Wachezaji wa Yanga wapambane, wasiwaangushe mashabiki Taifa

Tuesday May 15 2018

 

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya soka ya kimataifa kwa ngazi za klabu, Yanga, kesho Jumatano watashuka Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kutupa karata ya pili katika mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga itaingia ikiwa wenyeji wa Rayon Sports ya Rwanda katika mechi ya Kundi D huku ikiburuza mkia wa kundi kwa kutokuwa na pointi nyuma ya Wanyarwanda hao wenye alama moja baada ya sare ya 1-1 nyumbani walipoikaribisha Gor Mahia ya Kenya.

Vijana wa Jangwani wanaikaribisha Rayon wakitokea kuchezea kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa vinara wa kundi, USM Alger katika pambano la kwanza lililochezwa Algeria na kuifanya Yanga ianze vibaya.

Hata hivyo kesho ni nafasi kwa Yanga ya kusahihisha makosa ili kujitengenezea nafasi nzuri ya kumaliza katika moja ya nafasi mbili za juu za kundi kufuzu moja kwa moja hatua ya robo fainali.

Mbali ya kutaka kujiuliza mbele ya wapinzani wao, lakini Yanga inapaswa kufanya kweli ili kuwapa faraja wanachama na mashabiki wake ambao wameishuhudia timu yao ikishindwa kutamba katika mechi saba mfululizo ilizocheza tangu kuondoka kwa Kocha George Lwandamina.

Lwandamina aliondoka ghafla kurejea kwao Zambia na kuiacha timu hiyo chini ya wasaidizi wake hali iliyoifanya klabu kumleta Kocha Mpya, Mwinyi Zahera ambaye bado hajaanza rasmi kazi kwa kinachoelezwa hana vibali vya kufanya kazi.

Katika kipindi hicho chote, Yanga imecheza mechi hizo saba na kuambulia vipigo vitano zikiwamo vitatu mfululizo katika Ligi Kuu Bara cha mwisho kikiwa ni cha juzi dhidi ya Mtibwa Sugar mjini Morogoro.

Vipigo vingine ilivyokumbana navyo katika Ligi Kuu ni vile vya Simba na Prisons, huku ikipoteza pia mechi mbili za kimataifa katika Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Wellaita Dicha ya Ethiopia na USM Alger.

Mechi zao mbili walizonusurika kulala ni zile za Singida United waliofungana bao 1-1 na ile ya Mbeya City iliyomalizika pia kwa sare kama hiyo.

Jambo hilo la kushindwa kupata ushindi katika mechi mfululizo, si tu zimewanyima furaha wanachama na mashabiki wa Yanga, lakini pia zimeiponza timu hiyo kupoteza taji la Ligi Kuu Bara mbele ya Simba iliyonyakua taji mapema.

Kutokana na hali ilivyo, ni wazi nyota wa Yanga wana kazi kubwa ya kuwapa furaha wanachama na mashabiki wao kwa kuhakikisha kesho wanainyoosha Rayon.

Hakuna asiyejua faida ya kucheza nyumbani, japo soka huwa na matokeo ya kushangaza wakati mwingine bila kujali timu inacheza wapi.

Yanga itakuwa kwenye uwanja wenye uwezo wa kuingiza mashabiki wake wengi, ambao uwepo wao ni sawa na mchezaji wa nyongeza kwa Watoto wa Jangwani.

Licha ya kufahamika kuwa ndani ya Yanga hali si nzuri kiuchumi na wachezaji wamepoteza morali, lakini bado ni nafasi yao kuonyesha kujali na kuithamini jezi na nembo ya klabu hiyo sambamba na heshima ya bendera ya Taifa wanayoipeperusha.

Tunawasisitiza wachezaji wa Yanga kuweka kando matatizo yao kwa muda na kuelekeza nguvu katika mchezo huo, ili kuhakikisha wanashinda kujiweka pazuri kabla ya kumalizia mechi nne za mwisho.

Kama wataruhusu kupoteza mchezo huo wa nyumbani mbele ya Rayon, wachezaji wa Yanga lazima wajue wataiweka timu yao pabaya zaidi katika mbio zao za kutaka kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kutinga robo fainali ya michuano hiyo.

Ni kweli Yanga ilishawahi kufika robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa kwa miaka miwili mfululizo, 1969 na 1970 pia kufanya hivyo katika Kombe la Washindi mwaka 1995 kabla ya michuano hiyo haijaunganishwa na Kombe la CAF na kuzaliwa kwa Kombe la Shirikisho la Afrika la sasa.

Hata hivyo Yanga bado inapaswa kuwania rekodi mpya kama inavyoshiriki kwa sasa ya kuwa klabu pekee ya Tanzania kushiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza mwaka 2016 kabla ya kurudia tena mwaka huu ikiwa ni rekodi mpya.

Hivyo basi wachezaji wa Yanga pamoja na makocha wake washuke uwanjani kuivaa Rayon wakitambua wana kazi kubwa.

Tunaamini kila kitu katika soka kinawezekana ili mradi mipango na maandalizi mazuri sambamba na dhamira ya dhati watakayokuwa nayo wachezaji kwa kujituma kwa nidhamu uwanjani na kuepuka makosa yanayoweza kuwagharimu.

Kazi kwenu sasa!