Advertisement

Ramos anaposomesha mastraika wetu kijanja

MASHABIKI wa Liverpool bado wana hasira na Sergio Ramos. Hata Wamisri, huenda hawataki kulisikia jina hilo hata kidogo. Beki na nahodha huyo wa Real Madrid alijitengenezea uadui mkubwa, kwa tukio lake la Mei 26 pale kwenye Uwanja wa NSC Olimpiyskiy, mjini Kiev.

 

BY BADRU KIMWAGA

IN SUMMARY

Siku hiyo ndiyo iliyopigwa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2018, Liverpool na Real Madrid walikuwa wakihitimisha mbio nzima za michuano hiyo kwa msimu uliopita.

Advertisement

MASHABIKI wa Liverpool bado wana hasira na Sergio Ramos. Hata Wamisri, huenda hawataki kulisikia jina hilo hata kidogo. Beki na nahodha huyo wa Real Madrid alijitengenezea uadui mkubwa, kwa tukio lake la Mei 26 pale kwenye Uwanja wa NSC Olimpiyskiy, mjini Kiev.

Siku hiyo ndiyo iliyopigwa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2018, Liverpool na Real Madrid walikuwa wakihitimisha mbio nzima za michuano hiyo kwa msimu uliopita.

Liverpool iliyokuwa ikipigiwa chapuo kutokana na rekodi iliyowekwa kwenye mechi zao kabla ya kufika fainali, ilikufa kwa mabao 3-1.

Kabali ya kihuni ya mkono ambayo beki huyo alimpiga MO Salah na kumfanya aende kuanguka na kujiumiza bega, liliwatia hasira mashabiki wa Liverpool na Wamisri kuliko hata kipigo chenyewe cha mabao ya Karim Benzema na mawili Gareth Bale.

Ramos alifanya uhuni ule ili kuthibitisha kuwa yeye ni beki anayejua kuwadhibiti mastraika wasumbufu. Ndivyo beki anavyotakiwa. Hapa kwetu kuna wakati tunawalalamikia na kuwatukana kina Kelvin Yondani ama Aggrey Morris au Juma Said ‘Nyosso’ kwamba ni wakorofi. Hapana, sio wakorofi ila beki wa kweli hawezi kuwa laini laini na roho nyepesi hata ya kuogopa kuchinja kuku. Wakati mwingine beki anatakiwa kuwa na roho ngumu. Bakar Malima aliwahi kumfanyia kitu kibaya, Dua Said mashabiki wakataharuki. Lakini Jembe Ulaya alikuwa akitimiza tu wajibu wake.

Ramos alijua kabisa Salah ndiye roho ya Liverpool na huifanya timu yake itishe hasa akicheza sambamba na Sadio Mane na Roberto Firmino. Akaona ngoja kwanza amalizane na huyu mmoja, kisha atajua cha kufanya kwa wengine.

Hivyo Salah alitumia dakika 31 tu uwanjani na kuiacha mechi ya fainali ikichezwa na wenzake, huku yeye akiwa benchi akiugulia kwa maumivu na pia kwa kipigo ambacho timu yake ilichokutana nacho mbele ya The Blancos.

Salah aliumia zaidi kwa kubaini zilikuwa zimebaki siku chache kabla ya Fainali za Kombe la Dunia pale Russia. Japo madaktari wa Misri walipambana na jamaa kurudia uwanjani mapema, lakini hakuwa na makali ya kutisha, ndio maana Misri ilikuwa ya kwanza kuaga michuano hiyo bila hata pointi, japo Salah alifunga mabao matatu.

Ramos ana rekodi ya kulimwa kadi 173 zikiwamo nyekundu 19, huku akishikilia rekodi ya mchezaji wa timu ya taifa ya Hispania aliyelimwa kadi nyingi, mbali na kuvuna za kutosha pia katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hata hivyo kama walivyosema wahenga, kila mwenye mabaya na zuri hakosi. Ramos ana rekodi tamu za ufungaji mabao, pengine kuliko hata baadhi ya mastraika wetu wa klabu za Ligi Kuu Bara.

Advertisement

Ndio, wiki mbili zilizopita tu wakati Real ikipata ushindi wa mabao 4-1 ugenini dhidi ya Girona aliweke rekodi ya kufunga kwa misimu 15 mfululizo. Straika gani mwenye rekodi ya kufunga mfululizo nchini ukimuondoa John Bocco ‘Adebayor’?

Tena Bocco rekodi yake ni ya misimu 10 tu, lakini ni angalau anaweza kutembea kifua mbele kujivunia kwani mabao yake 98 alitotupia kambani sio haba. Kazi ya mshambuliaji ni kufunga, lakini Ramos ni beki ila hiyo rekodi yake ni darasa tosha kwa mastraika wetu. Mastraika wanaofunga bao na kuanza kupiga kelele kwenye vyombo vya habari, kisha anapotea mazima.

Beki huyo baada ya kuzindua msimu kwa bao moja dhidi ya Girona, alirudia tena Jumapili iliyopita wakati The Blancos wakipata ushindi mwingine mnono dhidi ya Leganes. Alifunga bao kwa mkwaju wa penalti na kumfanya afikishe bao la 57 katika mechi 434 ya La Liga.

Wala hujakosea! Hilo lilikuwa bao lake la 57 katika La Liga, pia ni la 79 katika historia yake ya uchezaji soka kwa ngazi ya klabu tangu 2003-04 katika jumla ya mechi 619.

Katika misimu yake 16 ya kucheza La Liga ni msimu wake wa kwanza tu wa 2003-04 ndio hakufunga kipindi hicho akiwa Sevilla, lakini msimu uliofuata wa 2004-05 alifanya mambo na kuendelea mpaka sasa 2018-19 akiwa ameshafunga mawili.

Ramos amekuwa akilinda lango la timu yake kwa kila aina ya mbinu ili tu lisiguswe, lakini pia akiifungia mabao muhimu. Amekuwa mtu wa kuamua matokeo hata katika mechi ngumu. Ufanyaji kazi wake uwanjani ni darasa tosha kwa nyota wetu.

Ndivyo beki anavyotakiwa kucheza, lakini pia wakati mwingine kujitoa kwa ajili ya timu yake. Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kabla ya kustaafu na Aggrey Morris ni aina ya uchezaji wa Ramos hata kama wameachwa mbali sana na Mhispania huyo.

Lakini jinsi Ramos anavyojitoa kuibeba timu na kuifungia mabao muhimu ni somo kwa washambuliaji wa soka nchini hasa wa klabu za Ligi Kuu Bara.

Ni aibu kubwa kwa mshambuliaji anayetegemewa na timu katika kuipa matokeo anamaliza dakika 90 bila hata bao la kuotea! Mchezaji anajisikiaje kuitwa straika, huku msimu mzima wenye mechi zaidi ya 200 ukiisha akiwa hana lolote! Sawa wakati mwingine hukwamishwa na kuwa majeruhi, kukamiwa na hata kuwekwa benchi tu na makocha wao, lakini straika unashindwa kufunga wakati hiyo ndio kazi yako.

Meddie Kagere na Heritier Makambo wamekuja juzi tu, lakini tayari kasi yao ya ufungaji inathibitisha kuwa kweli wao ni washambuliaji, kama ilivyokuwa kwa Amissi Tambwe, Emmanuel Okwi, Donald Ngoma, Kipre Tchetche ama Obrey Chirwa! Hapo ndipo nalazimika kuwakumbusha wamuangalie Sergio Ramos na kazi anayoifanya kama beki, lakini pia wamuangalie anavyowasomesha kijanja katika ufundi wa kutupia kila msimu, kisha nao waanze kuchangamka sasa!

More From Mwanaspoti
Advertisement
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept