Manchester City, Chelsea na Liverpoo ambao wamevunja benki kunasa mastaa wa maana kwa ajili ya kusaka ubingwa.

Mourinho na jeshi lake wamemaliza ratiba yake ya kujifua, anajiandaa kuingia kwenye msimu wa tatu akiwa na Man United huku akiwa tayari amewanasa wachezaji watatu, kiungo wa Kibrazili, Fred, beki Diogo Dalot na kipa Lee Grant.

Hata hivyo, kabla ya msimu uliopita kumalizika Mourinho aliahidi kuingia sokoni kwa kushindo ili kukisuka upya kikosi chake, lakini mambo yanaonekana kuwa bado magumu.

Ishu ya kiungo Paul Pogba inaonekana kuwa moto zaidi baada ya wakala wake, Mino Raiola kutua jijini Manchester kujaribu kuishawishi United imuuze mteja wake kwa Barcelona huku Anthony Martial, akitaka kuondoka kwenda Chelsea ama Tottenham.

Lakini taarifa mpya na ambazo zitawapa mzuka mashabiki wa Man United ni kwamba, Mourinho na Woodward wanapanga kufanya kufuru huku zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya dirisha la usajili kufungwa rasmi keshokutwa Alhamisi.

Mourinho ameeleza, wamekuwa kwenye harakati nyingi na Woodward na kwamba, kabla ya kuanza kampeni za Ligi Kuu England kwa kuvaana na Leicester City, Ijumaa, atakuwa amewanasa mastaa watatu wa maana.

“Bosi wangu (Ed Woodward) anafahamu ni kitu gani ninataka kwenye kikosi changu kwa muda mrefu, nafahamu anafanya jitihada nyingi kwa ajili yangu hivyo, tusubiri kuona kitu gani kitatokea kabla ya dirisha kufungwa,” Mourinho amekiambia Kituo cha MUTV, baada ya mchezo waliopoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Bayern Munich.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya mastaa ambao Mourinho na Woodward wanapambana kwa sasa kuhakikisha wanazinasa saini zao kabla ya dirisha kufungwa rasmi Alhamisi.

WILLIAN

- Chelsea

Winga wa Brazil anayekipiga Chelsea, Willan amekuwa kipenzi cha Mourinho kwa muda mrefu na ndiye aliyemsajili Chelsea akitokea Shakhtar Donetsk mwaka 2013.

Licha ya kwamba, kuna taarifa kuwa Willian amechagua kubaki Stamford Bridge kwa msimu mwingine zaidi, lakini winga huyo amekuwa akisakwa na Mourinho kwa muda mrefu sasa na taarifa mpya ni kuwa, mabosi wa Chelsea na United wanajaribu kuangalia uwezekano wa kuingia dili la kubadilisha wachezaji. Mabosi wa Chelsea wamekuwa wakimhusudu winga wa Man United, Anthony Martial.

HARRY MAGUIRE

- Leicester City

Kiwango alichokionyesha beki huyu wa Leicester City kimemkuna sana Mourinho na sasa anataka kumshusha Old Trafford kuungana na wakali wengine kama Eric Bailly, Victor Lindelof, Chris Smalling, Marcos Rojo na Phil Jones ambao wanaunda ukuta wa United.

Lakini kwa sasa mabeki hao wanasumbuliwa na majeruhi na Mourinho anamsaka kwa nguvu zote Maguire ili kusaidia kumlinda De Gea pale langoni mwake. Leicester iko tayari kumuachia beki huyo, lakini inataka dau la Pauni 65 milioni huku mwenyewe akieleza kuwa, ni bahati kubwa kupata nafasi ya kukipiga United.

IVAN PERISIC

- Inter

Martial ndio ameshamtibua Mourinho na winga wa Inter Milan, Ivan Perisic ndiye chaguo la Mreno huyo, ambaye kama akitua basi kazi ya Romelu Lukaku itakuwa kupasia tu nyavuni.

Perisic ni bonge la fundi na uwezo wake uliiwezesha Croatia kushika nafasi ya pili kwenye Kombe la Dunia 2018, lakini Milan imekuwa ikitaka dau kubwa ili kumruhusu kwenda kujiunga na Mourinho.

TOBY ALDERWEIRELD

- Tottenham

Tayari Manchester United na Spurs zimekubaliana kufanya biashara ya Toby Alderweireld, ambaye alikuwa mchezaji wa kwanza kabisa kuhusishwa na uhamisho wa kwenda Old Trafford.

Toby ana uwezo wa kucheza kama beki wa pembeni au kati na muda mrefu alikuwa akitajwa kwenda kuchukua nafasi ya Luke Shaw, ambaye amekuwa majeruhi mara kwa mara.

Kwa sasa yuko kwenye mwaka wa mwisho wa mkataba wake na hilo limemfanya Kocha Mauricio Pochettino, kuridhia kupigwa bei.

Hata hivyo, mabosi wa United wapo tayari kulipa dau ambalo halitazidi Pauni 50 milioni huku Mtendaji Mkuu wa Spurs, Daniel Levy, ambaye ni bingwa wa kufanya biashara akitaka Pauni 70 milioni.

Jerome Boateng-Bayern Munich

Baada ya kuchapwa bao 1-0 juzi usiku, mabosi wa Manchester United wakaanzisha mazungumzo na wenzao wa Bayern Munich kuhusiana na saini ya Jerome Boateng.

Boateng, ambaye dili lake kwenda PSG limekwama, haonekani kuwa na furaha na dau lake limetajwa kuwa ni Pauni 45 milioni huku rapa maarufu duniani, Jay Z akihusika na mpango mzima wa biashara hiyo.

Hata hivyo, United inataka kupunguziwa bei ya Boateng, ambaye mwezi ujao atafikisha miaka 30. Beki huyo wa kati anasimamiwa kazi zake na Kampuni ya Roc Nation Sports inayomilikiwa na Jay Z.

Yerry Mina

-Barcelona

Taarifa ni kuwa Everton wamekubali kulipa dau la Pauni 28.5 milioni kwa ajili ya huduma ya beki wa kati wa Colombia, Yerry Mina kutoka Barcelona kutokana na mazungumzo na Man United kukwama.

Hata hivyo, Mourinho bado hajapoteza dhamira yake ya kusaka saini ya Mina, ambaye alikuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Colombia kule Russia 2018.

Advertisement