Usiyempenda huyoo kaja!

NYON, USWISI,

WANAUME nane wametinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na leo Ijumaa pale Jiji la Nyon Uswisi watajua nani atacheza na nani katika hatua nusu fainali.

Pale England, timu zote nne za England zimetinga hatua ya robo fainali. Liverpool, Tottenham, Manchester United na Manchester City. Hii ni mara ya kwanza kwa timu zote nne za England kutinga robo fainali tangu walipofanya hivyo kwa mara ya mwisho msimu wa 2008-09.

Kule Hispania amekwenda Barcelona peke yake baada ya Real Madrid kupoteza ubingwa ilioutwaa mara tatu mfululizo chini ya kocha, Zinedine Zidane huku Atletico Madrid ikitolewa na Juventus licha ya kuongoza kwa mabao 2-0 katika pambano la kwanza.

Halafu Cristiano Ronaldo na Juventus yake imetinga hatua hiyo baada ya kupiga shoo ya kibabe dhidi ya Atletico. Lakini pia timu mbili za Ajax kutoka Uholanzi na Porto ya Ureno ambazo zilikuwa zinaonekana vibonde zimefanikiwa kuingia kundi moja na wababe.

Na leo mchana pale Uswisi mechi za robo fainali zitajulikana na katika hatua hii hakutakuwa na timu kubwa wala ndogo badala yake yoyote anaweza kupangwa na yoyote bila ya kujali chochote. Ni tofauti na hatua za makundi au hatua ya mtoano iliyopita.

Wakati huo huo timu za nchi moja zinaweza kupangwa katika pambano moja na hii ina maana Manchester United inaweza kucheza na Manchester City, au Liverpool ikacheza na Tottenham au Manchester United ikacheza na Liverpool.

Baada ya kupangwa kwa mechi za robo fainali, wapangaji watapanga pia ratiba ya nusu fainali ambapo tayari itajulikana timu zipi zina uwezekano wa kukutana na timu zipi katika hatua ya nusu endapo zitafanikiwa kusonga mbele.

Mechi za kwanza za robo fainali zitachezwa Aprili 9 na 10 na mechi za marudiano zitachezwa Aprili 16 na 17. Mechi za nusu fainali za kwanza zitachezwa April 30 na Mei Mosi. Wakati mechi za marudiano za nusu fainali zitachezwa Mei 7 na 8.

Pambano la fainali linatazamiwa kupigwa katika Uwanja wa Wanda Metropolitano mnamo Juni Mosi. Uwanja huu ni wa klabu ya Atletico Madrid ambayo imekosa fursa ya kucheza pambano la fainali baada ya kung’olewa katika michuano hiyo na Juventus.

Kuelekea katika ratiba hii ya robo fainali ni wazi timu za England zitatamani zaidi kupangwa na timu za Ajax na Porto ambazo zinaonekana kuwa vibonde katika hatua hii ingawa Ajax waliwashangaza mashabiki wengi wa soka kwa kuwavua Real Madrid ubingwa wa Ulaya katika uwanja wao wa nyumbani wa Santiago Bernabeu. Timu hizo za England pia zitapenda kuepuka kucheza wenyewe kwa wenyewe huku pia zikiepuka kupangwa na Juventus na Barcelona ambazo zinaongozwa na wakali wawili wa soka duniani kwa sasa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Juventus na Barcelona pia zitapenda kupangwa na Porto na Ajax huku zikiepuka kupangwa na timu za England pamoja pia kuepuka kupangwa wenyewe kwa wenyewe katika pambano ambalo kama likitokea basi mastaa Messi na Ronaldo wanaweza kukutana kwa mara ya kwanza uwanjani tangu Ronaldo alipohamia Italia kwa dau la Pauni 88 milioni katika usajili wa dirisha kubwa la majira ya joto mwaka jana Juve ilipomnasa.