Zile tano Ozil hakuwepo mjue

Friday October 12 2018

 

ENGLAND. KUMBUKA wakati Arsenal anapiga mtu 5-1 kwenye Ligi Kuu England Jumapili iliyopita, supastaa wao Mesut Ozil hakuwapo uwanjani.
Basi kwa taarifa yenu tu, Ozil amepona na atakuwapo uwanjani kwenye mechi ijayo ya ligi hiyo, ambapo wababe hao wa Emirates wanaonolewa na Unai Emery watashuka uwanjani kukipiga na Leicester City.
Mechi iliyopita ya ushindi wa Bao Tano, Arsenal walikuwa ugenini kwa Fulham huko Craven Cottage na kitu kizuri ni kwamba ulikuwa ushindi wa tisa mfululizo kwa timu hiyo katika michuano yote ya msimu huu.
Kwenye Ligi Kuu England, baada ya kupoteza mechi mbili za mwanzo dhidi ya Manchester City na Chelsea, Arsenal wameliamsha dude na kuchapa timu zote sita zilizofuatia ambazo zilikumbana na timu hiyo kwenye ligi. Na sasa baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa itakuwa zamu ya Leicester City kupewa dozi yake.
Ozil alionekana akifanya mazoezi na wenzake, Hector Bellerin na Alexandre Lacazette Jumanne na hakuonekana kuwa na tatizo lolote, hivyo atakuwa na muda mwingi wa kupumziko kabla ya kufikia siku hiyo ya kuwakabili Leicester City. Habari njema kwa Washika Bunduki hao kwamba mechi hiyo itapigwa Emirates. Hata hivyo, taarifa za kutoka ndani ya Arsenal ni kwamba Ozil atalazimika kugombea namba na Henrikh Mkhitaryan na Alex Iwobi ili kuanzishwa kwenye mechi hiyo kwa sababu kwa Emery hakuna mwenye namba yake.

Advertisement