Mwasiti: Tatizo ni misimamo ya kijinga

Monday January 13 2014

Mwanamuziki wa zouk nchini, Mwasiti Almas

Mwanamuziki wa zouk nchini, Mwasiti Almas ambaye leo anatarajia kutambulisha kibao chake kipya cha Serebuka, Picha na Mwandishi Wetu 

SEREBUKA ndiyo wimbo utakaotambulishwa rasmi leo Jumatatu na mwanamuziki wa zouk nchini, Mwasiti Almas, ikiwa ni singo yake ya nane tangu aanze muziki miaka minane iliyopita.

Serebuka imekuja ikiwa ni baada ya binti huyo aliyevuma kipindi cha nyuma na singo yake Nalivua Pendo kukaa kimya kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu.

Ndiye msanii wa kwanza wa kike nchini Tanzania ambaye tangu aanze muziki hajawahi kutoa singo kisha isifanye vizuri. Mwasiti alianza kwa wimbo wake wa Niambie na kufanikiwa kufanya nyingine kama Mapito, Nalivua Pendo, Hao, Siyo Kisa Pombe na nyinginezo.

Mashabiki wa muziki nchini walimsikia Juni 2012 alipotoa wimbo wake wa mwisho ‘Mapito’ aliomshirikisha Ali Nipishe na tangu hapo Mwasiti amekuwa kimya huku akionekana kwenye kampeni mbalimbali za elimu na afya zilizokuwa zikiendeshwa mwaka 2013.

Mwanaspoti lilikaa kitako na Mwasiti na kujadiliana naye mambo mbalimbali;

Mwanaspoti: Ukimya wako ulisababishwa na nini?

Mwasiti: Mara nyingi huwa napenda kuwaacha watu wengine nao wasikike lakini nilikuwa na mambo mengi ya kufanya na kuna kipindi kirefu tu, sikuingia studio kutokana na kampeni mbalimbali nilizokuwa nikizifanya kwa ajili ya jamii yetu. Nilikuwa na kampeni tofauti ikiwemo ile ya Tokomeza Ziro na ile ya Malaria, kwa hiyo nilikuwa bize na mambo hayo na kazi nyingine ambazo zilichukua muda mwingi nikaona ngoja muziki usubiri nikamilishe mambo ya msingi kwa taifa.

Mwanaspoti: Hebu tuambie kuhusu kampeni hizo na umefanikiwa kwa kiasi gani kufikisha ujumbe?

Mwasiti: Siku zote nimetanguliza utaifa mbele kitendo cha wadogo zangu kidato cha nne kupata ziro kilinisikitisha sana. Hivyo nikaona ni wakati wangu kuhakikisha natoa elimu vile ipasavyo na sehemu tulizotembelea tumefanikiwa kuwabadili watu kwa kiasi kikubwa kupitia sanaa.

Baada ya kukamilisha mchakato huo nikaona ni wakati mwafaka kuwapa Watanzania kile wanachokisubiri kutoka kwangu Januari 13 nitatoa kazi mpya kwa ajili yao.

Mwanaspoti: Kazi ipi hiyo tena!

Mwasiti: Wimbo wangu wa nane utaitwa Serebuka. Wimbo huu utakuwa maalumu kwa ajili ya watu walio katika uhusiano. Serebuka ni wimbo unaozungumzia matukio mengi ya mapenzi, sijazungumzia mtu mmoja nimezungumzia watu wengi ambao wamekutana na matukio mengi ya mapenzi.

Unashangaa watu wanafumaniana lakini bado wanapendana serebuka si raha peke yake wapo waliokaa katika uhusiano kwa muda mrefu kwa kudhani labda wataolewa lakini mwishowe mtu anakuja kuoa mtu mwingine lakini tunapaswa kutambua kwamba kila kitu kina muda wake na hakuna mtu asiye na mume au mke wake mwenyewe.

Mwanaspoti: Kwa mara ya kwanza wikiendi iliyopita uliweka picha na kutangaza ujio wako unahisi ni kwa nini watu wengi walijitokeza kukuunga mkono?

Mwasiti: Binafsi nilistaajabu niliweka ile picha kwenye mtandao wa ‘Instagram’ lakini mapokeo yake yalikuwa makubwa sana nilistaajabu watu wengi kuchukua ile picha na kuweka katika mitandao mbalimbali huku wengi wakiwa na shauku ya kuusikia.

Nimejifunza kitu kwamba napaswa kuiheshimu sana kazi yangu ya muziki kwani mashabiki wanaheshimu sana kazi yangu.

Mwanaspoti: Ni nini mipango yako kwa mwaka huu?

Mwasiti: Mwaka huu nimepanga kutoa nyimbo tatu ninafanya hivi makusudi na si kwamba nina kazi nyingi, pia kwa sasa nimeshamaliza albamu yangu na nina mikakati mingine mingi.

Mwanaspoti: Unadhani unaweza kuuza albamu?

Mwasiti: Inawezekana katika hilo, kwangu mimi naamini hivyo japokuwa wasanii wengi wana hofu na hilo.

Mwanaspoti: Nini kilisababisha 2013 usionekana katika shoo za jukwaani?

Mwasiti: Ni kweli hakuna shoo ya jukwaani ya kizazi chetu ambayo niliifanya kwa mwaka jana. Kwanza kabisa nilikuwa sina kazi mpya. Pia nilikuwa bize na kazi za kampeni. Nilifanya shoo lakini zilikuwa tofauti na shoo za kila siku nilizozoea kuzifanya kama shoo za kwenye mikutano mikubwa ambazo si za umri wetu.

Mwanaspoti: Kwa kipindi ulichokaa kimya bila kutoa singo unaonaje mchakato wa muziki wa kizazi kipya mambo yanakwenda sawa au ndivyo sivyo?

Mwasiti: Muziki umekua asikwambie mtu, namshukuru kwanza mwanamuziki Diamond anazidi kutufanya hata sisi kuanza kutambulika nje, sasa msanii ukisema natoka Tanzania watu wanaijua Bongo Fleva tofauti na awali. Lakini wapo wanaoingia na wapo pia wanaochuja na kutoka, huu ndiyo muziki.

Mwanaspoti: Unachukuliaje tabia ya baadhi ya wasanii kuanza kuwaponda watu wanaowazunguka katika fani au wasanii wenzao?

Mwasiti: Mara nyingi utakuta msanii fulani amefanya kitu kikubwa na hapo ndipo chuki inapoanzia, watu wanakuwa na wivu wa maendeleo wanashindwa kuiga mazuri wanaishia kuponda.

Mfano mzuri ni Diamond. Huyu anapigwa mawe sana wakati huu lakini hii yote inatokana na juhudi zake, anajituma na hategemei mtu amwambie fanya hivi anawaza usiku na mchana kuhakikisha kwamba anafanya kitu cha tofauti, lakini ukirudi nyuma unakuta kizazi chake hakijafanya hivyo.

Mwanaspoti: Kwa nini wasanii wa kike Tanzania huibuka na umaarufu wao hupotea baada ya muda mfupi?

Mwasiti: Wengi wao huwa hawaoni fursa, yaani wanapewa lakini wanazichezea na hii yote inatokana na misimamo ya kijinga. Unamkuta mtu hana mpango wa kufikiri nifanye hivi ili nipite hapa nitengeneze kazi nzuri ili niendelee kukaa kileleni, hawazioni kabisa fursa zinazowazunguka.

Mwanaspoti: Kuna ukweli kwamba wasanii wa kike wakibebwa hubweteka?

Mwasiti: Ni kweli wasanii wa kike wakipata nafasi wanasahau walikotoka na mwisho wa siku anakusubiri wewe utoe wimbo na ndipo na yeye atoe msikike wote redioni. Wanamuziki wa kiume wakipata nafasi hawazichezei lakini sisi tupo wachache tunapewa nafasi ambazo tunazichezea.