NO AGENDA: HAPA NDIO SHILOLE ALIPOCHAKAZWA

KAZI ipo na waliotaka kazi wanapewa dubleduble. Wanahenyeshwa, wanatamani kuomba poo! Dar es Salaam ina mambo alisema Sugu kwenye wimbo Dar es Salaam. Na baba yangu aliniambia nikichelewa kufa nitaona mengi.

Nayaona mimi Luqman! Biashara ya chakula nilizoea kuona ikitangazwa kwa yale mapishi yake, ladha yake au hata mwonekano wa chakula chenyewe. Siku hizi ni tofauti. Maakuli yanatangazwa kupitia kiwiliwili cha mpishi. “Karibuni biriani tamu,” mpishi anatangaza mitandaoni huku akijizungusha kuonesha neema za uumbwaji wake.

Mpishi anatangaza: “Mariam biriani ndiyo habari ya mjini. Karibuni sana Ijumaa hii.” Baada ya maneno hayo anajizungusha, anajitembeza kwenye kamera. Kideoni mitandaoni anaonesha kile ambacho Sheikh Hilal Kipozeo huita “neema za Allah.” Basi watu hoi! Hawaambiwi kitu kuhusu Mariam Biriani.

Unaambiwa hata wasiopenda biriani wamefunga safari kutoka Kiburugwa mpaka Kinyerezi kufuata biriani la Mariam. Bwa Shee alinishangaza kutoka Kishimundu mpaka Tabata kufuata biriani la Mariam. Nikamuuliza kilichomvutia ni mapishi au mpishi? Jibu alikuwa nalo basi? Akasema alijikuta tu yupo Tabata Kinyerezi kwa Mariam. Hakumbuki hata alipandaje gari!

Mshikaji wangu akaniuliza: “Hivi Wachaga na biriani wapi na wapi?” Nikamwambia ashike adabu, hao ni wakwe zangu! Hata hivyo, mimi nilijua kilichomtoa Bwa Shee Kishimundu siyo biriani la Mariam, bali Mariam Biriani. Sijui umenielewa? Namaanisha Bwa Shee alivutwa Kinyerezi na mpishi wala siyo mapishi.

Dar ina hatari Sheikh! Na wanaume wa Dar wamenishinda tabia. Dada yangu Zuwena ambaye mnamwita Shilole, si ndiye alikuwa habari ya mjini kwa mahanjumati. Tukaambiwa “Shishi Food” ndiyo habari ya mjini. Siku hizi simsikii. Masikio ya wanaume Dar yameelekezwa Kinyerezi.

Kimsingi wanaume wa Dar antena zao kwa sasa zimeshategeshewa Kinyerezi. Mawimbi ambayo hunasa kichwani kwa wanaume wa Dar ni Kinyerezi, biriani na Mariam. Hupita Kinondoni kwa Shishi kama hawamjui.

Shishi na umalkia wake wa nguvu aliotunukiwa juzikati na Clouds Media ni wa kuchakazwa vibaya namna hii na Mariam Biriani? Sijapenda!

SIJUI TUMEFIKAJE?

Jana niliona video nyingine ya mdada anayejiita Kidoti Misosi. Anasema biashara yake anafanyia Sinza. Anatangaza huduma unazoweza kuzipata kwake, naye anajizungusha, halafu anasema: “Si unaona mtoto nilivyotulia?” Anaonesha neema za Allah alizosema Sheikh Kipozeo.

Kidoti Misosi anakwenda mbele zaidi na kutangaza kuwa ana watoto wanne lakini yupo bomba. Sasa sijui ukila misosi yake ndiyo unakuwa na mwonekano kama yeye?

Kama ndivyo, basi wateja wake wengi wangepaswa kuwa wanawake ili wapate umbile kama lake. Shangaa; wateja wengi watamiminika wanaume.

Tumefikaje hapa wajameni? Chakula kinatangazwa kwa mwonekano wa mpishi? Hii ndiyo Tanzania ya intaneti. Mariam Biriani hajalipa tangazo lolote ili atrend mitandaoni. Watu wanachukua video, wanasambaziana WhatsApp, wanaposti Facebook na Instagram. Kutahamaki Mariam kawa maarufu.

Ngoja niliseme hili, Bakheresa angekuwa anaanza biashara nyakati hizi asingetajirika. Angekuwa anatengeneza maandazi matamu Kariakoo, halafu Shumbana wa Magomeni angekaanga maandazi ya kawaida tu. Na watu wangetoka Kigamboni, wangeyapita maandazi matamu ya Bakheresa Kariakoo na kuyafuata maandazi ya kawaida ya Shumbana.

Unajua kwa nini? Shumbana yeye angekuwa hatumii nguvu nyingi kuandaa maandazi mazuri. Ambacho angefanya ni kujivunia umbile lake la Miss Bantu. Angekuwa anajirekodi video na kuonesha umbile lake. Watu wangefunga safari kutoka Bagamoyo kuyafuata maandazi ya Shumbana, si kwa ubora wa maandazi, bali kwa mwonekano wa mkaanga maandazi.

Sasa hapo Bakheresa angetajirika vipi na maandazi yake hayanunuliwi? Angekaanga vitumbua na kwenyewe watu wangetoka Twangoma kumfuata Mwanaidi wa Kiwalani na vitumbua vyake. Hapa Bakheresa lazima ashukuru Mungu kuanza biashara miaka hiyo, intaneti ikiwa ni simulizi ya kusadikika na akili za wanaume wa Dar hazijawa hivi zilivyo. Angepata tabu sana.

Huo ni mfano kwamba hata sasa, kuna wafanyabiashara wengi wa chakula. Wanapika vizuri hakuna mfano. Hata hivyo hawaimbwi kama anavyoimbwa Mariam Biriani. Ndiyo maana Kidoti Misosi naye ameamua kuonesha umbile lake, watu wajue kwamba yaliyomo kwa Mariam na kwake yamo, hivyo waende.

Wajanja wa fursa mjini utaona wanaanza ‘scouting’ ya warembo mithili ya Mariam Biriani, halafu watatangaza “ukija kwetu utahudumiwa na warembo hawa.” Kwa vile wanaume wa siku hizi Dar akili zao ni kama zinasombwa na upepo, utawaona wanajazana. Mwenye mgahawa hatapata shida kujitangaza. Walaji wenyewe watatangaza.

Utawasikia “Twende Kinyerezi kumfuata Mariam Biriani? Mambo ya Mariam Biriani yanapatikana kwa wingi Mwananyamala.” Wafanyabiashara wenye kunadi biashara kwa ubora wa mapishi kama Shilole, wataendelea kuchakazwa vibaya.

Wanawake nao utawasikia wanajazana kwa Mariam Biriani. Si kwamba wanapenda biriani au wanampenda mpishi kama waume zao wanavyompenda. Wao wanakwenda kulinda ndoa na mapenzi yao. Wanamuona Mariam ni tishio kwao.

Hawajasahau kwamba abiria sharti achunge mzigo wake. Na wanaume nao hawapendi kwenda kwa Mariam na wanawake zao.

HAKUNA NAMNA

Mpika biriani leo anakuwa staa mjini. Amegeuka homa ya wanawake warembo hasa na wanahisi anaweza kupora waume zao. Silaha ni zile neema za Allah. Na kuna kamsemo kuwa mwanamke mwenye hizo neema, anajiamini kuliko mwanamke mrembo na msomi.

Mariam Biriani ni staa kwa sababu tupo dunia ya intaneti. Unaweza kufanya kituko Usoke leo, watu wakasambaza na ukavuma dunia nzima na kuifunika hotuba ya Donald Trump wa Marekani. Umaarufu wa intaneti ni kutrend. Na kutrend haihitaji kampeni. Watu wakivutiwa utatrend. Mariam anatrend na biriani lake kuliko Shilole na Shishi Food yake.

Usipouelewa ulimwengu wa intaneti unaweza kukondeana au ukafa kwa presha. Mambo usiyopenda yanaweza kutrend na unayotaka yasivume. Unatakiwa kuheshimu watu wanavyopokea vitu. Watu wameamua kumpokea Mariam Biriani.

Kuntrend kwenye intaneti ni mkumbo, yaani bandwagon. Basi tu watu wanazuzuka na jambo fulani, wanalihusudu. Ni kama ambavyo Pierre Liquid anavyotrend au Dk Louis Shika alivyobamba na sinema yake ya “900 Itapendeza” kwenye nyumba za Lugumi. Watu wakajikuta wanavutiwa na Shika.

Mariam riziki imemkuta kwenye pishi la biriani. Watu wanampenda. Wanapenda anavyojiinua kuonesha umbile alilojaliwa. Watu wanamfuata. Yeye anapiga hela. Binafsi sivutiwi na hii tabia ya kutangaza chakula kwa shoo ya umbo la mpishi. Nitafanyaje sasa? Uwezo wa kuzuia sina? Hata ndege za Emirates hutuonesha wahudumu warembo kama kivutio chetu ili tupande ndege zao.