Aliyemroga Marlaw Mungu anamuona

UPO wapi Marlaw? Umekuwa mgeni redioni na kwenye runinga. Wanatamba tu kina Diamond Platnumz na Alikiba. Watoto wa WCB na Kings Music ni moto. Wewe nini kimekusibu?

Ulipotoa Mbayuwayu mwaka 2012 nilikuuliza, kwa nini umetoa ngoma ambayo haibambi? Ukanijibu ile ilivuja tu kwa bahati mbaya, lakini haikuwa kwenye mipango. Kazi kubwa inafuata.

Sasa ni miaka saba tangu ulipotoa ahadi hiyo. Diamond Platnumz na Ali Kiba bado wanabamba sokoni. Wanavuka mipaka na sasa muziki wao ni tishio Afrika. Diamond amekuwa mbabe kuzidi hata Wanigeria wengi, wewe upo kimya.

Sikusikii Marlaw, umepotezwa sokoni. Wewe ndiye ulikuwa mwenyeji wa redio na runinga. Vile ukiimba kwa sauti bora na kiduku chako. Bembeleza, Rita, Bado Umenuna, Pii Pii (Missing My Baby). Ufundi wote huo umepotelea wapi?

Lawrence Marima ‘Marlaw’, hata namba ya simu ambayo tulikuwa tukiwasiliana kikazi, leo hii haipatikani tena. Naipiga tena na tena, jibu lake ni nambari ya simu unayoipiga kwa sasa haipatikani.

Kila nikiipiga inasema kwa sasa haipatikani ni mwendo wa kwa sasa haipatikani, hayo maneno ‘kwa sasa’, yananipa matumaini kuwa upo muda itapatikana.

Hata mkeo, Besta, naye hasikiki kimuziki. Hamuimbii tena Baby Boy wake ambaye alipokuwa akimuona alitabasamu. “Baby Boy napokuona natabasamu.” Au Marlaw wewe ndiye Baby Boy uliyeimbwa, kwa hiyo baada ya kukupata na kufunga ndoa, ameona hana haja tena ya kuimba?

Ndio, alikuwa anamuimbia Baby Boy na huyo Baby Boy tayari alishampata na yupo naye ndani, amuimbie mwingine nani? Najiuliza mwenyewe na kujijibu mwenyewe kwa mambo yenye kuwahusu wengine. Jawabu la uhakika sipati, basi tu ni hali ya kujifikirisha kwa yaliyo juu ya upeo. Si unajua tena akili ya kufikiria yanayoendelea kwenye nyumba za watu?

Baada ya ndoa tu na safari ya kuporomoka kwa Marlaw ikawadia. Angalau Besta yeye anaweza asizungumzwe kwa sababu hakuwahi kuongoza mkondo wa sanaa. Marlaw alikuwa kileleni kabisa.

Au baada ya ndoa mlikatazana kufanya sanaa? Wanasema wasanii ni tabaka la watu wenye wivu kwa sababu wanajua hali halisi ya kimazingira. Kwamba mwanamuziki akienda kufanya ziara ya muziki, anakuwa na uwanja mpana wa kuchepuka.

Je, Marlaw ulimkataza Besta kuimba? Je, naye alikwambia chagua kati ya ndoa na muziki? Ni wivu ndio unaowafanya mkatazane kuimba? Nini hasa ambacho kimewaingilia katikati?

Je, majukumu ya ndoa yamekuwa mazito kiasi kwamba nafasi inakosekana ya kutunga nyimbo, mashairi na sauti zake? Maana muziki ni kazi yenye kuhitaji muda wa kutosha. Huwezi kuifanya kwa uzuri wake, kama nafasi ya kutenda inakuwa finyu. Vipi hizi taarifa kuwa hata Besta haupo naye tena? Eti mmeachana! Au kuachana kwenu ndiyo sababu ya anguko lako?

Mfalme wa Kiduku Marlaw, sikutarajia kama angekuwa mpotevu wa haraka kiasi hiki. Leo hii mapromota hawawazi kuhusu kumpandisha jukwaani, maana hayupo kwenye mzunguko wa soko.

Ma-DJ hawafikirii kazi mpya ya Marlaw, kwani baada yake wametokea wasanii wengi tu wazuri. Hivi karibuni Darassa alikuwa akiuliziwa sana atoe wimbo mpya. Sioni watu wakimuulizia Marlaw. Ameshasahaulika. Besta nini kimetokea? Umemfanya nini?

Hapa hatuzungumzii suala la nyakati za kutamba, bali uwezo wa msanii na jinsi ambavyo anaweza kujirudisha sokoni hata baada ya kupotea. Hakuna mdau wa muziki nchini ambaye anaweza kuutilia shaka uwezo wa Marlaw.

Je, ni siasa ndizo zimemfanya apotee? Uchaguzi Mkuu 2010, Marlaw ndiye alikuwa msanii kinara kati ya waliotumiwa na CCM kwenye kampeni zake, hususan kumpigia debe Rais wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete, aliyekuwa akiwania kuchaguliwa kwa muhula wa pili.

Marlaw aliubadili wimbo wake Pii Pii (Misiing My Baby) na kuuwekea mashairi ya kuipigia debe CCM na Jakaya. Watu wengi walidhani kuporomoka kwa Marlaw baada ya Uchaguzi Mkuu 2010 ni sababu za kujihusisha na siasa. Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, naye aliamini hivyo, kwani alipata kuniambia.

Hata hivyo, baada ya Diamond na Ali Kiba kuendelea kutamba sokoni wakiwa wametoka kushiriki kikamilifu kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015, zilizomuingiza madarakani, Dk John Magufuli, bila shaka mtazamo unabadilika.

Baada ya uchaguzi, Diamond na Ali Kiba wameendelea kufanya sanaa yao vizuri, hivyo wale ambao waliwachukia kwa mitazamo yao ya kisiasa, wamepata mgeuko wa fikra. Wanafurahia mizigo mipya.

Sasa tukubaliane, kilichompoteza Marlaw sokoni baada ya Uchaguzi Mkuu 2010 siyo kujihusisha kwake na siasa, bali nini ambacho alikifanya baada yake.

Unapokuwa kwenye ushindani wa soko na Diamond Platnumz, lazima ufanye kazi kwa kiwango cha kupita kawaida. Ukienda kikawaida-kawaida, utashtukia Diamond yupo Mawenzi au Kibo, wakati wewe ndiyo kwanza upo Marangu unatafuta njia za kuanza kuupanda Mlima Kilimanjaro.

Kasi dawa yake ni kasi kipeo cha pili jumlisha akili kipeo cha tatu. Yaani akili na kasi jumla yake iwe kipeuo cha tano, ndipo utamuweza Diamond.

Ndiyo maana leo hii Marlaw yupo Marangu, Diamond amesimama kileleni Mlima Kilimanjaro.

Ukiniambia kipaji cha kuimba, nitakwambia Diamond hathubutu kwa Marlaw. Kama utataka jibu kuhusu kasi na akili katika muziki, nitakujibu kuwa Diamond hapimwi kwa mzani wa kupimia manyoya. Mzani wa Diamond ni ule wa makontena bandarini.

Marlaw na Alikiba walitoka wakifuatana. Marlaw akawa vizuri kiasi kwamba akatangulia kufanya live band, sasa wapi tena? Hata Kiba naye alifichwa, kilichomrudisha ni kazi nzuri na sasa yeye na Diamond wanagawana vilele vya Kibo na Mawenzi.

Nina uhakika, Marlaw akilisoma soko vizuri na kudhamiria kurejesha heshima yake, atarudi vizuri na kuwafuata Diamond na Kiba kileleni au watagawana vilele. Tena ikiwezekana atamshusha mmoja na kukaa yeye. Ila lazima awe na jumla ya akili na kasi kipeo cha tano. Vinginevyo, kama kuna mtu alimroga Marlaw, basi Mungu anamuona!