Waturuki wamtaka Ozil wao nyumbani

Thursday September 13 2018

 

SI unakumbuka sakata la Mesut Ozil kuhusiana na Uturuki kabla ya fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Russia lilivyokuwa?

Basi wababe wa Uturuki, Fenerbahce wameripotiwa kuwa na mpango wa kwenda kupiga hodi huko Arsenal kwenye dirisha la usajili wa Januari ili kumchukua kiungo huyo kumrudisha nyumbani kwenye asili yake, staa huyo aliyeamua kuitumikia Ujerumani kwenye soka la kimataifa.

Ozil alitangaza kuachana na Timu ya Taifa ya Ujerumani, mwenyewe akidai kuna sababu za kibaguzi, jambo ambalo limepingwa vikali na wachezaji wengine wa timu hiyo ya Taifa ya Ujerumani.

Picha aliyopiga Ozil na kiongozi wa Uturuki kabla ya fainali hizo za Uturuki ilidaiwa kuibua utata mkubwa. Lakini, kuhusu kupata huduma yake, Fenerbahce itabidi ipambane sana kwa sababu Ozil ana mkataba na Arsenal hadi mwisho wa msimu wa 2020-21. Ripoti za kutoka Emirates zinadai Ozil hayupo kwenye wakati mzuri na Kocha Unai Emery, hivyo jambo hilo linamfanya afikirie kuachana na timu hiyo na kutimkia kwingineko wakati dirisha lijalo la usajili litakapofunguliwa.

Ozil amekuwa kwenye Ligi Kuu England tangu mwaka 2013 aliponaswa kutoka Real Madrid.

Advertisement