Nyota watano hawa hapa kumrithi Ronaldo

Wednesday July 11 2018

 

KABLA ya Ujio wa Cristiano Ronaldo, Real Madrid ilikuwa na mastaa wengi tu. Ndio wengi wamekuja na kupita.

Ronaldo de Lima, Kaka, Zinedine Zidane, Luis Figo, Raul Gonzalez, David Beckham, Pavon, Roberto Carlos, Fernando Morientes na Steve McManaman, wote walikuja Santiago Bernabeu wakaondoka.

Kama daladala, Los Blancos imekuwa na kawaida ya kuleta Galacticos mpya kila mwaka. Pesa za Fiorentino Perez hazijawahi kushindwa. Sera yao ni kikitoka kitu, kinaingia kitu na baada ya Cristiano Ronaldo kutimkia Juventus, tayari rada ya Perez inatafuta Galactico mwingine.

Sokoni kuna wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa sana. Kuna wachezaji wenye thamani kubwa sana na hapa Mwanaspoti inakulekea orodha ya nyota watano wenye nafasi kubwa ya kuvaa viatu vya Cristiano Ronaldo ndani ya kikosi cha Julen Lopetegui.

 

EDEN HAZARD

Kama kuna mtu anayeonekana kuelekea Santiago Bernabeu ni kuingo wa Chelsea, Eden Hazars. Taarifa zinaonesha kuwa, Perez ni shabiki mkubwa wa Mbelgiji na zaidi ya mara moja, amejitahidi kupata saini ya nyota huyu bila mafanikio.

Kabla ya mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia, dhidi ya Ufaransa, ikiwa ni saa chache kabla Juventus hawajamtangaza Ronaldo kama mchezaji wao, Hazard alinukuliwa akisema ndoto ya kuichezea Real Madrid ni ndoto ya kila mchezaji. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa kiungo huyo kuzungumza ishu hiyo.

Hazard ni hadhi ya kuitwa Galactico. Ana hamu ya kutwaa ligi ya mabingwa. Uwezo wa kufanya hivyo anao, ila anahitaji tu kuwa sehemu sahihi. Hakuna klabu inayoweza kumpa uhakika huo kama Real Madrid. Akiwa amebakisha miaka miwili tu katika kandarasi yake, ni dhahiri kuwa, safari ya kuondoka Stamford Bridge, imeiva.

 

NEYMAR

Uhamisho wa Neymar kwenda PSG uliushtua ulimwengu wa soka na kubadilisha historia ya mchezo huo. Kila mtu hakuamini kama Neymar angeondoka Barcelona lakini pili, hakuna aliyejiandaa kukubali Paris Saint-Germain wangetoa pauni milioni 222 kwa ajili ya saini ya bwana mdogo huyu.

Kwa kuwa soka ni mchezo wa maajabu na mikasa, Dunia inajiandaa tena kushuhudia maajabu mwengine. Tayari Ronaldo na Juventus wameshafanya yao. Sasa ni muda wa Perez naye kufanya yake. Sijui itakuaje lakini habari zilizopo ni kwamba, Real Madrid wanamtaka Neymar.

 

KYLIAN MBAPPE

Huyu wala hata hahitaji maelezo mengi. Anachokifanya huko Russia kinatosha kumuelezea. Akiwa na umri wa miaka 19, anaingiza mkwanja wa kutosha tu, kwa hiyo pesa kwake sio tatizo. Amevunja rekodi ya David Trezeguet, hana mashaka tena.

Amevunja rekodi iliyowekwa na Pele miaka 60 iliyopita kwenye Kombe la Dunia 1958. Mungu ampe nini tena. Kilichobaki ni kubeba ndoo ya Champions League na Kombe la Dunia ambalo hata hivyo anakaribia kulichukua. Sasa hivi, anahitaji heshima. Anatamani kukaa meza na Galacticos.

 

HARRY KANE

Anaongoza kwa kufumania nyavu huko Russia. Ametupia wavuni mara sita. Kwenye EPL hakamatiki. Mashabiki wa Tottenham wanamuona kama 'mungu' wa White Hart Lane. Nahodha wa England, Harry Kane hana mpinzani katika kufukuzia kiatu cha Ronaldo pale Santiago Bernabue. kwanza bado ni mdogo.

ROBERT LEWANDOWSKI

Straika wa Bayern Munich, Robert Lewandowski ni mmoja wa mastraika hatari wanaoishi katika ulimwengu huu wa soka. Licha ya kushindwa kutamba huko Russia na Poland yake, ni kosa kabisa kumbeza uwezo wake. Perez anampenda, mashabiki wa Los Blancos wanamfagilia, kwanini asiende kwa mfano?

Advertisement