Wasanii wa muziki wa kizazi kipya wabadilike, wanapotea

HADI kufika hapa ulipo muziki wa kizazi kipya, kuna watu waliohenyeka kuupigania.

Kwa wanaokumbuka muziki wa kizazi kipya ulichukuliwa sivyo ndivyo hasa kwa watu wazima. Ulionwa kama muziki wa kihuni tu na hasa namna wasanii wake walivyokuwa wakiimba na kuvaa miaka hiyo wakati ukichipukia.

Lakini juhudi kubwa zilizofanywa na waasisi wakiwemo waimbaji na watayarishaji hasa katika kuubadilisha kiasi cha kupendwa na watu wa rika lote.

Kwa leo muziki huo umeshika hatamu katika fani ya muziki ukifunika miondoko yote ikiwamo Dansi iliyokuwa imetawala miaka kadhaa ya nyuma kabla ya muziki wa kizazi kipya kuibuka.

Muziki wa kizazi kipya umeufunika hadi taarabu, ambao ulikuwa ukikimbiza kwa namna ulivyokuwa upo juu.

Kwa hakika wote walioshiriki kwa namna moja hadi nyingine kuusimamisha muziki huo kiasi cha sasa kuwa kimbilio la wengi kujipatia ajira wanastahili heshima kwao.

Heshima kubwa kwao kutoka kwa wasanii wanaoushiriki muziki huo ni kuhakikisha wanautendea haki na kuzidi kuusongesha mbele ili uzidi kupasua anga ndani na nje ya Afrika.

Lakini kwa bahati mbaya kuna baadhi ya wasanii na watayarishaji waliokuta njia imeshatengenezwa katika muziki huo kwa sasa wanataka kuurejesha kule ulipotoka.

Ndio, wasanii na watayarishaji hao ni wale wanashindana kuimba nyimbo za ovyo zenye maneno yenye ukakasi na jumbe visizo za maadili.

Kila uchao wasanii na watarishaji wmekuwa wakichuana kuimba nyimbo zenye jumbe za matusi na wakishindana kutengeneza hata video za ovyo ambazo haziwezi kusikilizwa na kuangaliwa na watu wa rika lote ma watu wenye heshima zao.

Baraza la Sanaa la Taifa limekuwa likijaribu kudhibiti nyimbo za hivyo, lakini bado halijaweza kukomesha. Wale watu wazima waliokuwa wakiupenda muziki huo wameanza kuupa kisogo.

Wamerejea kule walikokuwa wakiamini muziki huo ni wa kihuni kwa sababu ya wasanii na watayarishaji wachache wasiojua kazi kubwa iliyofanywa ili kuuinua muziki huo hadi kufikia ulipo sasa.

Mwanaspoti kama wadau wakubwa wa sanaa ya muziki inafungua kinywa na kuwakumbusha wasanii wanaotamba kwa sasa kuwa, mashabiki wao wamechoka kuimbishwa nyimbo za ovyo.

Wanapenda kusikiliza nyimbo zenye maana. Nyimbo zenye jumbe zinazoeleweka. Wamechoka kusikiliza nyimbo za matusi. Wamechoka kuziona video za utupu na wanataka muziki makini.

Wakumbuke walioupigania muziki huo na kuutengenezea njia mpaka ukakubalika mbele ya jamii hawakuwa na kazi ndogo.

Kazi waliyoifanya ilikuwa kubwa ndio maana leo wao wamekuwa na kazi nyepesi, kiasi cha kuwatajirisha na kuwa na m ajina makubwa, huku waasisi wakiishia katika lindi la umaskini.

Sio kama wanaifurahia au waliridhika na hali hiyo, bali ni kwa vile jamii haikuamini muziki wao wakati wakiupigania na walikuwa kueleweka wakati dunia imeshasonga mbele na zama zao kupita, lakini heshima na juhudi zao zikiendelea kudumu.

Tunarudia kuwakumbusha wasanii wa muziki wa kizazi kipya kuwa kama rusha roho ilichangia kuunganisha muziki wa taarabu, basi wajue wakiendelea na kuimba upuuzi nao wataanguka.

Inaweza utandawazi unawadanganya na kuwafanya waamini, watu wanafurahiwa kuimbiwa nyimbo za ovyo kwa kuiga wasanii wa mataifa mengine wanavyofanya.

Watambue kuwa, kila nchi ina mila, desturi na utamaduni wao na Tanzania nayo ina mila na tamaduni zake, hivyo ni lazima ziheshimiwe, zienziwe na kufuatwa hata kama sanaa yao inawaruhusu kuiga wenzao wa nje.

Waige mambo ambayo yatasaidia kujenga heshima na utu wa Mtanzania na sio kila upuuzi wa wenzao waulete nchini kupitia uhuru wa sanaa.

Mwanaspoti haivutiwi na wala haikubali kinachoendelea kwa baadhi ya wasanii wachache waliokijita kwenye kuimba nyimbo za matusi na kufyatua kila uchao video za nyimbo za ovyo.

Sio utamaduni wa Mtanzania na wala sanaa sio kichaka cha kuharibu kizazi kilichopo na kijacho, ndio maana tunakemee na kutaka wasanii hao wachache wajue wanachokifanya hakifurahiwi.

Wakati mwingine wanaona kama wanabanwa na serikali hususani Basata pale wanapozifungia nyimbo na video zao, lakini ukweli ni kwamba wasanii wenyewe wanalazimisha wafanyie hivyo.

Badilikeni!