Mashabiki Simba, Yanga wawe na heshima na ustaarabu Taifa

Muktasari:

  • Mchezo huo ambao ni mwendelezo wa Ligi Kuu Bara ikiwa ni raundi ya sita, umevuta hisia za mashabiki wengi kutokana na ubora wa vikosi vyote viwili kwa msimu.

KWA takribani wiki sasa soka la Bongo limekuwa na hamasa kubwa kutokana na kukaribia kabisa kwa mtanange wa watani wa jadi, Simba na Yanga. Wababe hawa wa soka la Tanzania na mabingwa wa kihistoria, watakutana keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo ambao ni mwendelezo wa Ligi Kuu Bara ikiwa ni raundi ya sita, umevuta hisia za mashabiki wengi kutokana na ubora wa vikosi vyote viwili kwa msimu.

Yanga ambayo imekuwa na ukata mkubwa ilionekana kuwa itakuwa dhaifu mbele ya Simba msimu huu, ambayo inaogelea kwenye neema tangu kuingia kwa mfanyabiashara na bilionea kijana, Mohamed Dewji (MO), ambaye amefanya uwekezaji wa maana.

Hata hivyo, tangu kuanza kwa ligi, Yanga imeshinda mechi zake zote huku Simba ikipoteza mmoja na kwenda sare mmoja. Imeambulia pointi moja mbele ya Ndanda FC kisha ikapoteza mbele ya Mbao FC. Mchezo huo wa Jumapili utakuwa na ushindani mkubwa huku kila upande ukitaka kushinda ili kuendeleza rekodi za kibabe dhidi ya mwenzake, lakini pia kujiweka mahali pazuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Kutokana na ushindani, ndipo Mwanaspoti tumeona ni busara na wakati mwafaka kuwakumbusha mashabiki wa timu hizo ambao, ndio wanatajwa kuwa na mivutano mingi wanapokutana kudumisha nidhamu na ustaarabu ndani ya uwanja.

Imekuwa ni jambo la kawaida kwa mashabiki wa timu hizo kuingia ama kuwa chanzo cha vurugu kabla, baada na wakati wa mechi kutokana na upinzani mkubwa walionao. Tunawakumbusha mashabiki wa Simba na Yanga kuwa, michezo ni sehemu ya furaha na burudani hivyo, waende uwanjani kushangilia timu zao wakitambua kwamba, suala la nidhamu, amani na utulivu halina mjadala na linapaswa kupewa kipaumbele.

Itakumbukwa miaka ya nyuma, mashabiki wa wababe hao wamekuwa wakihusika kwenye vurugu kwenye viwanja pindi upande mmoja unapopoteza dhidi ya mwingine.

Wote tunakumbuka matukio yasiyokubali kwenye michezo ya kurusha chupa za maji uwanjani, kushambulia waamuzi pamoja na kuchapana makonde wenyewe kwa wenyewe.

Pia, tunakumbukumbu ya uharibifu wa miundombinu ya viwanja ikiwemo kung’olewa viti kwenye viwanja kama ilivyotokea pale Uwanja wa Taifa wakati mashabiki wa Simba, wakionyesha hasira zao kwa kile walichodai uamuzi mbovu wa mwamuzi wa mchezo.

Licha ya kwamba, matukio hayo yalichukuliwa kwa uzito mkubwa na timu husika kuadhibiwa ikiwemo kutozwa faini, lakini yameacha kumbukumbu mbaya na isiyokubalika katika michezo hivyo, kila shabiki anapaswa kuhakikisha hilo halijitokezi tena kwenye soka la Tanzania. Hivyo, Mwanaspoti tunaamini kuwa mashabiki watakwenda uwanjani kuangalia burudani ya soka na sio kushiriki kwenye kufanya vurugu. Kila mmoja atakwenda Taifa akiwa mlinzi wa amani kwa kukataa kutoshiriki kwenye vitendo vya kuhuni na kuwaripoti kwa vyombo za usalama uwanjani, mashabiki ambao wataonekana kuashiria uvunjifu wa amani.

Lakini, tukiacha hilo la mashabiki, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama uwanjani hapo, vinapaswa kuimarisha ulinzi ili kudhibiti vitendo vyote vya uvunjifu wa amani. Mchezo wa watani hao wa jadi ulijulikana mapema tu kabla hata kuanza kwa ligi hivyo, tuna imani Jeshi la Polisi limejipanga vyema kutoa ulinzi kwa mashabiki.

Ni muhimu idadi ya mashabiki ikadhibitiwa ili isizidi uwezo wa idadi ya mashabiki wanaotakiwa kuingia uwanjani hapo.

Kama uwanja una uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000 basi idadi hiyo isizidi ili kukabiliana na athari yoyote inayoweza kutokea. Katika hili, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapaswa kutimiza wajibu wake kuhakikisha idadi ya tiketi zinazotolewa inakuwa sahihi.

Yale mazoea ya watu kuingia uwanjani bila tiketi ndio huleta matatizo kutokana na uwanja kujikuta kubeba idadi kubwa kinyume na uwezo wake. Endapo TFF itauza tiketi 60,000 basi kusiwepo na mtu atakayeingia uwanjani hapo kwa mipango mipango na kujuana ili kuwa na idadi kamili ya watu waliopo uwanjani hapo. Tunalisema hili kwa sababu tunafahamu kuna ujanja ujanja unaotumiwa na baadhi ya mashabiki kuingia uwanjani hasa kwenye mechi kubwa kama ilivyo ya Simba na Yanga.

Kuna idadi kubwa ya mashabiki huingia uwanjani kwa sababu tu ya kufahamiana na walinzi ama maofisa wa TFF ama timu husika wanaokaa kwenye mageti, jambo ambalo limekuwa changamoto kubwa kufahamu idadi kamili ya watu waliopo uwanjani. Ikumbukwe soka ni burudani na sio uhasama hivyo, suala la ustaarabu ni muhimu.