DIAMOND PLATNUMZ NI JINIAZ, MWENYE KIWANGO CHA DUNIA

Diamond Platnumz

DUNIA ilishakuwa na Aristotle. Ugiriki ya Kale ndipo alitokea. Aristotle ni moja ya zawadi zenye thamani kubwa ambazo Mungu aliipa dunia. Aliondoka miaka dahari lakini hadi leo tunaendelea kunufaila na mafundisho yake, hekima zake na ugunduzi wake.

Aristotle alikuwa mtu mwenye kipaji kikubwa mno. Alimudu mambo mengi katika nyanja tofauti. Aristotle alikuwa mwanasayansi, mwanasiasa, mwanahisabati, mwanasaikolojia na mwanajamii kwa jumla. Kote ukigusa, utaona alitisha kwa kiwango cha juu mno.

Aristotle alikuwa masta wa Biologia, Zoologia, Saikolojia, Fizikia, Metaphysics, Logic, Ethics, Rhetoric, Muziki, Mashairi, Uchumi, Siasa, Utawala na Hisabati. Huo ni muhtasari wenye kuonesha umafia wa Aristotle. Alikuwa na kichwa adimu mno.

Watu aina ya Aristotle hutokea mara chache duniani na hata wakiwepo huwa ni wa kutafuta. Jamii yoyote yenye bahati ya kuwa na majiniaz kama Aristotle, kwanza lazima ijivunie kisha iwatambue na kuwapa hadhi ambayo wanastahili.

JINIAZ DIAMOND

Diamond Platnumz ni aina ya majiniaz wa kiwango cha dunia ambao Tanzania ina bahati kuwa naye. Tofauti ya Aristotle na Diamond ni kwamba Aristotle alikuwa mahiri wa maeneo mengi ya kitaaluma, lakini Diamond yeye ni wa mambo ya mtaani na biashara.

Diamond ni msanii mwenye mafanikio makubwa. Kwa Tanzania amekuwa wa kwanza katika eneo la biashara ya muziki. Umaarufu wake kimataifa haufananishwi na yeyote kabla yake. Amekuwa mwenye bidii kubwa katika kujitangaza ndani na nje ya nchi.

Si wa kwanza kugonga kolabo na wasanii wa mataifa mengine, ila ndiye namba moja kwa kolabo nyingi daraja la kimataifa. Diamond anaongoza kugongewa hodi na wakali wa mataifa mengine wakiomba kumshirikisha kwenye nyimbo zao.

Diamond amefanikiwa kuisimamisha ngome kubwa ya muziki kutoka Tanzania kwenda duniani. Wasafi Classic Baby (WCB), hivi sasa siyo tu lebo ya muziki, bali taasisi imara ya burudani inayofunika Afrika Mashariki na inayotoa ahadi njema Afrika na duniani kote.

Nguvu ya jina la Diamond na uimara wa ngome yake ya kibiashara aliyoitengeneza, imevutia wenye pesa zao kuwekeza fedha kwa jina lake, na kwa matokeo hayo, hivi sasa Diamond ni mkurugenzi wa Wasafi TV na Wasafi FM. Hapo ni padogo?

Diamond kwa sasa ni muuza karanga mzuri, anauza pafyumu za jina lake. Na amefanikiwa kuwafanya wasanii wa lebo yake ya muziki wote kuwa mastaa. Diamond ni kielelezo cha ule msemo wa hata ukigusa shaba inageuka dhahabu. Diamond akigusa chupa inakuwa almasi.

Tuendelee; Diamond ndiye anaongoza kwa nyimbo zake au za wasanii wa lebo yake kuingia kwenye mgogoro wa kimaadili na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata). Diamond ana ujasiri usiopimika wa kuingiza kwenye nyimbo zake maneno tata yenye kutafsiriwa kama matusi. Hivi sasa lipo jipya la wimbo Mwanza wa Rayvanny akimshirikisha Diamond. Rayvanny ni msanii wa WCB.

Diamond ndio msanii wa kwanza Tanzania kumtisha Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza. Alimtolea maneno ya shombo, kisha akasema “nitakurupuka naye”, sijui alimaanisha nini? Alitoa maneno hayo baada ya kufungia nyimbo zake. Nyimbo zinafungiwa lakini hakomi.

Katika mapenzi, Diamond ni msanii anayeongoza kwa migogoro na wanawake wake. Na migogoro hiyo inakuwa kwenye uso wa vyombo vya habari. Na katika hayohayo mapenzi, imethibitika familia yake ina mamlaka makubwa kwenye maisha yake ya kimapenzi, na huweza kuamua aina ya wanawake anaokuwa nao.

Diamond ni wa kwanza kumwaibisha girlfriend wake, Wema Sepetu kwa kumgandisha ukumbini Mlimani City bila kupokea pesa alizotaka kumtuza jukwaani. Diamond akawa anaendelea kupiga shoo kama hamuoni Wema, ila wengine waliokwenda kumtuza alipokea pesa zao.

Diamond akamrekodi sauti Wema akimbembeleza kimapenzi na kuisambaza kwenye vyombo vya habari. Hicho ni kipimo kuwa Diamond pia ni mkali wa kuwashughulikia wanawake zake pindi anapoingia kwenye migogoro nao.

Alipata kuchukua video ya aliyekuwa girlfriend wake, Jokate Mwegelo, akicheza wimbo wake wa Mdogomdogo. Diamond aliiposti video hiyo Instagram na kuandika maneno “Na bado mtanyooka tu”.

Hivi sasa Diamond anaendelea kushughulika na mzazi mwenzake, Hamisa Mobeto. Shughuli siyo ndogo. Kuoneshana na kupigana vijembe. Ikumbukwe kuwa familia ya Diamond ilivujisha sauti ya Mobeto, ili kuzijengea nguvu tuhuma kwamba mrembo huyo anamuwangia Diamond. Vilevile Diamond ndiye aliuthibitishia umma kwamba mrembo huyo hupiga misele kwa vigagu.

Kuhusu suala la kutokuwa mwaminifu kwenye mapenzi Diamond sifa zake ni tele. Ndio chanzo cha kumwagana na mama wa watoto wake wawili, cheupe wa Uganda, Zari ‘The Boss Lady’. Hata yeye mwenyewe alishaimba hakomi, kwamba anafumaniwa lakini anasaliti tena.

Diamond ni mwenye wageni wengi wa kike nyumbani kwake, Madale. Nyumba ambayo aliita State House, yaani Ikulu kwa namna ambavyo aliihusudu. Zari baada ya kuona State House inakaribisha sana watoto wa kike, wanaojazana kwenye swimming pool mpaka vyumbani, akaandika Instagram: “Ati siyo State House tena ni guest house.”

Ubabe katika mapenzi? Diamond usimchezee. Wema alikuwa Marekani akiwa girlfriend wa mwanamuziki Chaz Baba. Wakati anaanza safari ya kutoka Marekani kurejea Tanzania, Wema alikuwa wa Chaz Baba. Alipofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, akikamilisha taratibu za mizigo ili atoke, Wema alikuwa wa Chaz Baba. Ila alipotokeza eneo lililoandikwa “Abiria Wanaowasili”, Wema akawa wa Diamond. Ubabe wa kiasi gani?

Diamond yupo kwenye mgogoro na aliyekuwa msimamizi wa muziki wake, Ruge Mutahaba. Ugomvi umekolea kweli. Diamond mwenye bifu na Ommy Dimpoz baada ya Ali Kiba. Wataje Q Boy Msafi na Rich Mavoko. Utaona kwamba hata katika bifu Diamond ni wa kiwango cha juu.

Kusanya mambo yote hayo na uyaweke kwenye kapu moja; kibiashara, kimuziki yupo vizuri sana. Kimapenzi, vitimbi vya mapenzi, migogoro na bifu kwenye jamii, pia yupo imara. Ni hapo unaweza kujiuliza: “Anamudu vipi yote hayo?” Ni hakika kwamba Diamond ni jiniaz wa daraja la dunia. Anamudu mambo mengi kwa ufanisi mkubwa.