#WC2018: Rekodi 6 za kuvutia timu za Afrika Kombe la Dunia

Muktasari:

Lakini ukiachana na hayo kwa timu za Afrika, itabakia kuwa ndoto kufika fainali. Pengine ndoto itakayodumu milele.

KOMBE la Dunia 2018 lilimalizika rasmi usiku wa Jumapili naa Ufaransa kutwaa ubingwa kwa mara ya pili (mara ya kwanza ikiwa 1998)/ Mcroatia alijiwekea historia ya kufika fainali kwa mara ya kwanza. Kabla ya hapo hakuwa amefuzu zaidi ya nusu fainali.

Lakini ukiachana na hayo kwa timu za Afrika, itabakia kuwa ndoto kufika fainali. Pengine ndoto itakayodumu milele.

Na huku sasa Bara Afrika likisubiri hadi 2022 kujaribu bahati kwa mara ya nyingine tena,  hizi hapa ndio rekodi za kukumbukwa zilizoachwa na timu za Afrika 2018 kule Moscow, Urusi.

Kwa mara ya kwanza Afrika yakosa 16 Bora

Kwa mara ya kwanza tangu 1982 Afrika ilikosa mwakilishi  kwenye raundi ya 16 katika shindano la Kombe la Dunia.

Timu tano za Afrika zote kwa mpigo zilishindwa kufuzu kwa hatua ya 16 bora, zilinyofolewa kwenye hatua ya makundi.

Misri waliorejea kwenye Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya kushindwa kufuzu katika kipindi cha miaka 28, walipoteza mechi zao zote.

 

Nigeria kikosi kichanga zaidi

Nigeria waliweka rekodi ya kipekee kule Moscow kwa kuwa  kikosi cha pekee chenye wachezaji wachanga zaidi.

Super Eagles waliwashirikisha wachezaji 18 wenye umri wa chini ya miaka 25 huku mchanga zaidi akiwa kipa wao mwenye miaka 19.

Lakini hata zaidi wachezaji wote hao 18 walikuwa wakishiriki kombe la dunia kwa mara ya kwanza.

 

Tunisia wafungaji bora

Licha ya Senegal na Nigeria kuonyesha mchezo mzuri zaidi kwa timu zote tano za Bara Afrika zilizotuwakilisha kule Moscow, hakuna iliyofanikiwa kufunga magoli mengi kulimko Tunisia.

Tunisia waliyaaga mashindano hayo  kama wafungaji bora wa timu za Afrika kwa kufunga jumla ya mabao matano kutokana na mechi tatu.

 

Makocha wawili Wafrika

Kwa timu zote 32 zilizoshiriki Kombe la Dunia 2018, makocha wote walikuwa wa kizungu isipokuwa wawili pekee Aliou Cisse na Nabil Maaloul.

Maaloul aliyejiuzulu wadhifa wake hivi karibuni na Cisse beki kisiki wa zamani wa Senegal, ndio makocha pekee wa Kiafrika miongoni mwa 32 waliokuwa Moscow.

Hata nazo timu zingine za Afrika Nigeria, Morocco na Misri makocha wao walikuwa wa Kizungu.

Misri walikuwa na Mwargentina Hector Cuper aliyetimuliwa baada ya shindano, Nigeria, Mjerumani Gernot Rohr, Morocco na Mfaransa Herve Renard.

 

Mchezaji mkongwe zaidi atoka Afrika

Ukiachana na suala la kuwa Afrika ndio iliyokuwa na kikosi kichanga zaidi ikiwakilishwa na Nigeria, vilevile Bara ndiyo iliyokuwa na mchezaji mkongwe zaidi kushiriki kombe hilo la dunia.

Kipa wa Misri Essam El-Hadary aliweka rekodi  mpya ya kuwa mchezaji mkongwe zaidi kuwahi kushiriki Kombe  la Dunia.

El-Hadary alishiriki dimba hilo akiwa na miaka 45 hivyo kuweka historia mpya. Lakini hata zaidi hii ilikuwa ndio mara yake ya kwanza kushiriki Kombe la Dunia.

Kwa kushiriki, El-Hadary aliifuta rekodi ya kipa wa Colombia Faryd Mondragon aliyekuwa na umri wa miaka 43 alipoiwakilisha taifa lake kwenye Kombe la Dunia la kule Brazil miaka minne iliyopita.

Kipa huyo wa Misri kiumri aliwazidi makocha watatu waliokuwepo Moscow. Kocha wa Senegal Aliou Cisse mwenye miaka 42, kocha wa Serbia Mladen Krstajic (44) na kocha wa Ubelgiji Robert Martinez (44).

 

Morocco yawakilishwa na wachezaji wa Kizungu

Huku mataifa kama Ubelgiji na Ufaransa yakiwakilishwa na wachezaji ambao uhalisia wa asili yao ni Afrika, Morocco ilikuwa kinyume.

Licha ya kuwa timu ya Afrika,  kikosi cha Morocco asilimia 90% ya kikosi chake kiliundwa na wachezaji wasio wazalendo.

Kati ya wachezaji 23 waliounda timu hiyo, 17 hawakuwa wazawa wa Afrika.  Wachezaji hao 17 walizaliwa nje ya Bara Afrika kule uzunguni hivyo kuwapa uhuru wa kuwa na uraia wa mataifa mawili.