Hivi Simba Day ni wazo la nani?

AGOSTI 8 kila mwaka, Tanzania hushuhudia tamasha kubwa la michezo hususan soka linaloandaliwa na Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam.

Tamasha hili lilianza kama masihara mwaka 2009, katika mwaka wa mwisho wa utawala wa Mwenyekiti Hassan Dalali ‘Handsome Boy’ na Katibu Mkuu, Mwina Kaduguda ‘Simba wa Yuda’.

Viongozi waliofuata baada ya Dalali na Kaduguda, wakaendelea kulienzi tamasha hili na kuligeuza kuwa utamaduni miongoni mwa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo ya Msimbazi. Kwa kuzingatia Simba Day huangukia siku ya mapumziko ya kitaifa kwa ajili ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane), watu wengi hupata nafasi ya kuhudhuria uwanjani na kuzidi kulinogesha.

Miaka mingi baadaye, tamasha hili limekuwa kubwa kiasi cha kuwavutia watu wengi na kuujaza Uwanja wa Taifa, wenye viti 60,000 kama ilivyohuhudiwa

mwaka 2017. Hili si tamasha dogo hata kidogo. Lakini je, nani aliyetoa wazo la kuanzishwa tamasha hili?

HASSAN DALALI?

Mwenyekiti wa Simba wakati tamasha hili likianzishwa, Hassan Dalali, anasema yeye ndiye aliyetoa wazo la kuanzishwa kwa tamasha hili kwenye Kamati ya Utendaji. Anasema wazo hilo lilimjia wakati akitafakari namna ya kupata pesa za kulipia hati ya kiwanja ambacho walitoka kupewa na serikali maeneo ya Bunju.

“Simba ilikuwa haina uwanja, mimi nikatafuta uwanja…nikaenda wizarani. uwanja ule thamani yake ilikuwa Shilingi 106 milioni. Klabu haina pesa…ndo nikabuni hili jambo. Kwa mwaka wa kwanza tuliweza kupata milioni 70. Tukachukua milioni 20 tukapeleka wizarani kuzuia ule uwanja’.

KASSIM DEWJI

Katibu Mkuu wa zamani wa Simba, Kassim Dewji, ambaye wakati tamasha hilo likianzishwa alikuwa mmoja wa watu wa Kundi la Friends of Simba, anadaiwa kuwa yeye ndiye aliyetoa wazo hilo kwa uongozi wa Hassan Dalali.

Kwa mujibu wa chanzo kikubwa ndani ya uongozi wa sasa wa Simba ambacho na chenyewe ni kati ya wale Friends of Simba, KD ndiye alikuja na wazo hilo na

kumpelekea yeye kabla ya kulifikisha kwa uongozi wa Dalali.

“Unajua hawa wazee hawataki tu kusema ukweli. Wakati wa utawala wa Dalali na Kaduguda, sisi ndio tuliokuwa tunaongoza klabu nyuma ya pazia. Dalali alikaa pale kama shati tu. Kassim akaja na wazo hilo, mimi nikaliona linafaa na ndipo likapelekwa kwenye kamati ya utendaji ili liwe rasmi.

“Lakini kwa kuwa wakati ule Simba ilikuwa chini ya Dalali kama mwenyekiti, unaweza ukampa sifa katika kulifanikisha lakini sio kutoa wazo…yeye wenyewe anaujua ukweli huu.”

WENZETU HUWEKA WAZI

FC Barcelona ni klabu iliyofanikiwa sana na sera ya kuibua vipaji kutoka kwenye akademi yao maarufu ya La Masia.

Mwaka 2002 La Masia ilitangazwa kama akademi bora zaidi duniani na mwaka 2010 ikaandika historia kuwa akademi ya kwanza (na pekee hadi sasa) kutoa wachezaji watatu waliofika fainali ya kuwania uchezaji bora wa dunia (Ballon D’Or), Andrés Iniesta, Lionel Messi na Xavi.

Akademi hii ilianzishwa mwaka 1979 na Rais wa klabu hiyo Josep Lluís Nunez.

Lakini wazo halikuwa la kwake, lilikuwa la mchezaji nyota wa klabu hiyo, Johan Cruyff.

Cruyff ambaye mwaka 2015 alikuja Tanzania kama kocha wa wachezaji wa zamani wa FC Barcelona waliocheza na wachezaji wa zamani wa Tanzania, alimfuata Rais Nunez na kumpa wazo hilo.

Rais Nunez alichokifanya ni kumteau Oriol Tort kusimamia mradi huo na kuweka wazi wazo hilo halikuwa la kwake bali la Cruff. Leo hii dunia inajua Johan Cruyff ndiye aliyetoa wazo la kuanzishwa kwa La Masia.

HITIMISHO

Ukweli wa hili ni lazima upatikane ili kila anayestahili sifa, apewe na historia imkumbuke kwa hilo. Hata Mwalimu Nyerere ambaye aliongoza mapambano ya uhuru wa nchi hii, hakuwahi kujitapa yeye ndiye aliyetunga jina zuri la nchi yetu la Tanzania. Historia inamtambua MOHAMED IQBAL DAR kuwa ndiye mtu aliyebuni jina hilo.

Kwenye Simba Day ya mwaka huu, Kassim Dewji na Hassan Dalali wajitokeze kwa pamoja waweke ukweli wazi ili rekodi zikae sawa na historia imtendee haki anayestahili kupewa heshima ya kubuni Simba Day.