NO AGENDA: Davido, wizkid wametuma ujumbe kwa bongo flevaz

Sunday February 3 2019

 

By Luqman Maloto

UINGEREZA ilikuwa inaionea gere Marekani na Hollywood yake. Mji uliokamilika kwa shughuli za sanaa na starehe. Baba wa Hollywood, Hobart Whitley, alifanya kazi ya almasi mwaka 1886, kuifanya Hollywood iwe ilivyo leo.

Karne ya 20 ilipokuwa inaelekea ukingoni, Waingereza wakaona bora watende japo nusu ya Hollywood. Ikajengwa wilaya inayoitwa The 02. Ndani yake kuna viwanja vya ndani (arena) kwa ajili ya shughuli mbalimbali, klabu za muziki, kumbi za sinema zilizo chini ya Cineworld, mabaa, migahawa. Kutaja kwa uchache.

The 02 ipo London. Ndani yake kuna 02 Arena ambayo ina matumizi mengi. Mechi za tenisi huchezwa humo. O2 Arena huingiza watu 20,000 kwa ajili ya maonesho ya muziki wa live. Unazidiwa kidogo kwa ukubwa na Manchester Arena yenye kuingiza watu 21,000.

Watu wa Ulimwengu wanatambua hakuna arena iliyo bize kwa shughuli za michezo na burudani kama Madison Square Garden, iliyopo New York, Marekani. Hufanya mapambano ya boxing, mechi za basketball, myeleka, shoo za muziki. Kuorodhesha vichache.

Taarifa ni kuwa Madison Square Garden, kwa sasa inazidiwa mishemishe na 02 Arena.

Mauzo ya tiketi kwa mwaka yamekuwa yakitoa matokeo. Kwa mujibu wa rekodi za mwaka 2017, 02 Arena iliuza tiketi 1.4 milioni, wakati Madison waligonga 1.2 milioni. Arena nyingine zikafunga tela.

Je, mpaka hapo unahitaji maelezo gani ujue 02 Arena ni kiwanja cha dunia? Uambiwe nini utambue hilo ni eneo ambalo ni ndoto ya wengi kufika na kujionea utamu wa vilivyomo? Zaidi, ni kivutio cha wanamuziki wakubwa kupiga shoo ndani yake.

TWENDE KWENYE SMS

Hujuma ya ujumbe mfupi si ndiyo mnaita SMS? Basi kuna SMS nimeipokea kutoka kwa Wizkid na Davido. Wanataka ifike kwa wanamuziki wa Bongo Fleva na mamlaka za sanaa za Tanzania. Uwaguse wadau muhimu wa muziki ambao ninyi huwakosea heshima na kuwaita mashabiki.

Oktoba 21, 2017, Wizkid alikuwa msindikizaji kwenye shoo ya rapa supastaa wa Atlanta, Georgia, Future. Shoo ilifunga watu kama kawaida ya 02 Arena. Inaachaje kujaza nyomi wakati Future ni rapa wa dunia?

Ilikuwa sehemu ya ziara ya Future, aliyoiita Hndrxx tour. Wizkid akasema, kama Future ameweza kwa nini naye asiweze. Mei 26, mwaka jana, akalipelela dude palepale 02 Arena.

Watu wakabeza, wakasema Wizkid ana msuli mdogo, asingeweza kuijaza 02 Arena japo nusu. Zingatia kuwa Wizkid ni mtoto wa Afrika, kujaza arena yenye hadhi ya kidunia, iliyopo Ulaya, tena jicho kuu la Ulaya, London, England.

Nini kilitokea? Mauzo ya tiketi yalikuwa ya kutisha. Menejimenti ya 02 Arena wakatangaza kufunga mauzo ya tiketi kabla ya siku ya onesho. Si ndiyo mnaita Sellout? Yes, Wizkid aliuza tiketi zote kabla ya siku yenyewe.

Wale wa kungoja kununua tiketi siku ya mwisho, walipewa pole zao. Onesho la Wizkid liliitwa Afrorepublik Festival. Kuna mastaa walimsindikiza. Walikuwepo Wanigeria na Waingeereza; Maleek Berry, Yxng Bane, Kojo Funds, Giggs, Tekno, Not3s, Tiwa Savage, Mr Eazi na Giggs.

Baada ya shughuli ya Wizkid, mjanja mwingine wa Nigeria, Davido akaona kama homeboy wake ameweza, yeye nini kimshinde? Akafanya kila kilichotakiwa kufanywa na hapa juzikati, ilikuwa Januari 27, mwaka huu, Davido aliifanya 02 Arena ifurike. Kama Wizkid ndivyo na Davido alivyofanya kwa shoo yake ya 02 Arena kuwa sellout kabla ya siku ya tukio. Davido ameifikia rekodi iliyowekwa na Mnigeria mwenzake, Wizkid.

NGOJA NIWATAFUNIE

Ni hivi, Wanigeria wanaandika historia. Kwa sasa hawaishii kuwa wababe Afrika, bali wanachomoza kwenye mataifa ambayo yamekuwa yakijiamini kuwa yenyewe ndiyo wazazi wa muziki na sanaa zote, michezo na kila starehe.

Kwenda Uingereza kupiga shoo ni kitu cha kawaida. Hata hivyo, kujaza 02 Arena si tukio la kuelezewa kwa maneno yenye uzani mwepesi. Wizkid na Davido wameonesha kuwa muziki wa Afrika unaweza kuishika dunia.

Kwa nini mastaa wa Marekani na Ulaya wawe wanakuja Afrika kuvuta mkwanja mrefu kwa shoo ya muda mfupi? Davido na Wizkid wamethibitisha kwamba inawezekana bila shaka yoyote vipaji vya Afrika kwenda kukusanya madola na paundi. Muhimu ni kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kuthubutu.

Ujumbe kutoka kwa Wizkid na Davido baada ya shoo zao za 02 Arena ni kuwa hawajichukulii poa tena. Wanajiona wanaweza kufanya mambo makubwa Ulaya na wamethibitisha kwa vitendo.

Mfano, mauzo ya tiketi kwa shoo ya Davido ilikuwa Pauni 40 (Sh122,000) mpaka Pauni 50 (Sh152,000), kutokana na muda wa mauzo.

Kadiri ilivyokuwa ukichelewa kununua na bei iliongezeka. Bei hiyo ni baada ya tozo. Hivyo, tiketi moja iliuzwa pauni 44 mpaka 55.

Ukichukua bei ya Pauni 40 kama kiingilio cha watu 20,000 waliohudhuria shoo ya Davido, majibu ni kwamba shoo hiyo peke yake, imeingiza zaidi ya Sh2.4 bilioni.

Na hiyo ni hesabu ya chini kabisa. Wana Bongo Fleva wachukue ujumbe huu. Waote ndoto kubwa za kufanya mambo makubwa kwenye ardhi za watu weupe. Waache majungu na kutengeneza timu zisizojenga. Wafikirie matokeo makubwa.

Muhimu zaidi ni kusaidiana, kuoneshana njia. Umeshapiga shoo sehemu fulani unampa pande na mwenzako. Umefanya mchongo unaona unalipa, muunganishe mwenzio. Davido hutembea chini ya falsafa inayoitwa: “We raise by lifting others”, yaani tunanyakuka tukiwanyanyua wengine.

Huwezi kunyanyuka ukipambana wengine wasinyanyuke. Utajikuta unatumia muda mwingi kuzuia wengine badala ya kuongeza kasi ili kufikia malengo. Kwa timu zenu wana Bongo Fleva za kutukanana mitandaoni na kujaziana dislikes au kuchawiana YouTube ili viewers wasiongezeke, hamtafika mbali. Kwanza wengine wanajiona wameshafika.