Breaking News
 

Zidane ataja wachezaji wake akitua Man United

Monday September 10 2018

 

HABARI ndio hiyo. Zinedine Zidane ameshaorodhesha majina ya wachezaji ambao atawasajili atakapotua Manchester United kama atapewa kibarua hicho kinachoshikiliwa na Jose Mourinho kwa sasa.

Kocha huyo wa zamani wa Real Madrid, Zidane amewaambia marafiki zake anatarajia kupokea simu kutoka kwa mabosi wa Old Trafford baada ya fukuto kubwa linaloikabili timu hiyo chini ya Kocha Mourinho.

Licha ya Makamu Mwenyekiti wa Man United, Ed Woodward kusisitiza Mourinho bado atapewa nafasi ya kuendelea kuinoa timu hiyo, Zidane mwenyewe amejiweka kwenye mkao wa kula akisubiri kibarua hicho kama kutakuwa na mabadiliko.

Katika kuhakikisha Man United itakuwa matata chini yake, Zidane tayari ameweka bayana majina ya wachezaji ambao atahitaji watue Old Trafford kuifanya timu hiyo kuwa tishio uwanjani.

Wachezaji waliopo kwenye orodha hiyo ya Zidane ni Toni Kroos, Thiago Alcantara, James Rodriguez na straika Edinson Cavani.

Zidane ndoto zake kwa sasa ni kuinoa klabu ya Ligi Kuu England na anasubiri kuona jambo hilo linafanikiwa kwa kutua Old Trafford.

Mabosi wa Man United wanafahamu wazi Mfaransa huyo anapatikana kwa sasa baada ya kuachana na Real Madrid mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kuipa mataji matatu mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kwa sasa hana kazi.

Kocha Mourinho kwa sasa anachopaswa kukifanya ni kuhakikisha Man United haipotezi tena mechi huko kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akipangwa kwenye kundi lenye changamoto linaloundwa na timu kali za Juventus na Valencia.

Advertisement