Mnalia Ruge kufa! Tusherehekeeni

ILIKUWA Aprili 2012. Kipindi ambacho Taifa la Tanzania lilikuwa limeondokewa na tunda jema la sanaa za maigizo, Steven Kanumba. Kwenye line ya simu nilikuwa nazungumza na Ruge Mutahaba.

Hapa niseme jambo kuhusu Ruge. Alikuwa akiamua kujitoa kwenye jambo, basi alijitoa kweli. Ruge alikuwa kwenye kamati ya kuratibu mazishi ya Kanumba aliyefariki dunia Aprili 7, 2012. Ruge aliubeba msiba wa Kanumba kama wa ndugu yake toka nitoke.

Sikuwa kwenye kamati ya mazishi, ila Ruge alitaka taarifa za kwenye vyombo vya habari kutoka kwenye kamati hiyo niandike mimi na nilisaini kwa niaba ya mwenyekiti. Ruge aliniamini katika kuandika, akanipa dhima hiyo. Nami niliona heshima.

Ruge alipokuwa akinielekeza ya namna ya kuandika taarifa jinsi mwili wa Kanumba ungetolewa Hospitali ya Taifa, Muhimbili, kupita barabarani hadi Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, aliniambia: “Tuwaoneshe watu kuwa huu siyo wakati wa kumlilia Kanumba bali kusherehekea maisha yake.” Nikashtuka!

Akaendelea: “Maisha ya Kanumba ndiyo yamefanya tumjue. Sasa tuwafanye watu washerehekee maisha yake. Watu wasimame kandakando ya barabara kumpungia mikono akipelekwa Leaders kuagwa.” Nikahamasika, hakika tulisherehekea maisha ya Kanumba. Takriban miaka miaka saba tangu Kanumba alipoondoka, Ruge naye ametutoka. Nilipata wakati mgumu sana nilipopokea taarifa za kifo cha Ruge aliyefariki juzi (Februari 26). Nilibaki nimezubaa tu. Machozi hayakutoka. Nikapokea maagizo ya kiofisi kuwa natakiwa kuandika makala kuhusu Ruge kwa ajili ya gazeti la Mwanaspoti.

Baada ya muda mrefu wa kuumia, nikakumbuka agizo la Ruge kuwa tusimlilie Kanumba bali tusherehekee maisha yake. Nikajiuliza, naumia nini sasa? Ruge alikuwa bonge la zawadi kwa Watanzania. Kwa nini nilie badala ya kusherehekea utamu wa maisha yake?

Ruge nguzo ya Clouds Media Group (CMG). Mwasisi wa redio za burudani Tanzania. Mchonga barabara ya sanaa Tanzania. Muibua vipaji vya sanaa na kuvikuza kupitia taasisi yake yake ya THT. Huyu tunamlilia au tunasherehekea utamu wa maisha yake?

Mtu aliyeitoa Clouds FM kuwa redio ya kwenye kachumba kamoja hadi kumiliki redio kadhaa, vituo viwili vya televisheni, majenga na ajira ya mamia ya Watanzania. Sasa ameondoka, ameiacha CMG ni maisha ya wengi. Huyo tunamlilia kivipi?

Ruge na mwenzake Joseph Kusaga, wakaweka falsafa ya vijana kwanza kwenye redio yao. Ikashuhudiwa vijana wenye vipaji wakipata jukwaa la kuonesha walichonacho. Vijana ambao pengine sehemu nyingine wasingepata nafasi, lakini kupitia Clouds FM wamekuwa mastaa wakubwa. Huyu Ruge ndiye ambaye aliona matamasha ya Fiesta yasiwe yanaishia tu kwenye muktadha wa burudani. Alitaka Watanzania waburudike lakini pia wapate mwanga na maarifa kuhusu kujikwamua na maisha yao. Akaanzisha mradi wa Fursa.

Kupitia Fursa, Ruge alikutana na jamii mbalimbali. Wengine walikuwa hawaoni mwanga wa kufanikiwa. Tayari kuna watu hutoa ushuhuda kuhusu jinsi makongamano ya Fursa yalivyowatoa kimaisha na leo wanaendesha biashara zao wakiwa na biashara zao.

Majukwaa ya Fursa yalimfanya Ruge akutane na akina mama na kuwajengea matumaini. Akapita vyuoni na kuwajaza fikra tofauti kuhusu changamoto za kimaisha na utatuzi wake. Vijana wengine wanatamba ni zao la Ruge. Je, huyo ni wa kumlilia? Tusherehekee maisha yake.

RUGE WA VIPAJI

Siku moja, mwaka juzi, nilikuwa ofisini kwa Ruge. Aliniita kwa ujenzi wa wazo fulani la mapambano ya kimaisha. Akaingia mmoja wa wasaidizi wake akiwa ameshikilia CV za mtu mmoja aliyeomba kazi. Ruge akauliza: “Nani huyo ameruhusu CV zije kwangu?”

Ruge akaendelea: “Utaratibu wetu wa kuajiri hapa unafahamika, lazima mtu aje kwanza tumuone anavyofanya kazi, tukiona anafaa ndiyo tumchukue. Mtu anaweza kuwa na CV nzuri lakini kazi hawezi.” Ruge alizungumza hivyo akiwa amehamaki. Anajua falsafa za uajiri ofisini kwake.

Falsafa inayozingatia vipaji na uwezo kwanza kisha vyeti vinafuata. Ni falsafa hiyo imefanya Clouds ionekane kampuni ya masela wenye vipaji. Masela ambao wamekuwa na athari kwa vijana wengi kutamani kuwa watangazaji. Masela wa Clouds wamewaambukiza vijana wengi mtindo wa kutangaza, uvaaji na mwonekano.

Ukizungumza na Gardner Habash, atakwambia kuwa yeye alikuwa hajui kama anaweza kutangaza. Alikwenda Clouds FM wakati redio hiyo ikiwa changa kabisa na kazi aliyoomba ni kuwa Ofisa Masoko. Ruge alipomsikiliza Gardner, akamwambia aachane na masoko awe mtangazaji. Gardner akashangaa lakini hivyo ndivyo ikawa. Leo Gardner ni mtangazaji kinara. Gardner ni zawadi ya Watanzania katika utangazaji. Ruge ndiye alimfanya Gardner awe alivyo.

Rapa Nikki wa Pili atakwambia alipokutana na Ruge alimwambia ana uwezo mkubwa wa kuzungumza kwenye majukwaa ya umma. Ruge akampa nafasi Nikki kwenye majukwaa ya Fursa. Leo hii Nikki anakiri kuwa hupokea mialiko mingi na analipwa vizuri kwenda kutoa hotuba za kijamii na uhamasishaji.

Hili eneo la kuwapa watu maisha kwa kuwaambia wanaweza tofauti na kile walichokuwa wanafanya, idadi ni kubwa. Niishie tu kusema kwamba Ruge alikuwa na jicho la kuona zawadi asili ndani ya mtu kuliko ambavyo mtu husika alijitambua. Barnaba ni mwanamuziki mkali mno na alama ya THT. Nani anajua kuwa Barnaba alikataliwa THT? Majaji walimuona hafai. Ruge akitazama dirishani, akiwa siyo mmoja wa majaji, aliona janki ana vitu zaidi. Akaomba majaji wamsikilize tena. Leo nani ana shaka kuhusu uwezo na kipaji cha Barnaba.

LAWAMA ZOTE KWA RUGE

Ruge ni alama ya ukuaji wa sanaa Tanzania. Amekuwa sehemu ya mafanikio ya wengi. Hata hivyo, ni Ruge huyohuyo ambaye amekuwa akibeba lawama kuwa yeye ni sababu ya anguko la wasanii wengi.

Zipo lawama nyingine alizibeba na kuzikubali kwa masilahi ya kampuni yake. Alikuwa mstari wa mbele kutoka na kuwaelewesha watu pale alipoona Clouds inasingiziwa au yeye binafsi anazushiwa. Mfano, mimi nilikuwa mwandishi wa kwanza kabisa kuandika kuhusu mradi wa Antivirus. Wana Hip Hop walioungana na kujiita Vinega walitoa Mixtape yenye maudhui ya kumshambulia Ruge na Clouds yote. Siku moja Ruge alinipigia simu kujaribu kunielewesha kuwa yeye na Clouds wanaonewa. Hili nililichukua kwa heshima, kwamba ingekuwa wengine wangejenga chuki, lakini Ruge hakuwa mjenga chuki, kwani chuki ni ukuta, naye alipenda kujenga daraja.

Ruge vile alizaliwa Marekani na chuo kikuu kusomea Marekani, alikuwa na roho ya kimarekani kweli. Mnaweza kugombana leo kwa masilahi na kesho mtapatana yakiibuka masilahi mengine. Ruge hakuwa na kinyongo cha kuendelea.

Kuna kipindi Clouds walikuwa na mgogoro wa Profesa Jay. Ukiangalia sababu ilikuwa Jay kushonana na Lady Jay, ambaye alikuwa kwenye vita na uongozi wa Clouds FM hasa Ruge na Joe Kusaga. Jay alipotaka kutoa wimbo “Kipi Sijasikia” mwaka 2014, ilibidi apate ushauri wa kumaliza tofauti zake za Clouds.

Ruge alikuwa mtu wa kwanza kumkubalia Jay kumaliza tofauti zake. Ni kipindi ambacho kundi la Hip Hop la Mapacha (Maujanja Suppliers) ambalo lilikuwa kinara wa Vinega, nao walipata suluhu na Clouds. Hulaumiwa sana, lakini ni kuonesha namna ambavyo alijenga ushawishi kwenye muziki. Clouds imekuwa jukwaa la kuitangaza na kuikuza Bongo Fleva. Matamasha ambayo kampuni tanzu ya Clouds, Prime Time Promotion imekuwa ikiyaandaa, ni jukwaa la wasanii kujitangaza na kupata kipato. Na wanasema palipo na riziki hapakosi husuda.

Hata mgogoro wa Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda na Ruge chanzo ni Ruge kuitetea kampuni yake. Ruge alikubali agombane na Makonda ili kuwalinda vijana wa Shilawadu. Makonda alidaiwa kuwavamia Shilawadu studio na kulazimisha maudhui fulani yarushwe Shilawadu.

Makonda alipotaka kuwakabili Shilawadu, Ruge alimwambia yeye ndiye alizuia maudhui aliyotaka yasiende hewani. Mwanzoni ukawa mgogoro wa Makonda na Clouds, lakini baadaye ukabadilika ukawa Makonda na Ruge. Kiukweli Ruge alibeba mizigo mingi.

Ruge alikuwa mlezi wa wanamuziki. Chidi Benz alipoivaa kesi ya kukutwa na dawa za kulevya Airport, Dar es Salaam, Ruge aliingia kati na kumsaidia Chidi kulipa faini. Ray C alipotopea kwenye utumiaji wa dawa za kulevya, Ruge alikuwa kama baba yake mzazi.

Gazeti likiandika na kutoa habari hasi kuhusu Ray C, Ruge alipiga simu kuomba ‘mwanaye’ apewe msamaha, kwani habari mbaya zingempoteza. Rais wa Nne, Jakaya Kikwete alipotokeza kumsaidia Ray, ni Ruge aliyesimamia matibabu yake mpaka akapona. Daima Ray C humwita Ruge baba. Wanasema Ruge alifanya makosa mengi katika sanaa. Nani asiye na makosa. Ukimsema Ruge alibomoa, basi alijenga sana. Lawama za Ruge zipo kila upande, hata walioshirikiana nyakati njema, baadaye walianza kumwita majina mabaya.

Ni Ruge aliyefanya onesho lililompa Diamond Platnumz thamani kubwa la Diamonds Are Forever, Mlimani City mwaka 2012. Ruge alimjengea Diamond menejimenti yake ya sasa ya akina Babu Tale na Said Fella. Hata hivyo, Diamond na Tale walianza mashambulizi kumsema vibaya Ruge. Ni yeye aliyemsaidia Diamond kusaini mkataba usiku na Davido wa kurekodi wimbo Number One Remix. Mkataba ulisainiwa THT. Rasimu ya mkataba iliandikwa na msaidizi wa Ruge bila malipo ili kumsaidia Diamond atoboe kimataifa. Na wimbo huo na Davido ukamfungulia Diamond milango mingi na alimfanya alivyo leo. Ni kama alivyomjenga Jaydee na wengine. Papii Kocha alipokuwa jela alishawishika kuamini Ruge alimuibia. Akaandika barua kumnyang’anya usimamizi wa kazi zake.

Ruge asivyo na kinyongo, Papii alipotoka jela na baba yake, Nguza Viking ‘Babu Seya’, alimpokea na kusimamia kazi ya wimbo wake “Waambie”. Ifike kipindi tukubali kuwa Ruge alikuwa na karama ya peke yake. Wengi hawawezi kuwa Ruge.