Van Persie bado anashikilia rekodi ya Wadachi England

Muktasari:

  • WANASOKA wa Kidachi siku zote wamekuwa wakileta mambo matamu kwenye Ligi Kuu England na kuacha kumbukumbu za kipekee kwenye michuano hiyo tangu ilipoanza mwaka 1992.
  • Rekodi tamu walioacha Wadachi kwenye michuano hiyo ni uwezo wao wa kupasia nyavu na kutokana na hilo hawa hapa ndio mastaa wanaoongoza kwa kufunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu England.

WANASOKA wa Kidachi siku zote wamekuwa wakileta mambo matamu kwenye Ligi Kuu England na kuacha kumbukumbu za kipekee kwenye michuano hiyo tangu ilipoanza mwaka 1992.

Rekodi tamu walizoziacha Wadachi kwenye michuano hiyo ni uwezo wao wa kupasia nyavu na kutokana na hilo hawa hapa ndio mastaa wanaoongoza kwa kufunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu England.

6.Marc Overmars - mabao 25

Winga mwenye kasi iliyowatesa mabeki kwenye Ligi Kuu England, Marc Overmars hakika huduma yake haiwezi kusahaulika huko Arsenal.

Msimu wake wa kwanza alipotua kwenye timu hiyo, alifunga mabao 12, likiwamo bao lake alilofunga Old Trafford nyumbani kwa Manchester United katika msimu wa 1997/98, ambapo Arsenal ilikuwa moto kweli kweli ndani ya uwanja. Bao hilo lilikuwa muhimu kwa mashabiki wa Arsenal kwa sababu Man United ndio waliokuwa wakishindana kwenye mbio za ubingwa. Winga huyo alitumikia Arsenal kwa miaka mitatu kabla ya kwenda kujiunga zake Barcelona kwa ada ya Pauni 25 milioni mwaka 2000.

5.Dirk Kuyt - mabao 51

Dirk Kuyt alitua Liverpool mwaka 2006 akiwa ametokea kufunga mabao 91 kwenye mechi za ligi kwa misimu minne, akiwa Anfield, staa huyo alikuwa akitumika kama kiungo wa kulia.

Halikuwa eneo lake bora kabisa la kufunga mabao. Hata hivyo, kwa Kuyt hakikuwa kitu kigumu kuendelea kutupia mipira kwenye nyavu za wapinzani, kwani alifunga mabao 51 kwenye Ligi Kuu England ikiwamo ile hat-trick yake dhidi ya mahasimu wakuu wa Liverpool, Manchester United mwaka 2011.

Kuyt alikuwa mchezaji mahiri kweli kweli kwenye kikosi cha Liverpool akiwa mtu muhimu kwenye mechi ngumu zile za kibabe kutokana na soka la staa huyo.

4. Dennis Bergkamp - mabao 87

Dennis Bergkamp anabaki kuwa mmoja kati ya wachezaji wa kigeni wenye vipaji vikubwa sana waliowahi kutokea kwenye Ligi Kuu England.

Alijiunga na Arsenal akitokea Inter Milan mwaka 1995 na kipindi hicho wachezaji wasiokuwa Waingereza ilikuwa shida kucheza kwenye soka la nchi hiyo. Licha ya kwamba anakumbukwa kwa uwezo wake wa kufunga mabao kwenye ligi hiyo, Mdachi huyo alionyesha kuwa ni moto katika misimu yake minne ya kwanza kwa sababu alikuwa akifunga mabao yanayoanzia tarakimu mbili. Alikuwa moto hadi pale alipokuja, Thierry Henry ndipo alipopunguza kasi yake ya kufunga kwa sababu alikuwa akifanya kazi ya kumtengenezea mabao fowadi huyo wa Kifaransa.

3.Ruud van Nistelrooy - mabao 95

Ruud van Nistelrooy wakati anahamia kwenye kikosi cha Manchester United mambo yalibaki kidogo tu yaharibike baada ya kupata maumivu mabaya ya goti ambayo yalitishia kumaliza maisha yake ya kisoka.

Lakini bahati njema zilitokea na hatimaye, straika huyo wa Kidachi akakamilisha uhamisho wake kutoka PSV Eindhoven na kutua Old Trafford kuungana na timu pekee aliyoichezea kwenye Ligi Kuu England. Van Nistelrooy alifunga mabao mawili katika mechi yake ya kwanza kwenye ligi hiyo, kisha akafunga mabao yanayoanzia 20 na kuendelea kwa misimu minne kati ya mitano aliyodumu kwenye ligi hiyo. Alishindwa kufanya hivyo kwenye msimu wa 2004/05 kwa sababu alikuwa majeruhi.

2.Jimmy Floyd Hasselbaink - mabao 127

Jimmy Floyd Hasselbaink alishinda mara mbili Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England, alishinda mara ya kwanza kwa ‘kushea’, katika msimu wake wa kwanza England akiwa na kikosi cha Leeds United 1998/99 kisha kushinda tena akiwa na wababe wa Stamford Bridge, Chelsea. Kwenye kikosi hicho cha The Blues, Jimmy alifunga mabao 70 ya Ligi Kuu kwa misimu minne kabla ya kutimkia zake Middlesbrough mwaka 2004. Aliwahi kuichezea pia Charlton Athletic.

1.Robin van Persie - mabao 144

Robin van Persie alikuwa na umri mdogo wakati anaanzishwa katika fainali ya Kombe la Uefa mwaka 2002 akiwa na kikosi cha Feyenoord.

Lakini miaka miwili baadaye alikwenda kujiunga na Arsenal na hapo mambo yake matamu yakaanza. Mwanzoni alisumbuliwa sana na majeraha, hadi hapo alipoanza kuonyesha makali yake kwenye msimu wa 2010/11. Msimu uliofuatia akafunga mabao 30 kwenye Ligi Kuu England akiwa na Arsenal kabla ya kuhamia Manchester United alikokwenda kufunga mabao 26 katika msimu wake wa kwanza na kunyakua ubingwa.

Van Persie ameondoka kwenye ligi akiwa amefunga mabao 144.