Tangulia Ruge, ndo umeimaliza safari

KATIKATI ya mwaka 1997 nikiwa Mwandishi wa Habari za Michezo na Burudani wa gazeti la Majira, Joseph Kusaga ananipigia simu na kunikaribisha ofisini kwake. Ofisi za Clouds zilizokuwa jengo la Kitega Uchumi lililopo Mtaa wa Samora.

Aliniambia kuna jambo anataka tuzungumze. Katika jengo lile, kulikuwa na ofisi mbili, moja ilikuwa ghorofa ya saba na nyingine ghorofa ya 10 ndiko kulikoanzia studio za Clouds. Kusaga nilimfahamu kwa kuwa amekuwa akiandaa matamasha ya kualika wanamuziki mbalimbali nakumbuka marehemu Brenda Fassie wa Afrika Kusini, pia alishamwalika Yvonne Chakachaka.

Pia Clouds wakati huo kabla ya redio, ndio waliolialika kundi la Wenge Musica BCBG kutoka DR Congo, enzi zile Wenge ikiwa moto chini ya JB Mpiana na Werrason Ngiama Makanda sambamba na kina Blaise Bula na wengine waliokuwa maarufu. Ilikuwa ile BCBG yenyewe.

Baada ya kupokea simu ya Kusaga, nilichukua daladala nikitokea ofisini Mtaa wa Lugoda hadi Posta na kufika Jengo la Kitega Uchumi. Ninapanda lifti hadi ghorofa ya saba zilizokuwa ofisi za Clouds.

Ninafungua mlango nakutana na Monica, msichana mrembo pale mapokezi. Alikuwa mweupe kiasi. Ananikaribisha na kumwambia nilikuwa mgeni wa Kusaga. Wakati ninaendelea kujitambulisha pale mapokezi, mara Kusaga mwenyewe naye anatokea kutoka ofisi yake akiwa amefuatana na mmoja wa Madij maarufu enzi hizo, Boniface Kilosa, ‘Bonny Love’. Wakati huo alikuwa akipiga disko, Bahari Beach.

Kusaga ni kama aliyekuwa anataka kwenda ofisi nyingine, ila aliponiona akaghairi. “Aah Ibra umefika…karibu sana”. Alinipokea kwa bashasha. Akanikaribisha ofisini kwake. Nilipoingia nikakutana na mtu mmoja alikuwa akisoma gazeti. Nikamsalimia. Baada ya salamu Kusaga alinikaribisha kwenye sofa.

Akanitambulisha kuwa huyu anaitwa Ruge Mutahaba na wote tukatambuana. Palepale tukaanza stori mchanganyiko. Sikuwa nikimfahamu sana Ruge, lakini kuanzia siku ile, ndipo tukaanza kufahamiana.

Tulizungumza mengi hasa fani ya uandishi enzi hizo nikiwa mchanga. Nilikuwa nina miaka miwili tu kwenye fani, lakini kubwa zaidi Kusaga pamoja na Ruge katika mazungumzo walikuwa wakizungumzia azma yao ya kufungua kituo cha redio. Joseph alisema pamoja na studio ya Arusha ya Mawingu, lakini wanataka kufungua nyingine Dar es Salaam. Tulizungumza mengi ya mpango huo. Na niliwapa uzoefu kwa kuwa wakati huo nikifanya kazi gazeti la Majira, nilikuwa nikitangaza, Redio Tumaini, nilikuwa ninaendesha kipindi cha habari za wiki kimataifa.

Kipindi nilichokiendesha pamoja na Mpendwa Mgweno ambaye kwa sasa yuko Shirika la Utangazaji Tanzania, TBC. Tukazungumza mengi na kuweka mikakati ya jinsi studio itakavyofanya kazi. Nikapelekwa hadi eneo lililopangwa kuwepo studio zenyewe. Ilikuwa juu kabisa ghorofa ya mwisho jengo hilo la Kitega Uchumi.

Wakati nikitembelea studio zilipokuwa katika michoro maana hata matangazo hayakuwepo, palepale nikapata akili ya kuandika makala. Mawingu Studio ya Arusha ilikuwa maarufu enzi hizo na umaarufu wake ulikua zaidi baada ya kuandaa shindano la urembo kimkoa na kumtoa mrembo wake, Said Kessy ambaye baadaye alikuja kuwa Miss Tanzania 1997 akitokea Arusha.

Nilitengeneza makala ya Studio Mawingu yenye maskani yake mkoani Arusha kufungua studio nyingine Dar es Salaam. Hiyo ilikuwa mwaka 1997.

Wakati natembelea patakapozaliwa Radio Clouds, huwezi kuamini, chumba kilikuwa kidogo, na hakikuwa na nafasi ya watangazaji wawili. Studio ilikuwa ya mtu mmoja na kulikuwa na chumba kingine kalikojaa santuri. Ilikuwa ni maandalizi ya kufungua studio mpya za Clouds. Pamoja na hayo santuri nyingine zilikuwa kwenye sanduku kubwa lililokuwa ofisini kwa Kusaga na Ruge. Hiyo ilikuwa kazi ya Bonnie Love wakati akikusanya kazi kwa ajili ya studio. Kilichokuwa kikifanyika, mpango wa awali ni kutumia zile kaseti na santuri zilizokuwa zikitumika kwenye disko kuwa ndizo zitumike kuanza nazo studio na nyingine zilichukuliwa studio ya Arusha.

Mambo mbalimbali yalikuwa yakikwamisha kuanza kwa studio ikiwemo kupatikana kwa vifaa vya kisasa. Lakini hata hivyo, kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na Ruge. Ninakumbuka Kusaga aliniambia, Ruge alikuwa akienda Marekani mara kwa mara kwa ajili ya kununua vifaa pamoja na mtu mwingine, Othman Njaidi. Haikuchukua muda mrefu. Miaka miwili baadaye, Clouds ikapata masafa na kuanza matangazo. Hiyo ilikuwa mwaka 1999. Mpango wa Ruge na Kusaga ukatimia. Hawakuanza mpango na kuishia kati, ulisimama na hadi leo hii Clouds ni habari nyingine.

Baada ya kupata masafa, kilichokuwa kikifanyika ni kupiga muziki mwanzo mwisho. Wakati redio inaanza sasa, hakukuwa na vipindi, ilikuwa ni muziki saa 24. Nakumbuka Bonni Love mwenyewe na kuna wakati alikuwa DJ Rankim Ramadhan. Tukiwa pale ofisini kabla ya redio, Ruge aliniambia anataka kufanya redio itakayokuwa maarufu kupita Redio Tanzania na Redio nyingine. Aliniambia anataka iwe maarufu zaidi na kuteka hata redio nyingine. Kweli mawazo yale yalitimia. Clouds ilipoanza, ilisikika kila kona na mpaka leo. Tulifahamiana baada ya kupeana hadidu mbili tatu za utangazaji. Baada ya pale ndipo tukawa marafiki. Kila tukio la Clouds nilikuwa mmoja wa watu muhimu kwao. Hata ujio wa Wenge BCBG nilikuwa mmoja wa wanakamati upande wa vyombo vya habari.

Nilikuwa na waandishi kadhaa akiwemo Fred Ogot (Guardian) na Cosmas Mlekani wa Nipashe. Tulishirikiana na Ruge pamoja na Kusaga kwa njia moja ama nyingine na zaidi ni kwa kuripoti ujio ule. Nilimfahamu vizuri Ruge tulipokuwa safarini kwenda Arusha mwaka 1997 kwenye shindano la Miss Arusha ambalo Saida Kessy alishinda. Shindano lilifanyika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya 77. Ruge tulizungumza mengi na alikuwa mtu mwenye akili za mbali. Alikuwa akipanga mambo mengine unaona kama hayawezekani, lakini aliyasimamia yakawezekana.

Ukisikia kuna vita, halafu kuna wale mabrigedia wanaopiga hesabu wamchape vipi adui, basi Ruge alikuwa mchora ramani mzuri. Kama Brigedia wa kuchora ramani, basi Ruge alikuwa namba moja. Alikuwa mtu mmoja mbunifu tangu zamani. Ukiorodhesha alichofanya, hata nafasi hapa haitoshi.

Ninakumbuka wakati ule alikuwa halali. Hata kukiwa na tukio linalofika saa nane usiku haondoki kuhakikisha kila kitu kimekaa sawa. Ruge alikuwa wa mwisho kutoka ukumbini. Huyo ndiye Ruge Mutahaba ambaye leo hii hayupo. Ametangulia mbele za haki. Maisha yake aliyapeleka zaidi kwa watu. Alikuwa mwenye kutaka mafanikio, lakini alikuwa akiona fahari zaidi kuona mtu amefanikiwa kupitia maelekezo yake. Hakuwa mwenye makeke sana. Kama kulikuwa na hitilafu, alikuwa akipambana kuona itilafu hiyo inamalizika. Hakuwa mkaidi wa kumwambia mtu, basi tusameheane. Nilipomfahamu na hata tulipokuwa tukiwasiliana, hakuwa mtu wa kukata simu, kuisikilizia simu na hakuona tabu kupokea. Mara zote alikuwa mtu wa kusikiliza na kama ni tatizo alilipatia suluhu. Hilo ndilo somo kubwa alilotuachia Ruge. Tangulia Ruge.

Hadi umauti unamfika, alikuwa Mkurugenzi na Mzalishaji wa Redio na Televisheni ya Clouds` s Media. Ruge alifariki Dunia juzi Jumanne usiku akiwa anapigania uhai wake nchini Afrika Kusini akisumbuliwa na tatizo la figo

Ruge alizaliwa 1970, huko Brooklyn New York, Marekani. Alipata elimu yake ya Msingi Shule ya Arusha Darasa la kwanza hadi la sita, akahama shule hiyo na kujiunga na Shule Msingi ya Mlimanii.

Alisoma Sekondari ya Forodhani kidato cha kwanza hadi cha nne na baadaye kidato cha tano na sita Sekondari ya Pugu. Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha San Jose Marekani alikopata shahada yake ya masoko pamoja na masuala ya usimamizi wa fedha.

Ruge alianza kusumbuliwa na maradhi ya figo katikati ya mwaka jana na alianza kupata matibabu yake katika Hospitali ya Kairuki Jijini Dar es Salaam na akatakiwa kwenda India kwa ajili ya matibabu. Ruge alitibiwa lakini baadaye akaamuliwa apelekwe Afrika Kusini alikoendelea na matibabu yake hadi umauti ulipomfika.